Na Said Mwishehe,Michuzi TV
MATUMIZI ya teknolojia, utoaji wa mikopo kwa ufanisi na usimamizi bora ni miongoni mwa maeneo muhimu katika kuimarisha sekta ya ushirika wa fedha na kuongeza manufaa kwa wanachama barani Afrika.
Hayo yameelezwa leo Oktoba 13,2026 jijini Dar es Salaam na Naibu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika -Tume ya Maendeleo ya Vyama vya Ushirika iliyo chini ya Wizara ya Kilimo, Udhibiti Collins Nyakunga, alipokuwa akizungumzq na waandishi wa habari katika Kongamano la vyama vya ushirika wa akiba na mikopo barani Afrika linaloendelea nchini Tanzania.
Ambapo amesema pia kongamano hilo linatoa fursa kwa washiriki kujadili mbinu bora za kuimarisha SACCOS na kuboresha huduma zinazotolewa kwa wanachama huku akisisitiza matumizi ya teknolojia, utoaji wa mikopo kwa ufanisi na usimamizi bora ni miongoni mwa maeneo muhimu kuimarisha sekta ya ushirika wa fedha na kuongeza manufaa kwa wanachama.
Pia amesema vyama vya akiba na mikopo vinatakiwa kuboresha huduma zake na kutumia teknolojia kuvutia vijana kujiunga navyo ili kuwawezesha kupata huduma za kifedha, kuanzisha biashara na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji
Kuhusu Tanzania kuwa mwenyeji wa kongamano hilo amesema imetokana na mafanikio yaliyopatikana katika usimamizi na uendelezaji wa sekta ya vyama vya ushirika wa akiba na mikopo nchini.Kongamano hilo linaonesha umuhimu wa kubadilishana uzoefu miongoni mwa nchi za Afrika katika kuboresha mifumo ya uendeshaji wa vyama hivyo na kuimarisha mchango wake katika maendeleo ya kiuchumi.
Kwa mujibu wa Nyakunga, matumizi ya teknolojia ni miongoni mwa masuala yanayojadiliwa, yakilenga kuboresha utoaji wa mikopo, kuongeza ufanisi wa marejesho na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha.
“Huduma zinazozingatia mahitaji ya vijana zinaweza kuwa muhimu katika kuwahamasisha kujiunga na SACCOS, hasa wale wanaotaka kuanzisha biashara ndogo, kupanua shughuli za ujasiriamali au kuwekeza katika shughuli nyingine za kiuchumi.”
Aidha, mikopo inayotolewa inapaswa kutumika kwa shughuli za uzalishaji na uwekezaji ili kuwasaidia wanachama kuongeza kipato, kuboresha maisha yao na kuimarisha uwezo wao wa kurejesha mikopo kwa wakati.
Nyakunga amesema masuala mengine yanayojadiliwa katika kongamano hilo ni utawala bora, uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali, ambayo ni muhimu katika kuhakikisha SACCOS zinaendeshwa kwa ufanisi na kulinda maslahi ya wanachama.
Amesema kuimarisha mifumo ya usimamizi kutasaidia vyama hivyo kuboresha huduma zake, kuongeza imani ya wanachama na kuendeleza uhusiano mzuri kati ya taasisi hizo na watu wanaotafuta huduma za kifedha.
Kongamano hilo, linaloratibiwa na Chama cha Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo Afrika (ACOSCA), linafanyika Tanzania kuanzia Oktoba 11 hadi 16, 2026, likitarajiwa kuwashirikisha wajumbe zaidi ya 600 kutoka Tanzania na nchi nyingine za Afrika.
Ufunguzi rasmi umepangwa kufanyika Oktoba 15, ukitarajiwa kuongozwa na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba.
Kongamano hilo linatarajiwa kutoa nafasi ya kujifunza mbinu mpya za kuimarisha huduma za kifedha, kuongeza ufanisi wa SACCOS na kupanua fursa za wananchi kushiriki katika maendeleo ya kiuchumi.



.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...