Na Janeth Raphael - MichuziTv
Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) inatarajia kuanza kutoa huduma za upasuaji mkubwa wa saratani kuanzia Oktoba mwaka huu, hatua inayolenga kuongeza wigo wa huduma za kibingwa nchini na kupunguza changamoto ya wagonjwa kusafiri kutafuta huduma hizo nje ya nchi.
Mkurugenzi Mtendaji ORCI, Dkt. Diwani Msemo, ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa huduma na mipango ya maendeleo ya Taasisi hiyo.
Amesema huduma hizo zitaanza baada ya kukamilika kwa ujenzi wa vyumba vya upasuaji, jambo litakaloiwezesha ORCI kutoa huduma zote za matibabu ya kibingwa ya saratani na kuwa miongoni mwa vituo vinavyotoa huduma hizo kwa kiwango cha juu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Dkt. Msemo amesema tayari madaktari bingwa saba wa upasuaji wamerejea nchini baada ya kumaliza masomo yao katika maeneo mbalimbali ya utaalamu, yakiwemo magonjwa ya mfumo wa mkojo, magonjwa ya wanawake na upasuaji wa jumla, huku madaktari wengine wanne wakiendelea na masomo.
Amesema Serikali pia imewekeza katika mifumo ya kisasa ya TEHAMA kwa lengo la kuboresha usimamizi wa taarifa za wagonjwa, kuongeza ufanisi wa huduma na kusaidia wataalamu kufanya maamuzi kwa wakati.
Mifumo hiyo ni pamoja na E-Medical Health System, Research Management System, Report Management System, Helpdesk Management System, Enterprise Resource Management System na Attendance Management System, ambayo amesema imewezesha upatikanaji wa taarifa kwa wakati, kuboresha ufuatiliaji wa huduma za wagonjwa, kupunguza matumizi ya nyaraka za karatasi, kuimarisha usimamizi wa rasilimali na kuongeza ufanisi katika upangaji, ufuatiliaji na utoaji wa maamuzi.
Aidha, amesema uwepo wa Call Center umeendelea kusaidia wananchi kupata taarifa na ufafanuzi sahihi kuhusu huduma zinazotolewa na ORCI, pamoja na kuwasilisha maombi, ushauri, maoni, pongezi na malalamiko kuhusu huduma wanazopokea.
Katika hatua nyingine, Dkt. Msemo amesema ORCI imeendelea kuimarisha huduma za uchunguzi wa mapema wa saratani, kampeni za uhamasishaji na utoaji wa elimu kwa umma kwa lengo la kupunguza vifo vinavyotokana na kuchelewa kugundua ugonjwa huo.
Amesema kupitia kampeni ya Tiba Mkoba, ORCI imefika katika mikoa 15 na maeneo mbalimbali ya kazi, ambako imetoa huduma za uchunguzi wa awali wa saratani kwa zaidi ya watu 200,000.
Wakati huo huo, ORCI inaendelea na maandalizi ya kuanzisha vituo vipya vya saratani katika mikoa ya Mtwara, Kigoma na Arusha, hatua inayolenga kusogeza huduma za kibingwa karibu zaidi na wananchi na kupunguza utegemezi wa wagonjwa kusafiri kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.
Kwa mujibu wa Dkt. Msemo, miradi hiyo inatarajiwa kutekelezwa kupitia vyanzo mbalimbali vya fedha, ikiwemo ufadhili wa Serikali na, pale itakapofaa, utaratibu wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Aidha, Taasisi hiyo inaendelea na maandalizi ya kuanzisha ORCI Consultancy Bureau, ambayo itatoa huduma za ushauri wa kitaalamu katika maeneo mbalimbali, ikiwemo ununuzi, usimikaji, upimaji, uanzishaji na matengenezo ya vifaa tiba pamoja na mafunzo ya matumizi na matengenezo ya vifaa hivyo.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...