Picha mbalimbali za matukio ya Mgombea mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emmanuel John Nchimbi kwenye mkutano wake wa hadhara uliofanyika leo Septemba 29,2025 katika viwanja vya Malamba Mawili,Jimbo la Kibamba wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam.










 

Na Karama Kenyunko, Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imezindua rasmi Mafunzo ya Ndani ya Nchi kwa wataalamu wanaosimamia Mradi wa Mawasiliano Vijijini (Tanzania Mobile Network for Rural Coverage Project – TMN4RCP).

Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam leo, Septemba 29, 2025.

Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa wizara hiyo, Salome Kessy amesema Serikali imejipanga kuhakikisha kila Mtanzania, mjini au kijijini, anapata huduma bora na za uhakika za mawasiliano ya simu, intaneti, na usikivu wa redio kupitia TBC Taifa.

“Katika dunia ya sasa inayosukumwa na kasi ya maendeleo ya kidijitali, hakuna taifa linaloweza kufanikisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi bila mifumo thabiti ya mawasiliano. Mradi wa Mawasiliano Vijijini ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira hii, na unakusudia kuwafikishia wananchi wote huduma bora za mawasiliano,” amesema.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwajengea wataalamu uwezo wa kusimamia miradi ya TEHAMA vijijini kwa weledi. Mafunzo yanahusisha usimamizi na uboreshaji wa mitandao ya simu vijijini (2G na 4G), teknolojia za LTE, uendeshaji wa miundombinu ya mawasiliano (Core Network), pamoja na mbinu za kushughulikia changamoto za sauti, intaneti na malipo ya simu vijijini.

Ameishukuru taasisi washirika TTCL, TBC na UCSAF kwa mchango wao katika utekelezaji wa mradi huo, akisisitiza kuwa jukumu la wataalamu hao ni sehemu ya mageuzi makubwa ya mawasiliano nchini.

Kwa upande wake, Mulembwa Munaku, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa wizara hiyo, alisema mradi huo umebuniwa na Serikali ili kuhakikisha maeneo yote ya Tanzania yanapata mawasiliano na usikivu wa redio.

“Kwa sasa, usikivu wa mawasiliano unafikia asilimia 75 pekee ya eneo lote la kijiografia la nchi. Kuna maeneo mengi hayana kabisa mawasiliano wala usikivu wa redio, ndiyo maana Serikali imekuja na mradi huu,” amesema.

Amesema kuwa mradi huo ni wa miaka miwili, ulioanza kutekelezwa Desemba 2024 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2026.

Kwa mujibu wa Munaku, mradi unahusisha ujenzi wa minara 636, kati ya hiyo 621 kwa ajili ya mawasiliano ya simu ambayo itaendeshwa na TTCL na makampuni mengine ya simu, huku 15 ikiwa ni ya redio itakayoendeshwa na TBC.

Amesema Serikali iliona umuhimu wa mafunzo kwa wataalamu wa ndani kwa kuwa mitambo hiyo inajengwa kwa teknolojia ya kisasa, na hivyo wataalamu 140 kutoka TBC na TTCL wanashiriki mafunzo hayo.

Aidha, kabla ya mafunzo haya ya ndani, wataalamu 72 kutoka mashirika mbalimbali walihudhuria mafunzo nchini China kati ya Februari na Juni mwaka huu.

Kwa upande wake, Kelvin Mwakaleke, Meneja wa Mradi huo, amesema Serikali ilisaini mkataba wa utekelezaji na Mkandarasi China Technical Import and Export Corporation (CNTIC) Oktoba 23, 2023 kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 108.5, mkopo nafuu kutoka Benki ya Exim ya China.

Utekelezaji wa mradi huo wa miezi 24 umeshaanza, ambapo hadi kufikia Septemba 29, 2025 umekamilika kwa asilimia 56. Kati ya minara 621 ya simu, upembuzi yakinifu wa minara 467 umekamilika, 261 imejengwa na 130 kati yake tayari inatoa huduma.

Ujenzi wa minara ya redio 15 unaendelea na unatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 30 mwaka huu. Vilevile, ufungaji wa miundombinu mikuu ya mawasiliano katika TTCL Dar es Salaam na Dodoma umekamilika kwa asilimia 90, huku ugomboaji wa vifaa ukiwa umefikia asilimia 65.

Mafunzo ya ndani yanayozinduliwa leo yataendelea hadi Novemba 7, 2025 na yanatarajiwa kuwanufaisha wataalamu 140 katika maeneo ya Radio Access Network (BTS Systems), Transmission (Backhauling), Power Systems, Civil Works (Towers), na Core Network.

Kwa hatua hiyo, Serikali imedhihirisha dhamira ya kuhakikisha kila kijiji nchini kinafikiwa na huduma za mawasiliano, ili kuimarisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za kijamii, kiuchumi na kiutawala.





Na Emmanuel Massaka – Michizi TV

Serikali imezindua rasmi Bodi mpya ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) katika hafla iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na ufanisi katika sekta ya utumishi wa umma nchini. Uzinduzi huo umefanyika katika kituo cha Mafunzo kwa Njia ya Mtandao cha chuo hicho.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Selemani Mkomi, alisema kuwa kuundwa kwa bodi hiyo ni hatua muhimu katika kuleta mageuzi madhubuti ya kiutendaji. “Ukiboresha Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, umeboreisha Utumishi wa Umma,” alisema, akisisitiza umuhimu wa chuo katika kuboresha rasilimali watu serikalini.

Bw. Mkomi aliwapongeza wajumbe wapya wa bodi na kueleza kuwa uteuzi wao umezingatia weledi, uadilifu na uzoefu katika nyanja mbalimbali. Alibainisha kuwa jukumu kuu la bodi ni kuhakikisha chuo kinatoa mafunzo yanayoendana na viwango vya kitaifa na kimataifa, pamoja na kutoa mchango katika mageuzi ya sekta ya umma.

Amesisitiza kuwa wajumbe wa bodi wanapaswa kutoa dira na ushauri wa kimkakati utakaowezesha chuo kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, kusimamia rasilimali kwa ufanisi, na kuimarisha nidhamu na maadili katika utumishi wa umma. Aidha, serikali imeahidi kuendelea kutoa mwongozo na sera zitakazowezesha chuo kutimiza malengo yake.

Wakati wa hafla hiyo, Bw. Mkomi aliwatambulisha wajumbe wa bodi wapya wakiongozwa na Dkt. Florens Martin Turuka (Mwenyekiti), Dkt. Ernest Francis Mabonesho (Katibu), pamoja na wajumbe wengine: Mhe. Jaji (Mstaafu) Awadh Mohamed Bawazir, Prof. Masoud Hadi Muruke, Balozi John Ulanga, Dkt. Faraja Teddy Igira na Bi. Leila Maurilyo Mavika.

Akitoa taarifa ya utendaji wa bodi iliyomaliza muda wake, Dkt. Florens Turuka alisema kuwa katika kipindi cha miaka minne, chuo kilipata hati safi za ukaguzi wa serikali mfululizo, jambo alilolieleza kuwa ni alama ya uwajibikaji na usimamizi bora wa fedha. Aliongeza kuwa bodi iliidhinisha sera na mifumo kadhaa ya kitaasisi ikiwemo sera za utafiti, TEHAMA,  ubora wa huduma na miundombinu.

Katika kipindi hicho, jumla ya wanachuo 43,753 walihitimu, na zaidi ya watumishi 46,000 wa umma walipatiwa mafunzo ya muda mfupi. Pia tafiti tumizi nane na machapisho 43 yaliandaliwa na chuo, huku zaidi ya watumishi 4,000 wakifaulu mitihani ya utumishi wa umma.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo na Afisa Mtendaji Mkuu, Dkt. Ernest Mabonesho, alisema kuwa zaidi ya watumishi 47,000 wa umma wamepatiwa mafunzo katika kipindi cha miaka minne, ikiwa ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na bodi iliyotangulia. Ameeleza kuwa mafunzo hayo yaligawanywa katika makundi ya umahiri, uongozi, maadili, utawala bora, na ujenzi wa uwezo.

Aidha, Dkt. Mabonesho alibainisha kuwa miradi ya miundombinu inaendelea kuimarishwa, ikiwemo kukamilika kwa awamu ya pili ya ujenzi wa Kampasi ya Singida kwa gharama ya Sh bilioni 2.2, na hatua nzuri za ujenzi wa Kampasi ya Tanga kwa ufadhili wa serikali. Pia alieleza kuwa chuo kina jumla ya watumishi 372, na kimeendelea na mikakati ya kuajiri, kuendeleza na kuwapandisha vyeo watumishi wake.
Uzinduzi wa bodi mpya umeonekana kuwa hatua muhimu katika kuimarisha dira ya chuo na kukuza ubora wa utumishi wa umma nchini, huku wajumbe wapya wakiahidi kuendeleza mafanikio yaliyopatikana na kubuni mbinu mpya za ufanisi na ubunifu.




























 

Na Karama Kenyunko Michuzi Tv

MAHAKAMA Kuu, Masijala Ndogo ya Dar es Salaam, imetoa siku 14 kwa Bodi ya Wadhamini ya Chadema upande wa Bara na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, kuwasilisha nyaraka zilizotakiwa na wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema Zanzibar(walalamikaji).

Nyaraka hizo ni Ripoti ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, taarifa za benki na tamko la mali za chama kuanzia mwaka 2019 hadi 2024.

Amri hiyo ilitolewa jana na Jaji Hamidu Mwanga wakati kesi namba 8323/2025 ilipoitwa kwa ajili ya uamuzi mdogo.

Katika kesi hiyo Walalamikaji ni Said Issa Mohamed, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu, wakijitambulisha kama wajumbe halali wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema Zanzibar wakilishwa na mawakili Alvan Fidelis, Dido Simfukwe na Fabian Joseph, huku upande wa wajibu maombi ukiwakilishwa na mawakili Hekima Mwasipu na Dk Rugemeleza Nshala.

Walalamikaji wanadai kuwa Katiba ya chama na Sheria ya Vyama vya Siasa zimekiukwa, hususani kwenye mgawanyo wa rasilimali kati ya Bara na Zanzibar.

Katika uamuzi wa mahakama Jaji Mwanga alisema sheria inaruhusu upande wa pili kuwasilisha nyaraka zilizoombwa iwapo zitathibitishwa na kutumika kusaidia mwenendo wa shauri hilo

“Kwa hali hiyo, natoa siku 14 nyaraka hizo ziwasilishwe Mahakamani na upande wa pili wapewe, kisha zipitiwe ndani ya siku 19 za kazi, yaani hadi Oktoba 24, mwaka huu. Baada ya hapo tutakutana kusikiliza mapingamizi yaliyowasilishwa na walalamikiwa,” alisema Jaji Mwanga.

Hata hivyo, alibainisha kuwa nyaraka za mihutasari ya vikao haziwezi kutolewa kwa kuwa mlalamikaji hakutaja tarehe mahsusi za vikao anavyohitaji, na pia baadhi ni siri za chama.

Kesi hiyo  imepangwa kusikilizwa tena Oktoba 30, mwaka huu.

Awali, wakili wa walalamikaji Alvan Fidelis alidai nyaraka hizo zina umuhimu mkubwa kwa shauri, kwani ndizo zitakazoonyesha iwapo rasilimali za chama ziligawanywa sawa kati ya Bara na Zanzibar.

“Nyaraka ziko mikononi mwa wajibu maombi. Hawajakataa kuwa nazo, bali wamedai kuna amri ya zuio. Lakini zuio hilo ni la kuzitumia, si kuziwasilisha,” alisisitiza.

Kwa upande wao, wakili wa Chadema, Hekima Mwasipu, alidai maombi hayo hayana mashiko kwa sababu nyaraka za kumbukumbu za vikao vya Kamati Kuu hazina uhusiano na kesi ya msingi.

Alidai walalamikaji walipaswa kubainisha ni kikao kipi kilijadili suala linalohusu mgogoro wao. Pia alidai kuwa nyaraka hizo zinaweza kupatikana kupitia Msajili wa Vyama vya Siasa iwapo Mahakama itaagiza.

Naye Dk Nshala alidai baadhi ya walalamikaji hawana viapo vinavyowaruhusu kuendelea na maombi hayo, huku akidai kuwa Said Mohamed si kiongozi tena wa Chadema baada ya uchaguzi wa Januari 21, 2025, na hivyo kujitambulisha kama kiongozi mwandamizi ni upotoshaji.




MASHINDANO ya raundi ya nne ya kumuenzi mchezaji gofu wa timu ya taifa wanawake marehemu Lina Nkya, Lina PG Tour yametamatika kwa kishindo mkoani Morogoro huku mchezaji wa kulipwa (Pro), Fadhyl Nkya akiibuka tena na ushindi na kujinyakulia kitita cha Sh. Milioni 6.8.

Mashindano hayo yaliyoanza kutimua vumbi Septemba 25, mwaka huu na kumalizika jana yameshirikisha wachezaji wa gofu wa kulipwa (Mapro), ridhaa (Elite Amateurs) na wasindikizaji kutoka maeneo mbalimbali nchini huku Fadhyl akishinda mara tano mfululizo.

Mbali na Fadhyl mshindi wa pili kwa upande wa wachezaji wa gofu wa kulipwa (Mapro) ni Rajab Iddy aliyepata Sh. Milioni 4.3 huku nafasi ya tatu na nne ikichukuliwa na Hassan Kadio pamoja na Nuru Mollel, nafasi ya tano ni John Said, wa sita ni Elisante Lembris na nafasi ya saba ni John Leonce.

Kwa upande wa wachezaji wa ridhaa (Elite Amateurs), mshindi wa kwanza ni Isiaka Dunia aliyejinyakulia kiasi cha Sh. Milioni 2.2, nafasi ya pili ikichukuliwa na Enoshi Wanyeche aliyepata Milioni 1.3 huku nafasi ya tatu ni Hawa Wanyeche aliyepata Sh. 900,000.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa michuano hiyo, Nkya alisema kuwa siri ya ushindi wake wa mara tano mfululizo ni mazoezi ya mara kwa mara ambayo amekuwa akiyafanya.

Alisema amekuwa akisafiri nchi mbalimbali kushiriki michuano ya gofu na kwamba kabla ya kwenda huko anahakikisha anafanya mazoezi ya kutosha ili kujiweka tayari kushindana na wachezaji wengine.

“Unajua huu mchezo kila mtu anaouwezo wa kushinda, hata hivyo nimekuwa nikisafiri sana nje ya nchi kucheza michuano ya kimataifa ambayo imenifanya niwe katika kiwango kizuri kushiriki katika michuano hii ya ndani,” alisema Nkya.

Aidha alisema ili nchi iweze kupata medali mbalimbali za kimataifa katika mchezo huo wanahitaji mashindano mengi na wadau kujitokeza kwa wingi ili wachezaji waweze kupata michuano mingi ya kucheza kwa mwaka.

Naye Miongoni mwa wasimamizi wa Lina PG Tour, Enock Magile amewashukuru wachezaji wote waliojitokeza na kuwataka walewote ambao hawakufanya vizuri kuendelea na mazoezi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kushiriki mashindano yajayo.

Alisema raundi ya tano na ya mwisho ya mashindano hayo kwa mwaka huu inatarajiwa kufanyika Novemba na kwamba kama hakutakuwa na mabadiliko itafanyika katika Viwanja vya Kili Gofu mkoani Arusha.

“Wachezaji wanaoshiriki kwa sasa ni wengi hivyo tunashukuru mashindano Morogoro yalianza vizuri na yamemalikiza kwa wakati, tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa, tuwaombe tu wachezaji waendelee kujiandaa na raundi ya tano ili kuhakikisha tunawapata wawakilishi wazuri katika michuano ya kimataifa,” alisema Magile

Mshindi wa jumla wa raundi ya tano ya Lina PG Tour ataiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa yatakayofanyika Dubai mwakani.






MICHUANO ya raundi ya nne ya kumuenzi mlezi na mwendelezaji wa gofu ya wanawake aliyefariki dunia miaka ya hivi karibuni Lina Nkya, Lina PG Tour imetamatika kwa kishindo mkoani Morogoro huku baadhi ya wachezaji walioibuka na ushindi wakijipatia zawadi mbalimbali zikiwemo fedha.

Mashindano hayo yaliyoanza kutimua vumbi Septemba 25, mwaka huu na kumalizika jana yameshirikisha wachezaji wa gofu wa kulipwa (Mapro), ridhaa (Elite Amateurs) na wasindikizaji kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Katika michuano hiyo mshindi wa kwanza kwa upande wa wachezaji wa gofu wa kulipwa (Mapro) ni Fadhyl Nkya aliyejinyakulia kiasi cha Sh. Milioni 6.8, wa pili ni Rajab Iddy aliyepata Sh. Milioni 4.3 huku nafasi ya tatu na nne ikichukuliwa na Hassan Kadio pamoja na Nuru Mollel.

Kwa upande wa wachezaji wa ridhaa (Elite Amateurs), mshindi wa kwanza ni Isiaka Dunia aliyejinyakulia kiasi cha Sh. Milioni 2.2, nafasi ya pili ikichukuliwa na Enoshi Wanyeche aliyepata Milioni 1.3 huku nafasi ya tatu ni Hawa Wanyeche aliyepata Sh. 900,000.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa michuano hiyo, Miongoni mwa wasimamizi wa Lina PG Tour, Enock Magile amewashukuru wachezaji wote waliojitokeza na kuwataka walewote ambao hawakufanya vizuri kuendelea na mazoezi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kushiriki mashindano yajayo.

Alisema raundi ya tano na ya mwisho ya mashindano hayo kwa mwaka huu inatarajiwa kufanyika Novemba na kwamba kama hakutakuwa na mabadiliko itafanyika katika Viwanja vya Kili Gofu mkoani Arusha.

“Wachezaji wanaoshiriki kwa sasa ni wengi hivyo tunashukuru mashindano Morogoro yalianza vizuri na yamemalikiza kwa wakati, tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa, tuwaombe tu wachezaji waendelee kujiandaa na raundi ya tano ili kuhakikisha tunawapata wawakilishi wazuri katika michuano ya kimataifa,” alisema Magile

Kwa upande wake mshindi katika mashindano hayo kwa upande wa wachezaji wa gofu wa kulipwa, Fadhyl Nkya amefunguka siri ya ushindi wake kwa mara tano mfululizo ni mazoezi ya mara kwa mara ambayo amekuwa akiyafanya.

Alisema amekuwa akisafiri nchi mbalimbali kushiriki michuano ya gofu na kwamba kabla ya kwenda huko anahakikisha anafanya mazoezi ya kutosha ili kujiweka tayari kushindana na wachezaji wengine.

“Unajua huu mchezo kila mtu anaouwezo wa kushinda, hata hivyo nimekuwa nikisafiri sana nje ya nchi kucheza michuano ya kimataifa ambayo imenifanya niwe katika kiwango kizuri kushiriki katika michuano hii ya ndani,” alisema Nkya.

Aidha alisema ili nchi iweze kupata medali mbalimbali za kimataifa katika mchezo huo wanahitaji mashindano mengi na wadau kujitokeza kwa wingi ili wachezaji waweze kupata michuano mingi ya kucheza kwa mwaka.

Mshindi wa jumla wa raundi ya tano ya Lina PG Tour ataiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa yatakayofanyika Dubai mwakani.

Top News