Na Janeth Raphael - MichuziTv

Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Faris Buruhani, amesema uongozi wa jumuiya hiyo hautavumilia vitendo vya kuwabagua, kuwavunja moyo au kuwanyima haki vijana wanaojitolea kwa uzalendo katika kukitumikia chama, akitaka tuhuma zilizotolewa kuhusu suala hilo zichunguzwe na kufanyiwa kazi.

Buruhani amesema vijana wengi wamekuwa wakitoa mchango mkubwa katika shughuli za chama bila kutarajia malipo, wakiongozwa na uzalendo na dhamira ya kuhakikisha CCM inaendelea kuimarika. Amesisitiza kuwa juhudi hizo zinapaswa kuthaminiwa badala ya kuwakatisha tamaa wale wanaojitolea kwa ajili ya maendeleo ya jumuiya.

Akizungumzia msimamo huo, Buruhani amesema kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa UVCCM, Mohammed Kawaida, inaakisi dhamira ya uongozi wa jumuiya hiyo ya kuhakikisha vijana wanapata haki zao na wanatendewa kwa usawa.

Ameeleza kuwa mchango wa vijana umeonekana wazi katika vipindi mbalimbali vya uchaguzi, ambapo wamekuwa wakijituma kwa nguvu na kujitolea muda wao kuhakikisha shughuli za chama zinafanikiwa.

“Hatutaweza kukubali kuona vijana wetu wanakatishwa tamaa na kubaguliwa huku sisi kama viongozi wao tukikaa kimya. Tunawaomba viongozi waliopata nafasi kupitia UVCCM kuwalinda vijana, kusimama imara kuwatetea, kuwatia moyo na si kuwavunja moyo,” amesisitiza Buruhani.

Aidha, ametoa wito wa kufanyiwa uchunguzi kwa tuhuma zilizotolewa, akionya kuwa kuziacha bila kupatiwa ufumbuzi kunaweza kudhoofisha ari ya vijana ya kujitolea na kupunguza hamasa yao ya kushiriki katika shughuli za chama.

Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa viongozi kuhakikisha vijana wanaojituma wanathaminiwa, wanalindwa na wanapata nafasi ya kutekeleza majukumu yao bila kukumbana na vitendo vya ubaguzi au kutotendewa haki.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Bara, Mussa Mwakitinya, amemhakikishia Buruhani ushirikiano wa dhati katika utekelezaji wa majukumu ya jumuiya hiyo, akisema vijana wamejipanga kwenda naye sambamba katika kuimarisha umoja na kuhakikisha chama kinaendelea kusonga mbele.

Mwakitinya amesisitiza kuwa mshikamano na ushirikiano miongoni mwa vijana ni nguzo muhimu katika kuimarisha UVCCM na kufanikisha malengo ya Chama Cha Mapinduzi.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...