Na Mwandishi Wetu, Pwani
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kupitia Idara ya Forodha na Ushuru wa Bidhaa, imetoa elimu kwa wadau wa Forodha mkoani Pwani kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2026, huku wazalishaji wakihimizwa kutumia fursa za unafuu wa ushuru wa forodha katika malighafi za uzalishaji.

Elimu hiyo imewaleta pamoja wawekezaji wa viwanda, mawakala wa Forodha na watumishi wa TRA, ikiwa na lengo la kuwajengea uelewa kuhusu mabadiliko hayo na namna yanavyoweza kutumika kuongeza uzalishaji wa bidhaa za ndani.

Akifungua mafunzo hayo, Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani, Peter Eliyona, amesema mabadiliko hayo ni muhimu katika kuboresha utendaji kazi na kuongeza uzalishaji wa bidhaa za ndani, huku akiwataka wawekezaji kutumia fursa za unafuu wa kodi kuongeza uzalishaji na ajira.

Mafunzo hayo yameendeshwa na Afisa Forodha Mkuu, Allan Maduhu, ambaye amesema mabadiliko hayo yamelenga kulinda viwanda vya ndani na kutoa unafuu wa ushuru wa forodha kupitia utaratibu wa Duty Remission kwa malighafi zinazotumika kuzalisha bidhaa nchini.

Amesema hatua hiyo inalenga kupunguza gharama za uzalishaji, kuhamasisha uwekezaji, kuongeza ushindani wa bidhaa zinazozalishwa nchini pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa muhimu kupitia mpango wa Import Substitution.

Kwa mujibu wa Maduhu, Serikali imetoa unafuu wa ushuru wa forodha kwa malighafi za kuzalisha bidhaa mbalimbali, zikiwemo sabuni, nguzo za umeme za zege, nyaya za umeme, misumari na bidhaa za chuma.

Malighafi nyingine zinazonufaika na unafuu huo ni za kutengeneza vifungashio vya maboksi, vifungashio vya kuhifadhi chai na kahawa iliyochakatwa, vifungashio vya mbegu za kilimo pamoja na vifungashio vya maziwa.

Naye mwakilishi wa JFAWM Motors, Farida Ngwekerwa, amepongeza mabadiliko hayo akisema yatasaidia kupunguza gharama za uzalishaji na kurahisisha upatikanaji wa bidhaa kwa wananchi.

TRA imewataka watumishi na wawekezaji kuendelea kuzingatia mabadiliko ya sheria na kutumia fursa zilizopo, hatua ambayo itasaidia kukuza uzalishaji wa ndani, kuongeza ajira na kuimarisha mchango wa sekta ya viwanda katika uchumi wa Taifa








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...