BANK of Africa Tanzania imeingia makubaliano ya ushirikiano na kampuni ya CFAO Mobility katika kuwezesha upatikanaji wa mikopo ya magari kwa watu binafsi, wataalam, wajasiriamali, wakulima na wafanyabishara mbalimbali nchini kote.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo jijini Dar es Saaam leo, Mkuu wa kitengo cha wateja wakubwa wa Bank of Africa Tanzania, Khalifa Zidadu, amesema ushirikiano huo unajibu hitaji linaloongezeka la kuwezesha upatikanaji wa mikopo ya magari ili kurahisisha usafiri, usafirishaji, biashara za utalii na huduma nyinginezo zinazozidi kupanuka zinazohitaji usafiri.
"Changamoto kwa wateja wengi sio lazima iwe hitaji la gari, lakini uwezo wa kukidhi gharama za awali huku ukiendelea kuwa na mtiririko wa pesa kwa biashara na matumizi mengineyo. Ushirikiano huu unashughulikia pengo hilo kwa kuchanganya chapa za magari zinazoaminika za CFAO na utaalamu wa magari na uwezo wa kutoa mikopo wa Bank of Africa Tanzania, na kuwapatia wateja njia sahihi ya kukopa gari wanalohitaji bila kuwa na shinikizo lisilo la lazima kwenye ukwasi wao,"Amesema Zidadu.
Ushirikiano huu umekuja wakati ambapo upatikanaji wa mkopo unaofaa unabaki kuwa kipaumbele muhimu kwa sekta ya biashara ndogo na za kati ya Tanzania. Bank of AfricaTanzania imeangazia mipango inayolenga kuboresha upatikanaji wa mikopo kwa biashara ndogo na za kati, hasa biashara zenye miradi inayoweza kutegemewa lakini haina mali za kuweka dhamana inayowezesha kupata mkopo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CFAO Mobility Tanzania, Ali TIMIMI, amesema ushirikiano huo utasaidia kufanya umiliki wa vyombo vya usafiri kuwa rahisi kwa kuwaunganisha wateja na magari sahihi kwendana na matakwa yao na njia rahisi ya kupata mkopo kuweza kuyamiliki.
"Kwetu CFAO Mobility Tanzania, kumiliki usafiri wa kuaminika ni kichocheo muhimu cha fursa za kiuchumi. Kwa wateja wetu wengi, gari si njia tu ya usafiri; ni mali inayosaidia kuendesha biashara, kuwahudumia wateja wao, kukuza shughuli zao na kujenga thamani. Ushirikiano wetu na Bank of Africa Tanzania unahusu kuwezesha uwepo wa fursa ya kumiliki chombo cha usafiri,"alisema TIMIMI.
TIMIMI aliongeza kuwa ushirikiano wa Bank of Africa Tanzania ambayo imebobea katika kutoa huduma za mikopo kwa wateja wake na utaalamu wa magari wa CFAO ambayo inauza aina mbalimbali za chapa za magari zinazoaminika utafanikisha kuunda safari ya wateja waliounganishwa zaidi; kuanzia kuchagua gari sahihi hadi kupata mkopo unaohitajika kumiliki chombo na mchakato wa kukipata ulio wa moja kwa moja, wa vitendo unaokidhi mahitaji ya wateja wa pande zote mbili.
Naye, Mkuu wa kitengo cha wateja Binafsi wa Bank of Africa Tanzania, Asupya Nalingigwa, amesema huduma hii ya kuwezesha kukopa magari inawawezesha wateja watakaokidhi vigezo kulingana na uwezo wao wa kulipa, kwa kipindi cha malipo cha hadi miezi 48, kwa ununuzi wa magari mapya kutoka CFAO.
Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa kampuni ya CFAO, Tharaia AHMED amesema kwamba mpango huo wa ushirikiano unafungua fursa za kiuchumi kwa wafanyabiashara , wakulima na wajasirimali katika usafirishaji wa bidhaa na huduma zao.
“Magari yetu ni yenye ubora wa hali ya juu na ya uwezo wa kutunza mazingira kwahiyo ni fursa ya kipekee kwa wakulima wanaosafirisha bidhaa kutoka shambani mpaka kwenye soko na wasafirshaji wa bidhaa mbalimbali nje ya nchini hii pia ni fursa kwao pia,” amesema Tharaia.



.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...