Na Janeth Raphael - MichuziTv

Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, ameitaka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kuimarisha udhibiti wa dawa bandia na kuongeza kasi ya kuwabaini wanaojihusisha na uingizaji na usambazaji wa dawa zisizokidhi viwango, akisisitiza kuwa wahusika wanapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Mchengerwa ameyazungumza hayo leo jijini Dodoma mara baada ya kuzindua bodi mpya ya TMDA ambapo amesema dawa zisizokidhi viwango vya usalama na ubora zinaweza kuhatarisha maisha ya wananchi, hivyo Serikali na mamlaka zinazohusika hazipaswi kuvumilia vitendo vinavyoweza kuhatarisha afya za watumiaji.

Ameitaka bodi, menejimenti na watumishi wa TMDA kutumia mbinu za kisasa za ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa ili kubaini mitandao inayojihusisha na biashara hiyo haramu. Miongoni mwa mbinu alizosisitiza ni uchunguzi wa taarifa zinazopatikana katika vyanzo vya wazi (Open-Source Intelligence), unaoweza kusaidia kubaini wahusika na kufuatilia shughuli zao.

Aidha, Waziri huyo ameeleza umuhimu wa Serikali kuangalia uwezekano wa kuimarisha sheria zinazohusu udhibiti wa dawa bandia, ili kuhakikisha wanaopatikana wakijihusisha na biashara hiyo wanakabiliwa na adhabu kali zinazolingana na uzito wa makosa yao, badala ya kuishia kupata adhabu ndogo za jinai.

Amesisitiza kuwa TMDA inapaswa kutekeleza majukumu yake kwa ujasiri na weledi, hususan katika kuzuia dawa ambazo hazijathibitishwa usalama na ubora wake kuingia sokoni na kutumiwa na wananchi.

Mchengerwa amebainisha kuwa mamlaka hiyo haipaswi kuyumba kutokana na ukubwa au ushawishi wa mwekezaji anayehusika, bali inapaswa kuweka mbele maslahi ya umma na kuhakikisha kila dawa inayoruhusiwa kutumika nchini inakidhi viwango vinavyotakiwa.

Ameongeza kuwa uzoefu wa udhibiti wa dawa duniani unaonesha umuhimu wa kuwa na mamlaka imara zinazoweza kufanya maamuzi magumu kwa kuzingatia ushahidi wa kisayansi, usalama na ubora wa dawa.

Amesisitiza kuwa TMDA ina wajibu mkubwa wa kulinda afya za Watanzania, hivyo udhibiti wa dawa nchini unapaswa kufanyika kwa haki, uwazi na bila upendeleo, ili kuhakikisha wananchi wanapata dawa salama na zenye ubora unaotakiwa.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...