Wakulima wa mwani Zanzibar, ambao wengi wao ni wanawake, wanatarajiwa kunufaika na malipo ya kidijitali na huduma mbalimbali za kifedha kupitia ushirikiano wa kimkakati kati ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mixx na Yas Business.

Ushirikiano huo, uliosainiwa leo Zanzibar, unalenga kutumia teknolojia kurahisisha malipo, kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha na kufungua fursa zaidi za kiuchumi kwa wananchi, hususan kupitia programu ya Seaweed Socio-Enterprise.

Kupitia makubaliano hayo, Mixx itawezesha wakulima wa mwani kupokea malipo yao kidijitali, hatua inayotarajiwa kuongeza usalama, uwazi na kasi ya malipo kwa wakulima wanaoshiriki katika mnyororo wa thamani wa zao hilo.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga, alisema ushirikiano huo unaendana na juhudi za kutumia teknolojia kuongeza fursa za kiuchumi na kurahisisha huduma kwa wananchi.

“Tunataka kuona wanawake na vijana wanaoshiriki katika shughuli za kiuchumi, hususan wakulima wa mwani, wanapata fursa ya kutumia teknolojia kwa manufaa yao. Ushirikiano huu utarahisisha huduma, kuongeza uwazi katika malipo na kuwafungulia wananchi fursa zaidi za kujikwamua kiuchumi,” alisema Waziri Soraga.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx, Angelica Pesha, alisema lengo la Mixx ni kuhakikisha huduma za kidijitali zinakuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi na si kurahisisha malipo pekee.

“Kwa mkulima wa mwani, tunataka teknolojia imsaidie katika maisha yake na shughuli zake za kiuchumi. Aweze kupokea fedha zake kwa usalama na kwa wakati, lakini pia apate huduma zinazoweza kumsaidia kuweka akiba, kupata mitaji na kukuza shughuli zake,” alisema Pesha.

Alisema kupitia huduma kama Kilimo Pesa na Mixx Kikoba, wakulima wa mwani watapata fursa ya kutumia huduma za kifedha zinazoweza kuwasaidia kukuza shughuli zao na kuimarisha hali zao za kifedha.

Mbali na sekta ya mwani, ushirikiano huo pia utasaidia utekelezaji wa programu nyingine za Zanzibar Maisha Bora Foundation. Mixx itawezesha huduma za kidijitali katika Mariam Mwinyi Walkathon, ikiwemo usajili, malipo na uchangishaji wa fedha, pamoja na kuangalia namna teknolojia itakavyosaidia programu za afya kama Afya Bora Medical Camps.

Pesha alisema makubaliano hayo yanaendeleza uwekezaji wa Mixx Zanzibar, ambako kampuni hiyo tayari imekuwa mshirika wa taasisi mbalimbali katika kupeleka huduma za fedha za kidijitali karibu na wananchi.

Kupitia ushirikiano na Zanzibar State Trading Corporation (ZSTC), Mixx imewezesha wakulima wa karafuu kupokea malipo moja kwa moja kupitia simu zao ambapo kwa mwaka jana pekee zaidi ya bilioni 48 zililipwa kwa wakulima wa zao hilo hatua inayoongeza urahisi na uwazi katika mfumo wa malipo.

Aidha, Mixx imechangia Shilingi milioni 350 kwa ajili ya bima ya wakulima kwa kipindi cha miaka mitatu na mwaka 2026 imetoa miche 25,000 ya mikarafuu bila malipo kwa wakulima Zanzibar.

Kampuni hiyo pia ni mshirika wa malipo ya kidijitali katika mabasi ya umeme ya ZanBus, huku kupitia Mixx Kikoba ikiwezesha vikundi vya kijamii kuweka akiba, kuchangia, kununua hisa na kukopeshana kwa njia ya kidijitali.

Naye, Afisa Mkuu wa Yas Business, Norman Kiondo, alisema Yas Business itatumia uwezo wake katika mawasiliano na teknolojia kusaidia ZMBF kurahisisha utekelezaji wa programu zake na kuwafikia wananchi wengi zaidi Zanzibar.

“Kwa upande wa Yas Business, tunataka teknolojia iwe sehemu ya kutatua changamoto halisi. Tutashirikiana na ZMBF katika kuimarisha mawasiliano, intaneti na mifumo ya kidijitali itakayorahisisha usajili, utoaji wa taarifa na ufuatiliaji wa programu mbalimbali. Kwa mkulima wa mwani, mshiriki wa kambi ya afya au mwananchi anayehitaji msaada, teknolojia inapaswa kumrahisishia kupata huduma,” alisema Kiondo.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Bi. Rehema Tukai, amesema ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuongeza fursa za kiuchumi na kijamii kwa wananchi, hususan wanawake na vijana wanaojishughulisha na kilimo cha mwani.

“Tunatamani kuona programu ya Seaweed Socio-Enterprise ikienda sambamba na matumizi ya teknolojia na huduma za kifedha za kidijitali, ili kuwawezesha wakulima wa mwani si tu kupata malipo kwa urahisi, bali pia kujenga uwezo wa kuweka akiba, kupata mitaji na kukuza shughuli zao za kiuchumi,” amesema Bi. Tukai.

Ameongeza kuwa ushirikiano huo utasaidia ZMBF kufikisha huduma na programu zake kwa wananchi wengi zaidi Zanzibar kwa ufanisi, uwazi na urahisi.

Ushirikiano kati ya ZMBF, Mixx na Yas Business unatarajiwa kuimarisha matumizi ya teknolojia katika programu za maendeleo Zanzibar, kwa lengo la kuongeza ujumuishaji wa kifedha na kupanua fursa za kiuchumi kwa wananchi.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...