Na Janeth Raphael - MichuziTv


MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Udhibiti wa Visumbufu Tanzania (TPHPA) imesema hatua za kudhibiti visumbufu na magonjwa ya mimea zimewezesha kuokoa mazao kwa kiwango kikubwa na kuimarisha uwezo wa Tanzania kufikia masoko ya kimataifa.

Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Prof. Joseph Ndunguru, amesema hayo jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Mamlaka kwa mwaka wa fedha 2025/26 pamoja na mipango ya mwaka 2026/27.

Amesema katika kipindi hicho, TPHPA iliweka nguvu katika kuimarisha afya ya mimea, kudhibiti visumbufu na magonjwa, kuboresha huduma za maabara, kutumia teknolojia za kisasa na kuhakikisha mazao yanayozalishwa nchini yanakidhi viwango vinavyohitajika katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wa udhibiti wa ndege waharibifu, Prof. Ndunguru amesema hatua zilizochukuliwa na Mamlaka zimefanikisha kuokoa takribani tani milioni moja za mazao, yakiwemo nafaka, mahindi, ngano na mpunga.

Katika kukabiliana na viwavi jeshi, TPHPA ilifanya udhibiti katika maeneo yaliyoathirika kwa kushirikiana na wakulima pamoja na kampuni zinazozalisha viuatilifu.

Juhudi hizo zilifanyika katika eneo la takribani ekari 228,525 na kusaidia kuokoa takribani tani 342,737 za mazao mbalimbali, huku mahindi yakiwa miongoni mwa mazao yaliyonufaika.

Aidha, TPHPA ilichukua hatua za kudhibiti changamoto ya balae fanya katika maeneo yaliyoathirika, hatua iliyosaidia kulinda takribani ekari 70,136 za mazao.

Prof. Ndunguru amesema mafanikio hayo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha uzalishaji wa mazao nchini unaendelea kuwa salama na wenye tija, huku Tanzania ikiimarisha uwezo wa kuuza mazao yake katika masoko ya kimataifa.

Kwa mwaka wa fedha 2026/27, Mamlaka inalenga kuendeleza udhibiti wa visumbufu na magonjwa ya mimea, kuimarisha mifumo ya afya ya mimea na kuongeza matumizi ya teknolojia ili kulinda uzalishaji na ushindani wa mazao ya Tanzania katika masoko ya kimataifa.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...