Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
VIJANA,Wasanii na Wadau wa Sanaa na Utalii wanatarajiwa kukutana katika tamasha kubwa la sanaa na utalii la Arusha Arts and Craft Festival, linalolenga kuvumbua vipaji, kuunganisha wadau na kufungua fursa za ajira kwa vijana.
Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika jijini Arusha kuanzia Oktoba 6 hadi 11 katika Viwanja vya General Tyre, likiwaleta pamoja wadau mbalimbali kutoka sekta binafsi na Serikali.
Akitangaza maandalizi ya tamasha hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Tanzania International Tourism Festival, Ibrahim Othman Jama, ameeleza kuwa lengo kuu la mradi huo ni kuleta tija ya kiuchumi na kijamii kupitia kuunganisha sanaa na utalii.
“Tumekuja na mkakati wa mradi ambao unaweza kuunganisha Watanzania, kuwashauri, kuwaelekeza, lakini pia kuvumbua vipaji vyao.Mfumo huu utasaidia kutengeneza mustakabali wa vijana kupitia maendeleo, ajira na ubunifu (creativity) kwa maslahi mapana ya nchi yetu,” alisisitiza Jama.
Jama aliongeza kuwa tamasha hilo linalenga pia kujenga kanzidata (database) kamili ya wasanii na wadau wa kazi za mikono na sanaa za ufundi, wakiwemo waliosajiliwa na wale ambao hawajasajiliwa, ili kurahisisha usimamizi na ushirikishwaji wao katika fursa mbalimbali za kimaendeleo.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Edward Buganga alisema Baraza hilo limejipanga kikamilifu kuunga mkono juhudi za wadau binafsi katika kuinua sanaa za ufundi nchini.
Buganga alibainisha kuwa, tofauti na matamasha mengi yaliyozoeleka ya muziki na fani nyingine, tamasha hili linakuja na mtazamo wa pekee wa kukuza sanaa za ufundi katika kiwango cha kimataifa.
Pia alibainisha kuwa kufanyika kwa tamasha hilo mjini Arusha kunatoa fursa ya kipekee kwa wageni wa kimataifa na wajumbe wa Mkutano Mkubwa wa Mabunge Duniani unaotarajiwa kufanyika nchini kujionea utajiri wa utamaduni na sanaa ya Mtanzania.
Ushirikiano huu kati ya Tanzania International Tourism Festival, BASATA, Bodi ya Filamu pamoja na Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) unadhihirisha azma ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuweka mazingira wezeshi kwa wasanii na kuendeleza uchumi wa ubunifu nchini.-
Naye Mwakilishi kutoka Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA), Grace Byabato, alisema taasisi hiyo itashiriki kikamilifu kutoa elimu kwa wabunifu kuhusu namna ya kulinda kazi zao na kunufaika na mfumo wa mauzo endelevu badala ya kutegemea mauzo ya mara moja pekee.
Mwakilishi wa Bodi ya Filamu Tanzania, Bope Kiungu, alieleza kuwa Bodi hiyo itaonyesha filamu mbalimbali kila siku viwanjani hapo, kuendesha mijadala ya kielimu na burudani, pamoja na kutoa huduma na fursa mbalimbali za sekta ya filamu na michezo ya kuigiza.


.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...