MAHAKAMA ya Rufani Tanzania imetupilia mbali ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) lililotaka kuruhusiwa kuwasilisha ushahidi wa nyongeza katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, na hivyo kuacha uamuzi wa Mahakama Kuu ukiwa palepale.

Uamuzi huo ulitolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani lililoundwa na Jaji Augustine Mwarija, Jaji Zahara Muruke na Jaji Amour Khamisi, ambao walikubaliana na uamuzi wa awali wa Mahakama Kuu uliotolewa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiana na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Akisoma hukumu, Jaji Mwarija alisema hoja kuu ilikuwa kubaini kama Mahakama Kuu ilikosea kwa kujadili na kukataa notisi ya ushahidi wa nyongeza bila kuipa Jamhuri nafasi ya kusikilizwa, lakini Mahakama ya Rufani ilibaini kuwa upande wa mashtaka ulipewa fursa ya kutosha kueleza msimamo wake.

Mahakama ilieleza kuwa notisi ya Jamhuri ililenga kuongeza maelezo ya ushahidi wa ACP Amini Mahamba kuhusu uchunguzi wa matukio ya Oktoba 29, 2025, maelezo ambayo hayakusomwa wakati wa mwenendo wa kupeleka shauri Mahakama Kuu (committal proceedings).

Hata hivyo, Lissu alipinga hatua hiyo akidai kuwa kifungu cha 308 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai hakiruhusu kuwasilishwa kwa ushahidi mpya kutoka kwa shahidi ambaye tayari ushahidi wake ulishawasilishwa wakati wa committal, bali kinahusu mashahidi ambao taarifa zao hazikusomwa kabisa.

Mahakama ya Rufani ilikubaliana na tafsiri hiyo, ikisema kifungu hicho kinatoa nafasi ya kumwita shahidi ambaye taarifa yake haikusomwa wakati wa committal, lakini hakitoi mamlaka ya kumrejesha shahidi aliyekwisha kutoa ushahidi ili kuongeza ushahidi mpya alioupata baadaye.

Kutokana na tafsiri hiyo, Mahakama ilisema notisi ya Jamhuri ilikuwa imewasilishwa kwa msingi usio sahihi wa kisheria na kwamba Mahakama Kuu ilikuwa sahihi kuifuta kwa kuwa haikukidhi matakwa ya kifungu cha 308 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Katika uamuzi huo, Mahakama pia ilikataa ombi la Lissu la kulipwa fidia kwa madai ya kukaa mahabusu kwa siku 139 kutokana na kusimamishwa kwa mwenendo wa kesi wakati maombi hayo yalipokuwa yakisikilizwa.

Jaji Mwarija alisema Mahakama ya Rufani haina mamlaka ya kushughulikia ombi hilo kwa kuwa si Mahakama ya kwanza kusikiliza shauri, akifafanua kuwa fidia ya aina hiyo inaweza kutolewa tu endapo mshtakiwa ataachiwa huru na kubainika kuwa shtaka lilikuwa la kipuuzi au la kumsumbua bila sababu.

Kutokana na sababu hizo, Mahakama ya Rufani ilihitimisha kuwa ombi la DPP halikuwa na msingi wa kisheria na hivyo likatupiliwa mbali, hatua inayomaanisha uamuzi wa Mahakama Kuu wa kuzuia kuwasilishwa kwa ushahidi huo wa nyongeza unabaki kuwa halali.

Na Janeth Raphael - MichuziTv

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali itaendelea kuimarisha maridhiano ya kisiasa kama msingi wa kuendeleza mchakato wa maboresho ya Katiba, huku akisisitiza kuwa hatua zote zitafanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi kwa maslahi mapana ya Taifa.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Julai 30, 2026, alipokutana na viongozi wa vyama 18 vya siasa nchini katika Ikulu ya Dar es Salaam, kwenye mkutano uliolenga kujadili masuala ya maridhiano ya kisiasa, mageuzi ya kisiasa, uchumi, huduma za jamii, ajira, uwekezaji na ulinzi wa amani nchini.

Akizungumza katika mkutano huo, Rais Samia alisema Serikali imejipanga kuendelea kushirikiana na vyama vya siasa ili kuhakikisha mchakato wa maridhiano unazaa matokeo yenye manufaa kwa Taifa, ikiwa ni pamoja na kufungua njia kuelekea hatua zinazofuata za maboresho ya Katiba.

Aidha, amewafahamisha viongozi hao kuhusu hatua zilizofikiwa katika maandalizi ya mchakato wa maridhiano visiwani Zanzibar, akieleza kuwa Serikali itaendelea kusimamia mchakato huo kwa uwazi na kwa kuzingatia misingi ya kisheria.

Rais Samia pia alitangaza kuwa Serikali itaendelea kufanya mikutano ya mazungumzo na viongozi wa vyama vya siasa angalau mara tatu kwa mwaka, akisema hatua hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano, kujenga uelewano na kutatua changamoto mbalimbali kupitia majadiliano.

Mbali na masuala ya kisiasa, Rais Samia alielezea hali ya uchumi wa nchi, akisema Tanzania imeendelea kushuhudia ukuaji wa uchumi wa asilimia sita katika mwaka uliopita, huku ukuaji wa asilimia 6.3 ukitarajiwa kufikiwa mwaka huu.

Amesema Serikali inaendelea kuweka mkazo katika kukamilisha miradi mikubwa ya maendeleo iliyoanza kutekelezwa pamoja na kuwekeza zaidi katika miundombinu ya kimkakati, ikiwemo reli, barabara, bandari na sekta nyingine muhimu kwa maendeleo ya uchumi.

Kuhusu uwekezaji, Rais Samia alisema maboresho yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam yameongeza uwezo wa bandari hiyo kuhudumia biashara ya ndani na kikanda, huku Serikali ikiendelea kupanua na kuboresha shughuli za bandari za Bahari ya Hindi pamoja na zile za maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.

Aidha, amewataka viongozi wa vyama vya siasa kushirikiana katika kulinda amani, umoja na maslahi ya Taifa, akisisitiza kuwa ulinzi wa Tanzania ni jukumu la pamoja linalohusisha Serikali, vyama vya siasa na wananchi wote.

Katika mkutano huo, viongozi wa vyama vya siasa waliwasilisha maoni na mapendekezo yao kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi. Serikali iliahidi kuendelea kuyapokea na kuyafanyia kazi kupitia majukwaa rasmi ya majadiliano na mifumo ya maamuzi.

Mkutano huo ni wa pili kuitishwa na Rais Samia tangu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Mkutano wa kwanza ulifanyika Machi 31, 2026, Ikulu ya Dar es Salaam, ukiwakutanisha wagombea wa urais na wagombea wenza kutoka vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi huo.






Na Janeth Raphael - MichuziTv

Watendaji wa Serikali za Mitaa nchini wamehimizwa kutenganisha majukumu yao ya kiutumishi na shughuli za kisiasa ili kulinda weledi, uadilifu na kutenda haki kwa wananchi, hatua itakayosaidia kuimarisha imani ya umma kwa Serikali pamoja na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma.

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Watendaji wa Serikali za Mitaa Tanzania (UWATA), Frank Kalinga, wakati wa uzinduzi rasmi wa umoja huo uliofanyika jijini Dodoma.

Kalinga amesema hadhi na heshima ya watendaji wa Serikali za Mitaa inategemea namna wanavyotekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma, huku wakiepuka kuchanganya wajibu wao wa kitaaluma na shughuli za kisiasa.

Amesisitiza kuwa watendaji ni kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi katika ngazi za msingi, hivyo wanapaswa kujenga mazingira ya kuaminika kupitia utendaji wenye uwazi, uwajibikaji na usio na upendeleo.

"Ni muhimu kila mdau kuheshimu mipaka ya mamlaka na majukumu yaliyoainishwa kisheria ili kuimarisha uwajibikaji na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi," amesema Kalinga.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Sospeter Mtwale, amesema kuanzishwa kwa UWATA ni hatua muhimu itakayosaidia kuimarisha uwezo wa watendaji wa Serikali za Mitaa, kukuza maadili ya utumishi wa umma na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa sera pamoja na miradi ya maendeleo katika ngazi za kata, vijiji na mitaa.

Mtwale amewataka watendaji kuendelea kuzingatia misingi ya utawala bora, uzalendo, uwajibikaji na usimamizi makini wa rasilimali za umma ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Ameeleza kuwa watendaji wana nafasi ya kipekee katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwamba usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo utachangia kuleta matokeo chanya, kuongeza thamani ya fedha za umma na kuharakisha maendeleo katika jamii.











NA: MWANDISHI WETU


Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa, na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu (MCC), Mary Chatanda, amebadilishwa mkoa wa ulezi wa kichama na sasa ni mlezi wa CCM mkoa wa Mara.

Mabadiliko hayo yamefanyika Julai 29, 2026, Zanzibar, kufuatia vikao vya Chama vinavyoendelea. Kabla ya mabadiliko hayo, Chatanda alikuwa mlezi wa mikoa ya Mjini na Magharibi, Zanzibar.

Akizungumzia mabadiliko hayo, Chatanda amekishukuru Chama chake kwa kuendelea kumuamini kutekeleza majukumu mbalimbali ya kichama.

"Nimepokea taarifa hii ya mabadiliko ya ulezi wa Chama mkoa kwa moyo wa unyeyekevu. Nakishukuru Chama changu kwa kuniamini. Niwaombe wanachama wenzangu na wananchi kwa ujumla tushirikiane kuhakikisha tunasukuma mbele gurudumu la maendeleo na Chama chetu".

Ameongeza kuwa "Serikali ya CCM chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imepeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo mkoani Mara, ni wajibu wetu kuhakikisha fedha hizo zinatumika kama ilivyokusudiwa katika kuboresha maisha ya wananchi". 

Akiwa mlezi mkoani humo, pamoja na mambo mengine, Chatanda anawajibika kuwaunganisha wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla.

Aidha, kuimarisha uhai wa Chama, kuongeza idadi ya wanachama na kuhimiza utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Vilevile, anawajibika kujenga uhusiano mzuri baina ya Chama na serikali.

Mkoa wa Mara unaundwa na wilaya za Bunda, Butiama, Musoma, Rorya, Serengeti na Tarime.



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Mjumbe wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) na Kaimu Meneja wa Huduma za Kiswahili wa Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN), Mgaya Kingoba, amesema uhuru wa kutoa maoni una mipaka ya kisheria na kimaadili, hivyo haupaswi kutumiwa kutoa matusi, kudhalilisha wengine, kuchochea chuki au kusambaza taarifa zisizo sahihi.

Kingoba amesema hayo leo, Julai 30, 2026, alipowasilisha mada kuhusu “Kuimarisha Uzalendo katika Uandishi wa Habari ili Kulinda Amani, Umoja na Mshikamano” katika siku ya pili ya mafunzo kwa watumishi wa Bongo FM, redio dada ya TBC (Shirika la Utangazaji Tanzania), yaliyofanyika katika Ofisi za JAB jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 29, 2026.

Amesema ukosoaji ni sehemu muhimu ya uhuru wa kujieleza, lakini unapaswa kulenga kuonesha kasoro na kuchochea maboresho badala ya kushambulia watu, kutumia lugha ya kejeli au kubomoa imani ya jamii kwa taasisi.

“Mkosoaji mzalendo hafichi makosa, lakini pia hatumii matusi, kejeli au upotoshaji. Anakosoa kwa ukweli, ushahidi na lugha ya staha, akiwa na lengo la kujenga na kuboresha,” amesema Kingoba.

Ameeleza kuwa mkosoaji mzalendo hujenga ukosoaji wake katika misingi ya ukweli, ushahidi, muktadha, lugha ya staha, maslahi ya umma na mapendekezo ya suluhisho.

Aidha, amewataka watangazaji kutambua kuwa uhuru wa kujieleza hauondoi wajibu wao wa kulinda utu wa watu, amani na mshikamano wa kitaifa.

Kingoba amesema uzalendo katika utangazaji hauishii katika kuipenda nchi kwa maneno, bali unapaswa kuonekana katika maamuzi ya kitaaluma yanayolinda ukweli, umoja, amani na maslahi ya Taifa na kwamba uchaguzi wa maneno na namna ya kuendesha mijadala ya moja kwa moja unaweza kujenga jamii au kusababisha migawanyiko.

Akiwasilisha mada kuhusu Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, amesema Sheria hiyo inatambua uhuru wa Waandishi wa Habari na vyombo vya habari katika kutafuta, kuhariri, kuchapisha na kutangaza habari, lakini inaweka pia wajibu wa kuzingatia sheria, maadili, weledi na haki za wengine.

Amesema uhuru wa habari na uwajibikaji vinapaswa kwenda pamoja ili kulinda taaluma, maslahi ya jamii na Taifa.

Mafunzo hayo yanalenga kuwaongezea washiriki uelewa kuhusu Sheria ya Huduma za Habari, maadili ya uandishi wa habari, uzalendo na wajibu wa watangazaji katika kutumia uhuru wa kujieleza kwa weledi na uwajibikaji.













Na George Maziku, Nyang'hwale


MGODI wa wachimbaji wadogo wa dhahabu wa Mwamakiliga, unaopatikana Kijiji cha Mwamakiliga, kata ya Izunya, wilaya ya Nyang'hwale, Mkoani Geita umewawezesha zaidi ya watanzania 6000 kujiajiri kwenye kazi mbalimbali mgodini hapo na kujipatia kipato.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mgodini hapo, Meneja msaidizi wa mgodi huo Mashaka Kulwa Chitela amesema wananchi kutoka ndani na nje ya wilaya ya Nyang'hwale na mkoa wa Geita wamenufaika kwa kujipatia kazi mbalimbali.

Amesema kuwa wananchi hao wanajishughulisha na kazi za uchimbaji, uokotaji wa mawe ya dhahabu(maarufu ukwale), biashara ya mitambo ya kusaga mawe (crushers), ubebaji wa mifuko ya mawe, boda boda, mama lishe, biashara ya nyumba za kupangisha, maduka, na nyingine nyingi.

"Mgodi wetu umeisaidia sana serikali katika kupunguza idadi ya watanzania wasio na ajira, hapa kuna umati wa zaidi ya watu 6000 wanaojipatia riziki zao za Kila siku. Wapo wachimbaji, kina mama wa ukwale, makago wanaobeba na kupakia mifuko ya mawe, boda boda, mama lishe, wenye gesti, maduka na wafanyabiashara wengine wengi", amesema Chitela.

Ameongeza kuwa, "Tumetengeneza ajira za uhakika zaidi ya 100 katika kada za ukaguzi, ulinzi, ulipuaji na uhudumu wa ofisi. Tuna imani kubwa kwamba tukipata leseni ya uchimbaji tutazalisha ajira Nyingi zaidi."

Amebainisha miongoni mwa watu walionufaika na mgodi huo ni wakazi wa kijiji cha Mwamakiliga na kata ya Izunya ambao wamekuwa wakipewa kipaumbele katikà nafasi mbalimbali za kazi zinazojitokeza mgodini hapo.

" Tumekuwa na upendeleo maalum kwa wananchi wa kijiji hiki ambao ni wenyeji wetu, walinzi wengi wa mgodi wetu wanatoka hapa Mwamakiliga. Pia tumechukua vijana 25 wa hapa kijijini na Kisha kuwafundisha kazi ya ukaguzi wa migodi", amesitiza Chitela.

Amefafanua mbali na kuzalisha ajira hizo, mgodi wake umekuwa chanzo cha uhakika cha mapato ya halmashauri ya wilaya ya Nyang'hwale kupitia ushuru mbalimbali ikiwemo ushuru wa huduma.

Amesema hata Serikali kuu imekuwa ikinufaika na uwepo wa mgodi huo kupitia malipo ya mrabaha, ambayo ni asilimia 3 kwa kila mifuko 100 ya mawe yenye dhahabu.

"Serikali imetuamini na kutukabidhi jukumu la kusimamia na kukusanya mapato yake katika mgodi huu, kazi hiyo tumekuwa tukiifanya kwa uaminifu mkubwa. Halmashauri yetu ya Nyang'hwale na serikali kuu wote wanapata mapato yao bila ubabaishaji", amebainisha Chitela.

Kuhusu usalama wa mgodi wake kwa wachimbaji na watu wengine wanaofanya kazi mgodini hapo, Chitela amesema suala la usalama kwao ni kipaumbele namba moja, na kwamba mgodi huo haujawahi kupata ajali yoyote kubwa kutokana na umakini wao mkubwa katika usalama.

"Mgodi wetu ni salama kabisa, kwetu suala la usalama ni kipaumbele cha kwanza na idara yetu ya ukaguzi ina watu wa kutosha na makini. Ukaguzi wa duara unafanyika wakati wote mchana na usiku, masaa 24 na mara ikibainila kama duara fulani ni hatarishi, tunasimamisha moja uchimbaji mpaka marekebisho yafanyike",amesema.






Victor Masangu,Bagamoyo


Mwenyekiti wa Jumuiya ya ya Wazazi Taifa Ndg. Fadhili Maganya amewasa viongozi wa CCM kuhakikisha kwamba wanavalia njuga na kusimamia ipasavyo suala la mikopo ya asilimia kumi ambayo inatolewa na Halmashauri.

Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara yake ya kikazi Wilaya ya Bagamoyo yenye lengo la kuona uhai wa chama pamoja na kuimarisha jumuiya zake zote sambamba na tenbelea miradi ya maendeleo.

Mwenyekiti huyo amebainisha kwamba kumekuwepo na baadhi changamoto ya utoaji wa fedha ambazo zinatolewa na mfuko wa Tasaf aziwafikii walengwa na zinakwenda kwa watu wengine ambao hawastahili

"Kuna malalamiko mengi ambayo yamekuwa yakitolewa na wananchi kuhusiana na suala la utoaji wa fedha ambazo zinatolewa na mfuko wa Tasaf zinakwenda kwa watu wengine ambao hawahusiki kabisa,"amebainisha Mwenyekiti huyo.

Kadhalika amesema kwamba fedha za asilimia kumi ambazo zinatolewa kwa ajili ya makundi ya vijana,walemavu na wanawake zinatakiwa kutolewa kwa walengwa na sio kupewa watu wengine.

Akiwa katika chuo cha uuguzi na ukunga Mwenyekiti huyo amewahimiza wanafunzi hao kuzingatia maadili pamoja na kuwa wazalendo na nchi yao.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Shaibu Ndemanga amempongeza Mwenyekiti huyo wa Taifa kwa kufanya ziara hiyo ambayo itaweza kuleta matokeo chanya ya kimaendeleo.

Pia Mkuu huyo wa Wiaya amebainisha kuwa serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 27 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa bandari.

Naye Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo Abubakari Mlawa amebainisha kwamba bado kuna changamoto ya migogoro ya ardhi katika baadhi ya maeneo na kwamba wameshaanza kuifanyia kazi.

Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Subira Mgalu ameamua kutoa kiasi cha shilingi milioni 5 kupitia mfuko wa Jimbo kwa ajili ya kuweza kukarabati miundombinu ya majengo pamoja na uzio katika chuo cha uuguzi na ukunga Bagamoyo.

Mwenyekiti wa wazazi Mkoa wa Pwani Jackson KItuka amesema wataendelea kushirikiana na viongozi mbali mbali wa chama na serikali kwa ajili ya kuleta maendeleo.

Ziara ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi ya CCM Taifa imeendelea katika Wilaya ya Bagamoyo ambapo imetembelea miradi mbali mbali ya maendelo ikiwemo chuo cha uuguzi na ukunga,chuo cha kilimo kaole,kiwanda cha kuchakata taka hatarishi pamoja na miradi mbali ikiwemo Hospitali ya Chalinze na sekta ya elimu.



Na Said Mwishehe, Michuzi TV

SERIKALI kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), Umoja wa Ulaya (EU) na Ubalozi wa Ireland imezindua awamu ya nne ya ufadhili wa masomo ya nishati endelevu kwa wanawake 15 nchini.

Hatua hiyo itafanya idadi ya wanufaika wa mpango wa Women in Sustainable Energy (WISE) kufikia 60 tangu ulipoanzishwa mwaka 2023 kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Nishati na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya nishati.

Akizungumza katika uzinduzi wa dirisha la maombi jijini Dar es Salaam, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Emilian Nyanda, amesema Serikali inawekeza katika maendeleo ya rasilimali watu ili kuhakikisha nchi inakuwa na wataalamu wa kutosha wa kusimamia mabadiliko ya sekta ya nishati.

Amesema Tanzania inaendelea kutekeleza mikakati ya kuongeza uzalishaji wa umeme, kuimarisha matumizi ya nishati jadidifu, matumizi bora ya nishati na ajenda ya nishati safi ya kupikia, lakini mafanikio ya mipango hiyo yanategemea pia upatikanaji wa wataalamu wenye ujuzi.

"Haya si masomo pekee; ni uwekezaji wa moja kwa moja katika wataalamu watakaosimamia sera, teknolojia na ubunifu utakaoiwezesha Tanzania kufikia malengo yake ya maendeleo ya sekta ya nishati," amesema.

Nyanda amesema wahitimu wengi wa awamu tatu zilizopita tayari wamepata ajira katika Wizara ya Nishati, TANESCO, taasisi za utafiti na kampuni binafsi, huku wengine wakianzisha biashara zinazotoa huduma za kitaalamu katika sekta hiyo.

Amefafanua programu hiyo pia inaunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia na mpango wa Mission 300 unaolenga kuongeza upatikanaji wa umeme kwa Waafrika milioni 300 ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande wake, Meneja wa Maendeleo ya Vipaji wa UNDP Tanzania, Veronica Sigala, amesema mpango wa WISE unalenga kuwawezesha wanawake vijana kupata elimu ya juu na ujuzi wa kitaalamu utakaowawezesha kushiriki kikamilifu katika mabadiliko ya sekta ya nishati.

Amesisitiza mpango huo unachangia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), ikiwemo elimu bora, usawa wa kijinsia, nishati safi na nafuu, ajira zenye staha na hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

"Tanzania haiwezi kufanikisha mabadiliko ya sekta ya nishati kupitia miundombinu, sera na fedha pekee. Tunahitaji watu wenye ujuzi, na wanawake lazima wawe miongoni mwa wahandisi, watafiti, wabunifu na viongozi wa mabadiliko hayo," amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam(DIT), Profesa Preksedis Ndomba, amesema programu hiyo inaendana na maono ya taasisi ya kutumia elimu, utafiti na ubunifu kutatua changamoto za maendeleo ya taifa.

Amesema DIT imeongeza idadi ya wanafunzi wanawake katika taaluma za uhandisi kutoka asilimia 14 mwaka 2016 hadi asilimia 25 kwa sasa, huku ikilenga kufikia asilimia 35 mwaka 2031 na uwiano wa asilimia 50 kwa 50 ifikapo mwaka 2050.

Prof.Ndomba amesema zaidi ya asilimia 60 ya mafunzo yanayotolewa chuoni hapo ni ya vitendo kupitia mfumo wa Teaching Factory, hatua iliyowezesha zaidi ya asilimia 70 ya wahitimu kupata ajira au kujiajiri ndani ya miezi sita baada ya kuhitimu.

Amewahimiza wanawake wenye sifa kutumia fursa hiyo ya ufadhili, akisema kuongeza ushiriki wao katika sekta ya nishati kutasaidia kuimarisha ubunifu, kuongeza nguvu kazi yenye ujuzi na kuharakisha maendeleo ya uchumi wa Tanzania.






Na. Ramadhani Kissimba, Durban

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimeshauriwa kuimarisha ushirikiano na kuweka mikakati ya pamoja itakayochochea maendeleo ya viwanda pamoja na kuongeza mnyororo wa thamani wa bidhaa zinazozalishwa katika ukanda huo.

Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo TIB, Bw. Deogratius Kwiyukwa, kando ya Mkutano wa 9 wa Wiki ya Viwanda wa SADC (SADC Industrialisation Week) unaoendelea jijini Durban, Afrika Kusini.

Akizungumza kuhusu mijadala ya mkutano huo, Bw. Kwiyukwa alisema moja ya ajenda kuu ni namna nchi wanachama zitakavyowekeza katika viwanda vya kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa ndani ya ukanda wa SADC, hususan madini ya kimkakati (critical minerals), badala ya kuendelea kuuza nje ya nchi madini hayo yakiwa katika hali ghafi.

“Jambo kubwa lililojadiliwa ni namna ya kuyaongezea thamani madini ya kimkakati katika nchi yanakopatikana madini hayo ndani ya ukanda huu kabla ya kuuzwa katika masoko ya nje,” alisema Bw. Kwiyukwa.

Alibainisha kuwa mkutano huo umefungua fursa mpya za ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama, zikiwemo fursa za kuandaa mikakati ya pamoja itakayosaidia kufanikisha malengo ya maendeleo ya viwanda na uchumi yaliyowekwa na SADC.

Aidha, Bw. Kwiyukwa alizishauri nchi wanachama kuhakikisha sera na mipango yao ya maendeleo inaendana na dira na mikakati ya SADC ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye manufaa ya pamoja kwa ukanda huo.

Kwa upande wa Benki ya Maendeleo (TIB), Bw. Kwiyukwa alisema taasisi hiyo imeshiriki katika mkutano huo kwa lengo la kutafuta fursa za kushirikiana na taasisi nyingine za kifedha ndani ya ukanda wa SADC ili kuunganisha mitaji kwa ajili ya kufadhili miradi mikubwa ya maendeleo.

“Kama TIB, tumeshiriki katika mkutano huu kwa lengo la kujenga ushirikiano na taasisi nyingine za kifedha ili kuunganisha mitaji itakayowezesha kufadhili miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa na nchi wanachama wa SADC,” aliongeza Bw. Kwiyukwa.

Vilevile, Bw. Kwiyukwa alisisitiza umuhimu wa nchi wanachama kutafsiri kwa vitendo maazimio ya mkutano huo kwa kuwekeza katika sekta zinazozalisha ajira, hususan kwa vijana, ili waweze kutumia kikamilifu fursa za kiuchumi zinazopatikana ndani ya ukanda wa SADC.

Mkutano wa 9 wa Wiki ya Viwanda wa SADC umewakutanisha viongozi wa serikali, sekta binafsi, wawekezaji, taasisi za kifedha, wataalamu na wadau wa maendeleo kutoka nchi wanachama wa SADC. Mkutano huo unafanyika chini ya kaulimbiu isemayo: “Kukuza Viwanda Imara, Endelevu na Jumuishi kupitia Maendeleo ya Miundombinu, Mageuzi ya Kilimo na Madini kwa Ajili ya Dunia Yenye Haki.”

Kwa ujumla, mijadala ya Mkutano wa Wiki ya Viwanda wa SADC jijini Durban imeweka msisitizo mkubwa katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kuongeza thamani ya rasilimali za madini na bidhaa nyingine kabla ya kuuzwa nje, pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda, miundombinu na miradi ya maendeleo. Hatua hizi zinatarajiwa kuongeza ushindani wa uchumi wa ukanda wa SADC, kuvutia uwekezaji, kuimarisha biashara ya ndani ya ukanda na kuzalisha ajira zaidi, hususan kwa vijana.




Mchumi kutoka Wizara ya Fedha, Bi. Jesca Mboho, akifuatilia kwa makini mijadala inayoendelea katika Mkutano wa 9 wa Wiki ya Viwanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Industrialisation Week), unaofanyika jijini Durban, Afrika Kusini.






Meneja wa Utafiti na Biashara kutoka Benki ya Maendeleo (TIB), Dkt.Hilderbrand Shayo (kushoto), akiwa katika mazungumzo na Afisa Usimamizi Mkuu wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bi. Emerensiana Nyanda (katikati), pamoja na Mchumi kutoka Wizara ya Fedha, Bi. Jesca Mboho, mara baada ya kumalizika kwa vikao vya Mkutano wa 9 wa Wiki ya Viwanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), unaoendelea jijini Durban, Afrika Kusini.






Meneja wa Utafiti na Biashara wa Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB), Dkt. Hilderbrand Shayo, akitoa mchango wake wakati wa mijadala katika Mkutano wa 9 wa Wiki ya Viwanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Industrialisation Week), unaoendelea jijini Durban, Afrika Kusini.






Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo (TIB), Bw. Deogratius Kwiyukwa (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa Mkutano wa 9 wa Wiki ya Viwanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Industrialisation Week), unaofanyika jijini Durban, Afrika Kusini.







Afisa Sheria kutoka Tume ya Ushindani (FCC), Bw. Goerge Chananga akielezea ubora, matumizi na fursa za kiuchumi za mkonge unaozalishwa nchini Tanzania kwa mmoja wa wadau waliotembelea Banda la Tanzania, pembezoni mwa Mkutano wa Wiki ya Viwanda wa SADC (SADC Industrialisation Week 2026), unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (ICC), jijini Durban, Afrika Kusini.



(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha-Durban)






Na Janeth Raphael - MichuziTv

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetangaza mkakati mpya wa kuongeza kasi ya uwekezaji katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kupitia upanuzi wa huduma za kifedha, matumizi ya teknolojia za kisasa na ushirikiano na wadau mbalimba li, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uchumi wa Taifa na kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Julai 30, 2026, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Frank Nyabundege, amesema benki hiyo imejipanga kuongeza mchango wake katika kukuza uzalishaji wa kibiashara kwa kuhakikisha wakulima, wafugaji na wavuvi wanapata mitaji inayowawezesha kuongeza tija, kutumia teknolojia za kisasa na kuwekeza katika shughuli zenye thamani kubwa zaidi.

Amesema mafanikio yaliyofikiwa na TADB katika miaka ya hivi karibuni yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuimarishwa kwa mtaji wa benki kupitia Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hatua ambayo imeongeza uwezo wa taasisi hiyo kuwafikia wanufaika wengi zaidi nchini.

Kwa mujibu wa Nyabundege, ongezeko hilo la mtaji limeiwezesha TADB kuongeza kiwango cha utoaji wa mikopo, ambapo zaidi ya asilimia 73 ya mikopo yote iliyotolewa katika kipindi cha miaka mitano ilitolewa kati ya mwaka 2022 na 2025, jambo linaloonyesha kasi ya ukuaji wa huduma za benki hiyo.

Mbali na mtaji unaotolewa na Serikali, amesema TADB imefanikiwa kuvutia fedha kutoka kwa taasisi mbalimbali za maendeleo duniani, hatua iliyoongeza uwezo wa kufadhili miradi mikubwa ya uzalishaji, uchakataji na uongezaji thamani wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Akizungumzia mwaka wa fedha 2026/2027, Nyabundege amesema benki hiyo itaelekeza nguvu zaidi katika kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa sekta za uzalishaji, kuimarisha minyororo ya thamani ya mazao ya kimkakati, kuongeza ushindani wa bidhaa za kilimo katika masoko ya ndani na nje ya nchi pamoja na kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka mataifa mengine.

Pia amesema TADB itaendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa za kilimo, kufadhili miradi inayokabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kupanua fursa za kifedha kwa vijana na wanawake ili kuongeza ushiriki wao katika uchumi unaotegemea sekta ya kilimo.

"Tunalenga kuona sekta ya kilimo ikiendelea kuwa injini ya ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa kuzalisha ajira, kuongeza kipato cha wananchi na kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula na bidhaa za kilimo katika ukanda wa Afrika," amesema Nyabundege.

Aidha, amesema TADB itaendelea kushirikiana na Serikali, sekta binafsi pamoja na washirika wa maendeleo ili kuongeza rasilimali za uwekezaji na kuimarisha mchango wa sekta ya kilimo katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Sambamba na hilo, ametoa wito kwa wananchi kutembelea banda la TADB katika Maonesho ya 88 ya Kimataifa ya Kilimo (Nane Nane) mwaka 2026 ili kujifunza zaidi kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo, ikiwemo mikopo, dhamana za kifedha na fursa nyingine zinazolenga kukuza sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.







BOHARI ya Dawa (MSD) imeendelea kuthibitisha ubora wake katika usimamizi wa ununuzi wa umma baada ya kutunukiwa Tuzo ya Utendaji Bora katika Ununuzi wa Umma na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).

MSD imetambuliwa kama Taasisi Bora kwa Ujumla katika Matumizi ya Mfumo wa Kitaifa wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Kielektroniki (NeST) kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni uthibitisho wa uwazi, ufanisi na matumizi sahihi ya teknolojia katika utekelezaji wa shughuli za ununuzi wa umma.

Tuzo hiyo ilikabidhiwa Julai 29, 2026, wakati wa Kongamano la 10 la Kitaifa la Ununuzi wa Umma, linaloendelea katika Ukumbi wa AICC, Mkoani Arusha.


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser (kushoto), akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TCB, Bw. Adam Mihayo, mara baada ya Bw. Laiser pamoja na ujumbe wake kumtembelea ofisini kwake, jijini Dar es Salaam jana, kwa mazungumzo yenye lengo la kuimarisha mahusiano ya ushirikiano wa kimkakati kati ya taasisi hizo mbili katika kuangalia fursa za kibiashara.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser (kushoto), akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TCB, Bw. Adam Mihayo, mara baada ya Bw. Laiser pamoja na ujumbe wake kumtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, kwa mazungumzo yenye lengo la kuimarisha mahusiano ya ushirikiano wa kimkakati kati ya taasisi hizo mbili katika kuangalia fursa za kibiashara.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser (wa pili kushoto), akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TCB, Bw. Adam Mihayo (kushoto), pamoja na baadhi ya maofisa wa benki hiyo, mara baada ya Bw. Laiser pamoja na ujumbe wake kumtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, kwa mazungumzo yenye lengo la kuimarisha mahusiano ya ushirikiano wa kimkakati kati ya taasisi hizo mbili katika kuangalia fursa za kibiashara.





Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser (wa nne kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TCB, Bw. Adam Mihayo (wa tano kushoto), pamoja na baadhi ya maofisa kutoka benki zote mbili, wakipiga picha ya kumbukumbu mara baada ya Bw. Laiser pamoja na ujumbe wake kutembelea ofisini za TCB, jijini Dar es Salaam jana, kwa mazungumzo yenye lengo la kuimarisha mahusiano ya ushirikiano wa kimkakati kati ya taasisi hizo mbili katika kuangalia fursa za kibiashara.