Na Mwandishi Wetu

UJUMBE wa Tanzania umeunga mkono Mkataba mpya wa Kimataifa unaolenga kulinda haki, usalama na ustawi wa Wafanyakazi wa Mtandaoni ikiwa ni dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuhakikisha maendeleo ya teknolojia na majukwaa ya kidijitali yanakwenda sambamba na ulinzi wa utu wa mfanyakazi, usawa na haki za msingi za kazi.

Hayo yamejiri wakati wa hafla ya kuhitimisha Mkutano Mkuu wa 114 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) leo tarehe 12 Juni, 2026 uliyofanyika katika Ukumbi wa Umoja wa Mataifa, Jijini Geneva, Uswisi ambapo kupitia Mkutano huo, taarifa za Kamati mbalimbali zilipokelewa ikiwemo Kamati ya Upangaji wa Viwango vya Kazi ambayo imewezesha kuandaliwa na kupitishwa kwa Mkataba wa Kazi kuhusu Wafanyakazi Mtandaoni wa Mwaka 2026.

Katika kupitisha Mkataba huu, kura 406 zimeunga mkono kupitishwa kwa Mkataba husika, nchi Nane (8) hazijaunga mkono kupitishwa Mkataba na nchi 36 hazijaonesha kuwa upande wowote.

Mkataba huo mpya umeweka misingi ya kimataifa kuhusu: Ulinzi wa haki za msingi za wafanyakazi wa mtandaoni; Uainishaji sahihi wa hadhi ya ajira kulingana na hali halisi ya kazi; Malipo ya haki na uwazi; Upatikanaji wa hifadhi ya jamii; Uwazi na udhibiti wa mifumo ya kidijitali ikiwemo haki ya maelezo na mapitio ya maamuzi yanayofanyika kidijitali pamja na Ulinzi wa taarifa binafsi na haki ya kupata kusuluhisha migogoro.

Akitoa hotuba yake wakati wa kufunga Mkutano huo, Rais wa Mkutano Mkuu wa 114 wa ILO, Juan Castillo, amesisitiza kuhusu mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia makubaliano ya kihistoria kuhusu kazi za staha kwa kazi zinazofanyika kidijitali.

Amesema, kutokana na ukuaji wa sayansi na teknolojia, kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya Akili Unde (AI), hivyo, amesisitiza kwamba teknolojia inapaswa kutumika ili kuendeleza ustawi wa binadamu na si kuondoa utu wa wafanyakazi au kuongeza ukosefu wa usawa, huku akihimiza matumizi ya Akili Unde yanayozingatia maadili na haki za kazi.

Kwa upande mwengine, Juan Castillo amepongeza mfumo wa Utatu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) umekuwa ni chombo muhimu cha kuwaleta pamoja waadau husika, yaani Serikali, Waajiri na Wafanyakazi, akieleza kuwa majadiliano na mafikiano yaliyofikiwa katika siku 12 za Mkutano huo yamethibitisha umuhimu wa mazungumzo ya kijamii katika kukuza ustawi wa Sekta ya Kazi.

Upitishwaji wa Mkataba wa Kazi Kuhusu Wafanyakazi wa Mtandaoni haumaanishi kuanza kwa utekelezaji wa baadhi ya masuala yaliyoanishwa katika Mkataba huo kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita kupita Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano pamoja na Wadau wengine wa masuala ya Kazi,

Ulianzishwa kutekeleza viwango vilivyotajwa katika Mkataba huo ambapo miongoni mwa jitihada zilizochukuliwa ni pamoja na: Kukuza na kutambua wafanyakazi wa mitandaoni kwa kuimarisha uchumi wa kidijitali; Kuimarisha ulinzi wa matumizi ya mtandao kupitia Sheria na miongozo kama vile Sheria ya Makosa ya Mtandaoni na Kanuni za Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

Aidha, utoaji wa mafunzo ya TEHAMA kwa vijana yanalenga kuongeza fursa za ajira za kidijitali na kuwasaidia wafanyakazi wa mitandaoni kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kuingia kwenye soko la kimataifa na uimarishaji wa mifumo ya kidijitali umeendelea kupanua miundombinu ya TEHAMA kama vile upanuzi wa mtandao wa Vijijini na Mijini ili kuwezesha watu wengi zaidi kufanya kazi mtandaoni kwa ufanisi.

Mkutano Mkuu wa 114 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) umihitimishwa leo na kukamilika kwake ni mwanzo wa Kikao cha 357 cha Bodi ya Magavana ya ILO unaofanyika tarehe 12 na 13 Juni, 2026 Geneva, Uswisi ambapo Tanzania pia ni Mjumbe wa Bodi hiyo ikiwakilisha nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki.














Na Said Mwishehe,Michuzi TV

MSANII maarufu nchini katika muziki wa kizazi kipya a.k.a Bongo Fleva Rashidi Makwiro maarufu Chid Benz ametoa ya moyoni kwa kuishukuru Mamlaka ya Kudhihiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na wote waliomuwezesha kuachana na matumizi ya dawa za kulevya.

Chid Benz ametoa shukrani hizo Juni 12,2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa filamu iliyopewa jina Kifurushi ambayo ni maalum kuelezea madhara ya dawa za kulevya.

Pia ni filamu inayotoa elimu kwa madereva,makondakta na abiria kuwa makini kwa kutosafirisha vifurushi ambavyo hawajui ndani yake kuna nini.Ni filamu iliyoandaliwa na mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Bodi ya Filamu Tanzania pamoja na LATRA.

Katika uzinduzi wa filamu hiyo msanii Chid Benz ambaye ubora wake katika muziki umeeendelea kubaki katika viwango vya daraja la juu aliyepewa jukum la kutoa burudani kupitia vibao vyake kadhaa kikiwemo Dar es Salaam Stand up alitumia nafasi hiyo kutoa shukrani zake kwani kwa sasa ameachana kabisa na dawa za kulevya .

“Kamishina wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo nakushukuru sana.Uliamua kunisaidia kuniondoa kwenye matumizi ya dawa za kulevya.Nakushukuru kwasababu pia nikikupigia simu unapokea,meseji unajibu.”

Akiendelea kuzungumza Chidi Benzi amesema “natamani niwaambie ndugu zangu tuache dawa za kulevya lakini sidhani kama sasa hivi watu wanatumia maana nahisi dawa hizo hazipo mtaani.Kuna saa zingine naongea na ndugu zangu nauliza vipi mtaani freshi wanaambia sio freshi.

“Kwahiyo hiyo kazi ambayo imefanyika ya kukomesha dawa za kulevya imefanyika kwa ukubwa kwani zamani ilikuwa kwa mfano nikikaa kama hapa nikiuliza eh bwana vipi hapa naambiwa freshi pita nyuma lakini sasa nakwambia ah sio freshi Chidi.”

Ameongeza kwa upande yeye ameacha kabisa kutumia dawa za kulevya na sasa hivi hata bila kumwambia mtu kama anatumia mtu mwenyewe anamuwahi kumwambia ameacha.

“Hivyo nashukuru Serikali, nashukuru Mamlaka ,nakushukuru kila mtu nashukuru na

leo tuko pamoja na kuonyesha kwamba nina nguvu za kutosha ninaburudisha,”amesema na kusisitiza naye anaungana na Mamlaka kuwahimiza wamiliki wa mabasi,madereva,makondakta na wananchi kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika kutoa taarifa.

Aidha amesema filamu hiyo iliyozinduliwa itasaidia kuongeza uelewa wa jamii na kuimarisha mapambano dhidi ya usafirishaji wa dawa za kulevya nchini.







 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete (Mb.), amewasili mkoani Mtwara kuhudhuria Mahafali ya 43 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Kampasi ya Mtwara, yanayofanyika leo Juni 13, 2026.

Mara baada ya kuwasili, Mhe. Kikwete amepokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Donald William Msengi, pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.






 

Na mwandishi wetu - Dar es Salaam

Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Taasisi OpenMap Development Tanzania (OMDTZ), kupitia mradi wa Ramani Zetu, Sauti Zetu imeendesha warsha ya kupitia na kuthibitisha Mipango ya Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa kwa kata tano za Makurumula, Mabibo, Keko, Ubungo na Tabata jijini Dar es Salaam.

Warsha hiyo imewakutanisha viongozi wa serikali za mitaa, Kamati za Usimamizi wa Maafa za Kata, wataalamu wa usimamizi wa maafa, waratibu wa maafa wa mkoa na wilaya pamoja na wadau mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha mipango hiyo inakidhi mahitaji halisi ya jamii zinazokabiliwa na hatari ya mafuriko Dar es Salaam.

Akifungua warsha hiyo Mkurugenzi Msaidizi wa Operesheni za Maafa kutoka Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Kanali Selestine Masalamado amesema kuwa ubora wa mpango wa maafa hupimwa kwa uwezo wake wa kutekelezeka na kuleta matokeo chanya kwa wananchi, huku akisisitiza umuhimu wa mipango hiyo kuzingatia mazingira halisi, rasilimali zilizopo na uwezo wa taasisi husika.

“Mradi huu unaofadhiliwa na Zayed Sustainability Prize kupitia Taasisi ya Open Map Development Tanzania (OMDTZ), kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – Idara ya Usimamizi wa Maafa, umekuja wakati sahihi na tunamatarajio makubwa katika kuleta matokeo chanya kuhakikisha tunaimarisha masuala ya usimamizi wa maafa nchini, ”alisema Kanali Masalamado

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa OMDTZ, Bw. Innocent Maholi, alisema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya maafa kupitia matumizi ya teknolojia, uchoraji ramani shirikishi na uwekezaji katika mifumo ya tahadhari ya mapema katika maeneo hatarishi.

Naye Mratibu wa Maafa wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Gerald Sondo, amepongeza ushirikiano huo akieleza kuwa mipango hiyo itasaidia kuongeza utayari wa jamii, kuboresha uratibu wa mwitikio wa dharura na kupunguza athari za mafuriko katika Jiji la Dar es Salaam.

“Kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita, kamati za usimamizi wa maafa katika kata husika zimefanya tathmini ya vihatarishi, kubainisha njia za uokoaji na maeneo salama, kuandaa mifumo ya mawasiliano na uratibu pamoja na kupendekeza hatua za tahadhari ya mapema zinazoshirikisha jamii,”alisema Bw. Sondo.

Aliongezea kuwa, Mipango iliyothibitishwa itatumika kama mwongozo wa vitendo kwa jamii kabla, wakati na baada ya maafa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usalama wa wananchi na ustahimilivu dhidi ya mafuriko na majanga mengine.





Vijana wa Kikundi cha Kigamboni Vijana Unity wamepata fursa mpya ya kujiajiri baada ya Benki ya NMB kukabidhi bajaji tano zenye thamani ya Sh60 milioni, huku ikisisitiza kuwa nidhamu ya marejesho ndiyo itakayofungua milango ya mikopo kwa maelfu ya vijana wengine nchini.

Akikabidhi bajaji hizo jijini Dodoma Ijumaa, Juni 12, 2026, Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Amos Mubusi, alisema mikopo hiyo imetolewa kupitia ushirikiano kati ya benki na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa vikundi vilivyochaguliwa, kupatiwa mafunzo na kuthibitishwa kukidhi vigezo. Alisema NMB imekwishatoa zaidi ya Sh3 bilioni kwa vikundi 304 nchini, huku Sh228 milioni zikitolewa kwa vikundi 19 katika Jiji la Dodoma.

Mwenyekiti wa kikundi hicho, Antery Nestory, alisema wanachama wamejipanga kuhakikisha fursa hiyo haipotei baada ya kuwezeshwa bila kuweka dhamana ya mali. “Safari yetu ya kujenga maisha bora imeanza. Tutalindwa na nidhamu, utii wa masharti ya mkopo na usimamizi mzuri wa mapato,” alisema. Dodoma ni miongoni mwa halmashauri 10 zinazotekeleza awamu ya majaribio ya mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Dodoma ni miongoni mwa halmashauri 10 zinazotekeleza awamu ya majaribio ya mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.







Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kuthamini na kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi katika sekta ya elimu kutokana na mchango wake mkubwa kwenye kuongeza ubora wa elimu na kuandaa rasilimali watu yenye maarifa, ujuzi na maadili yanayohitajika katika maendeleo ya Taifa.

Dkt. Mwigulu amesema hayo alipokuwa Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 11 ya wahitimu wa Kidato cha Nne (Year 11–IGCSE) wa mwaka wa masomo 2025/2026 ya Shule ya Kimataifa ya Feza yaliyofanyika Salasala, Dar es Salaam, leo Ijumaa, Juni 12, 2026.

"Nimekuja leo kwa kuwa Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatambua ubia huu muhimu ambao shule yenu imekuwa ikifanya katika sekta ya elimu. Hatuwezi kuyataja mafanikio katika sekta ya elimu bila kutaja mchango wa shule za sekta binafsi, na kwa umuhususi shule za Feza," amesema Dkt. Mwigulu.

Amesema Taasisi ya Feza ni miongoni mwa taasisi zilizochangia kwa kiasi kikubwa mageuzi ya elimu nchini kwa kuweka viwango vya juu vya ubora wa elimu vinavyotambulika ndani na nje ya Tanzania.

"Hatungeweza kutaja mabadiliko na mageuzi makubwa yaliyofanyika katika sekta ya elimu bila kutaja mchango wa shule za Feza. Mmekuwa chachu ya mageuzi makubwa yaliyofanyika katika sekta ya elimu," amesema.

Aidha, Waziri Mkuu ameipongeza Taasisi ya Feza kwa kuendelea kuvutia wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali duniani, hatua inayoonesha kiwango cha ubora wa elimu inayotolewa na taasisi hiyo.

"Sina shaka nyote mtakubaliana nami kuwa viwango vya ubora wa shule hizi vimekuwa chachu ya kuvutia wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo India, Uturuki, China, Falme za Kiarabu, Lebanon, Somalia, Marekani na nchi nyingine," amesema.

Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kutekeleza mageuzi mbalimbali katika sekta ya elimu ili kuhakikisha mfumo wa elimu unaendana na mahitaji ya sasa ya dunia pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Amesema mojawapo ya hatua hizo ni utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, inayolenga kuimarisha upatikanaji wa elimu bora na kufanya elimu ya lazima kuwa ya miaka 10.

"Tumeyafanya mageuzi haya kwa kuzingatia mabadiliko makubwa yanayotokea duniani na kwa lengo la kuwaandaa vijana wa Kitanzania kukabiliana na changamoto na fursa za dunia ya sasa," amesema.

Sambamba na hilo, Dkt. Mwigulu ameipongeza Taasisi ya Feza kwa mchango wake katika utekelezaji wa miradi ya uwajibikaji kwa jamii ikiwemo kusaidia wanafunzi wenye uhitaji, kuboresha miundombinu ya shule za umma na kuchimba visima vya maji katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumzia nafasi ya elimu katika maendeleo ya Taifa, Waziri Mkuu amesema uwekezaji katika rasilimali watu ndiyo msingi wa maendeleo endelevu ya nchi yoyote duniani.

"Hakuna nchi yoyote iliyowahi kuendelea bila kuwekeza katika rasilimali watu ya kiwango cha juu. Hizi rasilimali nyingine zinaweza zisiwepo, lakini ukiwa na watu wenye maarifa, ujuzi na maadili unaweza kujenga Taifa lenye maendeleo makubwa," amesema.

Aidha, amewataka wahitimu kuendelea kuwa na nidhamu, kutumia maarifa waliyojifunza kwa manufaa ya jamii na Taifa, pamoja na kutumia mitandao ya kijamii kwa tija.

"Mkawe mabalozi wazuri wa mafunzo mliyoyapata hapa. Mafanikio ya kweli hayatapimwa kwa matokeo ya mitihani pekee, bali kwa aina ya watu mtakaokuwa baada ya hapa," amesema.





Na Chalila Kibuda, Michuzi TV

Chama cha Wafanyakazi wa Ukusanyaji wa Mapato Tanzania (TAREWU) kimesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano wa miaka mitano na kampuni ya BodyMind Insight (BMI) kwa lengo la kuimarisha afya ya akili, ustawi wa kisaikolojia na maendeleo ya wafanyakazi nchini.

Hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo imefanyika katika ofisi za BMI jijini Dar es Salaam, ambapo viongozi wa pande zote mbili walisisitiza umuhimu wa kuweka afya ya akili katika nafasi ya juu ndani ya mazingira ya kazi.

Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo, Katibu Mkuu wa TAREWU, Dkt. Michael Marere, alisema chama hicho kimeamua kuweka kipaumbele katika kulinda afya ya akili na ustawi wa wanachama wake ili kuongeza ufanisi kazini na kuboresha maisha yao kwa ujumla.

Alisema kupitia ushirikiano huo, wanachama wa TAREWU watapata elimu kuhusu afya ya akili, ustawi wa kisaikolojia na mbinu za kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kuathiri utendaji wao wa kazi.

“Makubaliano haya yatadumu kwa kipindi cha miaka mitano na yanaweza kuongezwa baada ya muda huo kuisha kulingana na mafanikio yatakayopatikana,” alisema Dkt. Marere.

Aliongeza kuwa afya ya akili imekuwa suala muhimu katika mazingira ya kazi ya kisasa na inahitaji kupewa uzito sawa na afya ya mwili kutokana na mchango wake katika kuongeza tija na ubunifu kazini.

“Wafanyakazi wenye afya bora ya akili huongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao na kuchangia maendeleo ya taasisi pamoja na taifa kwa ujumla. Katika mazingira ya kazi yanayobadilika kwa kasi, ni muhimu kuwawezesha wafanyakazi kujenga ustahimilivu wa kukabiliana na changamoto za maisha na kazi,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa BMI, John Ambrose, alisema afya ya akili ndiyo msingi wa mafanikio ya mtu binafsi na taasisi, akisisitiza umuhimu wa kujenga mazingira salama yanayozingatia ustawi wa wafanyakazi.

Ambrose alisema changamoto za afya ya akili zinaendelea kuongezeka duniani, huku ripoti ya Afya ya Akili Mahali pa Kazi ya mwaka 2026 ikionyesha kuwa asilimia 61 ya wafanyakazi wameongeza matumizi ya likizo zinazohusiana na afya ya akili mwaka huu.

Aliongeza kuwa asilimia 36 ya wafanyakazi duniani wanakabiliwa na matatizo ya usingizi, hali inayotajwa kuwa miongoni mwa changamoto kubwa za afya ya akili zinazowaathiri wafanyakazi wengi huku viongozi wengi wa taasisi wakikosa uelewa wa kutosha kuhusu tatizo hilo.

Aidha, alisema mzigo wa mikopo kutoka taasisi za kifedha umeendelea kuwa chanzo kingine cha msongo wa mawazo na changamoto za afya ya akili kwa wafanyakazi na makundi mbalimbali ya jamii.

Ambrose alisema ushirikiano kati ya BMI na TAREWU utasaidia kuongeza uelewa wa masuala ya afya ya akili na kuweka mifumo bora ya kusaidia wafanyakazi kuwa na ustawi unaochochea maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taasisi kwa ujumla.

Mkuugenzi wa BodyMind Insight Dkt.John Ambrose akizungumza namna watavyotoa huduma kwa wanachama wa TAREWU kuhusiana Afya ya Akili na Saikolojia katika maeneo ya kazi

Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Ukusanyaji Mapato Tanzania (TAREWU) Dkt.Michael Marere akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana TAREWU kuingia makubaliano na BodyMind Insight (BMI) kwa ajili ya wanachama wao kupata elimu ya afya ya akili na Saikolojia .
Hati zikioneshwa mara baada ya kusaini makubaliano baina ya Taasisi hizo mbili.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Ukusanyaji Mapato Tanzania (TAREWU) Dkt.Michael Marere na Mkurugenzi wa BodyMind Insight (BMI) Dkt.John Ambrose wakisaini hati za makubaliano katika hafla iliyofanyika Ofisi za BMI jijini Dar es Salaam.

-Ni inayozungumzia usafirishaji dawa za kulevya katika vyombo vya usafiri


Na Said Mwishehe,Michuzi TV

FILAMU iliyopewa jina la Kifurushi ambayo inalenga kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu mapambano dhidi ya dawa za kulevya imezinduliwa rasmi na itakuwa inaoneshwa katika mabasi yote yanayosafiri mikoa mbalimbali nchini.

Akizungumza leo Juni 12,2026 katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli kilichopo Mbezi jijini Dar es Salaam Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema mamlaka hiyo ilifanya majadiliano na LATRA na Bodi ya Filamu Tanzania na kuona umuhimu wa kuandaa filamu itakayooneshwa katika mabasi yote yanayosafiri mikoa kmbalimbali nchini.

Amesema hatua hiyo ni kama moja ya njia ya kutoa elimu kwa jamii ili kuzuia athari zinazoweza kusababishwa na usafirishaji wa dawa za kulevya.Filamu hiyo fupi imeandaliwa kuonesha uhalisia wa namna ambavyo mtu anaweza kuingia kwenye mtego wa kuwa sehemu ya wahalifu, kusafirisha dawa za kulevya kwa kubeba.

“Au kusafirisha mzigo auvifurushi asivyovifahamu pamoja na kutambua madhara ya kijamii na kiuchumi yanayoweza kujitokeza kutokana na kitendo hicho.Ni kwa msingi huo tumekuja na ‘’Kaulimbiu isemayo, Usafiri Salama bila dawa za kulevya.

Aidha amesema filamu hiyo inalenga kuongeza uelewa kwa madereva,makondakta, wahudumu wa mabasi, wasafirishaji wa mizigo, abiria na wananchi kwa ujumla kuhusu wajibu wao katika vita dhidi ya dawa za kulevya kwa kutoa taarifa za vitendo vinavyohusiana na usafirishaji wa dawa za kulevya.

Akieleza zaidi kuhusu sababu za kuja na filamu hiyo amesema dawa za kulevya ni tishio kubwa kwa afya za wananchi, ustawi wa familia, usalama wa jamii na maendeleo ya taifa letu na kwamba madhara ya dawa za kulevya yanachangia kuongezeka kwa changamoto za kiafya, uhalifu, kuzorota kwa familia, uvunjifu wa amani, pamoja na kudhoofika kwa nguvu kazi ya taifa, hususan vijana na hatimaye huathiri maeneo muhimu ya kiuchumi.

“Kutokana na athari hizo, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi thabiti wa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti biashara na matumizi ya dawa za kulevya.”

Amefafanu hatua hizo zinajumuisha operesheni za ukamataji, tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya, uchunguzi wa makosa ya dawa za kulevya pamoja na utoaji wa elimu kwa umma ili kujenga uelewa na ushiriki wa wananchi katika mapambano haya.

Ameongeza pia kwa siku za hivi karibuni, Mamlaka imeendelea kubaini mbinu mbalimbali zinazotumiwa na wahalifu kusafirisha dawa za kulevya ikiwemo kupitia vyombo vya usafiri wa umma.

“Mara nyingi dawa hizo hufichwa kwenye mizigo na vifurushi vinavyoonekana kuwa vya kawaida.Baadhi ya wananchi, abiria na hata wahudumu wa ndani ya vyombo vya usafiri wamejikuta wakihusishwa na makosa ya dawa za kulevya baada ya kubainika kubeba mizigo wasiyoifahamu.

“Ninitumie fursa hii kuwaomba wamiliki wa mabasi, makampuni ya usafirishaji na wadau wote wa sekta ya usafiri kuipokea na kuipa kipaumbele filamu hii kwa kuhakikisha inaoneshwa katika vyombo vyao vya usafiri.

“Ushirikiano wenu utasaidia kuwafikia kwa haraka wananchi wengi kila siku na kufanya kila safari kuwa fursa ya kutoa elimu na kuimarisha usalama wa jamii dhidi ya tatizo la dawa za

kulevya.Tumechagua kuzindua filamu hii hapa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli kwa sababu ni moja ya kituo kikubwa zaidi nchini kinachohudumia maelfu ya wasafiri kila siku.”

Aidha ametumia nafasi hiyo kutoa ujumbe kwa jamii ya Watanzania kwamba “Usikubali kubeba mzigo, kifurushi au bidhaa yoyote usiyoifahamu. Hakikisha unatambua unachobeba, kinatoka kwa nani na kinaelekea kwa nani. Kifurushi unachodhani ni cha kawaida kinaweza kubeba dawa za kulevya na kubadili maisha yako kwa matokeo hasi”.

Ameongeza kwa pamoja tunaweza kuzuia usafirishaji wa dawa za kulevya, kulinda vijana wetu, kuimarisha usalama wa jamii na kujenga Taifa lenye afya, nguvu kazi salama na maendeleo endelevu kupitia ujumbe uliopo kwenye filamu hiyo.





KUTOKA VUNJO.

KATIKA kuhakikisha kuwa wananchi wa Jimbo la Vunjo wanakabiliana na tatizo la uhaba wa ajira kwa kujiajiri wenyewe, Mbunge wa jimbo hilo Enock Koola amekuja kampeni maalum ya kuwafundisha wananchi ufugaji wa ng'ombe wa maziwa pamoja na samaki.

Mafunzo hayo yanayotarajiwa kutolewa kesho Juni 13 mwaka huu katika ukumbi wa shule ya viziwi kata ya njia panda.

Mafunzo hayo yatawasidia wananchi kujiajiri kupitia ufugaji wenye faida na kuwawezesha vijana kupata fursa ya ajira.

Hili ni mwendelezo wa juhudi za Mbunge Enock Koola ya kuhakikisha anainua uchumi wa wananchi wa jimbo hilo ambapo hapo awali alikuja na mkakati wa kufufua zao la kahawa kwa kuleta miche bora na ya kisasa kwa maeneo yanayolima zao hilo.

Katika kampeni ya miche bora ya miparachichi jumla ya vijana 60 walinufaika katika jimbo hilo, elimu ya ufugaji nyuki vijana 80 walinufaika, huku upande wa uvuvi na ufugaji ng'ombe vijana 80 watanufaika kutoka kila kata ili kwenda kutoa elimu kwa wananchi na vijana wengine.




Na Mwandishi Wetu

Baraza la Ushindani Halali Zanzibar (ZFCT) limefanya ziara ya mafunzo katika Tume ya Ushindani ya Haki (FCC) kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu katika masuala ya ushindani wa biashara, udhibiti wa bidhaa bandia pamoja na usimamizi wa mashauri yanayohusiana na ushindani.

Ziara hiyo iliyofanyika katika ofisi za FCC Juni 10, 2026 Jijini Dar es Salaam, imeelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao na kuhakikisha mazingira ya biashara yanakuwa ya haki kwa wadau wote.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa alisema kuwa kubadilishana uzoefu na taasisi za ndani ya nchi ni muhimu katika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa ushindani na kulinda maslahi ya watumiaji dhidi ya vitendo vinavyokiuka sheria za ushindani na biashara.

Alisema ujumbe wa ZFCT unapata fursa ya kujifunza namna FCC inavyotekeleza majukumu yake ya kudhibiti vitendo vya ushindani usio wa haki, kukabiliana na biashara ya bidhaa bandia pamoja na mifumo ya uchunguzi na uendeshaji wa mashauri mbalimbali yanayofikishwa mbele ya taasisi hiyo.

Kwa upande wake, ujumbe wa ZFCT ukiongozwa na Msajili wa Baraza, Bi. Fatma Yahya alieleza kuridhishwa na mafunzo na uzoefu uliopatikana katika ziara hiyo, ukibainisha kuwa utaisaidia taasisi hiyo kuimarisha utendaji wake katika kushughulikia rufaa na mashauri yanayohusiana na ushindani wa biashara Zanzibar.

ZFCT ni chombo kinachoshughulikia mashauri na rufaa zinazotokana na maamuzi ya mamlaka za ushindani, ambapo wadau wasiokubaliana na maamuzi yaliyotolewa huwasilisha kesi zao kwa ajili ya kusikilizwa na kutolewa uamuzi.

Ziara hiyo pia ilitoa nafasi kwa wataalamu kutoka pande zote mbili kujadiliana changamoto na fursa zilizopo katika usimamizi wa ushindani wa biashara, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana katika kujenga uwezo wa kitaasisi na kuimarisha utekelezaji wa sheria zinazolinda ushindani wa haki katika soko.

Top News