jk akikagua ujenzi wa nyumba kijijini buzwagi zinazojengwa na kampuni ya barrick


RAIS ASIFIA MRADI WA MAKAZI MAPYA BUZWAGI

Rais Jakaya Kikwete amesifia mradi wa makazi mapya wa Buzwagi kuwa ni wa kipekee unaonyanyua hali ya maisha ya mwananchi na kuchangia maendeleo, Rais alisema hayo baada ya kuzindua ujenzi wa nyumba 207 za makazi mapya ya wananchi wa vijiji vya Mwendakulima, Chapulwa na Mwime, Wilaya ya Kahama, Mkoani Shinyanga.

Raisi alisema utaratibu uliotumiwa na Kampuni ya Barrick, wa kuwajengea wananchi nyumba, kuwalipa fidia na kuwakabidhi shamba ni njia bora zaidi kuliko utaratibu uliozoeleka wa kuwalipa fidia kulingana na tathmini ya mali tu.

“Tangu nilivyokuwa Waziri wa madini sijawahi kuona mradi kama huu” alisema Rais Kikwete. “Ninawapongeza Barrick kwa kutekeleza mradi huu na ninawapongeza wananchi ambao wamekabidhiwa nyumba zao”.

Meneja Mkuu Mtendaji wa Barrick Tanzania, Deo Mwanyika, akitoa taarifa za mradi wa Buzwagi kwa Rais Kikwete alisema mradi wa Buzwaji utachangia maendeleo ya uchumi wa Tanzania moja kwa moja kwa kuwekezaji kiasi cha shilingi bilioni 450 wakati wa ujenzi wa Mradi na zaidi shilingi trilioni 1.6 katika kipindi chote cha uzalishaji wa mgodi.

“Uwekezaji huu utaongeza ajira nyingi mpya wakati wa ujenzi zitakazo ingiza jumla ya shilingi bilioni 75 kama mishahara” alisema Mwanyika. Vilevile kutakuwapo na ajira nyingine nyingi zaidi zitakazoingiza jumla ya shilingi bilioni 130 katika kipindi cha uendeshaji wa Mgodi.

Taratibu za kuaanda makazi mapya ni hatua mojawapo kwenye mchakato wa kuanza ujenzi wa mgodi wa Buzwagi. Mgodi wa Buzwagi utaanza kujengwa mara baada ya zoezi la uhamishaji watu kukamilika. Ujenzi unategemea kuchukua miaka miwili.

Mradi huo unatarajia kujenga jumla ya nyumba 207 kama makazi mapya ya wananchi waliokuwa wakiishi ndani ya eneo la Mradi wa Buzwagi. Mpaka sasa nyumba 81 zimeshajengwa na kukamilika na nyumba 64 zinaendelea kujengwa.

Kampuni imejiwekea lengo la kukamilisha nyumba 129 ifikapo mwisho wa mwezo Agosti mwaka huu. Mpaka sasa jumla ya kaya 27 wamekwishahamia kwenye makazi mapya.

Mpaka kukamilika mradi wote wa nyumba 207 umekadiriwa kugharimu Shilingi 1,700,000,000 (Bilioni Moja na Milioni Mia Saba); kati ya hizo Shilingi 510,000,000 (Mia Tano na Kumi Milioni) ni gharama za vibarua.

Meneja Mkuu Mtendaji alisema katika taarifa yake kuwa karibu vifaa vyote vya ujenzi vinanunuliwa kutoka Kahama na wakandarasi wamechukuliwa kutoka Mikoa ya Shinyanga na Mwanza na karibu mafundi na vibarua wote wameaajiriwa kutoka vijiji 6 vinayozunguka Mradi wa Buzwagi.

Kwa mujibu wa habari kutoka Buzwagi, m
chakato wa Mradi huu umeshirikisha wadau wote katika hatua zote muhimu kupitia Kamati Shirikishi ambayo iliundwa na wawakilishi kutoka vijiji vyote vinayozunguka mradi, serikali za vijiji, ofisi ya Mkuu wa Wilaya, ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya na wawakilishi kutoka Barrick.


Lengo la utaratibu huu ni kuwaelewesha wananchi na kuwashirikisha katika maamuzi kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu zoezi la uanzishwaji wa Mradi na ulipaji wa fidia. Pia ziliandaliwa ziara mbalimbali katika eneo la Mradi kwa ajili ya wananchi na viongozi wa Serikali ili kuwawezesha kuuelewa vizuri Mradi.

Uwekezaji wa Barrick utatoa fursa za ajira, mafunzo na biashara kwa wakazi wa vijiji vya jirani na Mradi/Mgodi pamoja na mji wa Kahama. Barrick itatoa mafunzo kwa watu walioko vijiji jirani na Mradi ili kuwaongea ujuzi wa kupata ajira katika migodi.

Kama inavyofanyika katika migodi yake mingine, Mgodi mpya utafanya manunuzi yake kwa kadri iwezekanavyo kutoka kwa wafanyabiashara waliopo karibu na mgodi, mji wa kahama na mikoaa ya kanda ya ziwa. Kwa mfano katika kila mwezi tayari Mradi unatumia shillingi million 32 kwa manunuzi ya vyakual kutoka katika maeneo ya Mikoa ya Shinyanga na Mwanza.

Barrick Gold Corporation ni moja ya kampuni kubwa zaidi za migodi ya dhahabu duniani. Hisa za Barrick zimeorodheshwa kibiashara kwenye masoko ya mitaji ya Toronto na New York.

Barrick Gold Tanzania inaendesha migodi mitatu ya Bulyanhulu, North Mara na Tulawaka, ambapo hivi karibuni itaanza ujenzi kwenye mradi wa Buzwagi.


Maeneo ya migodi ya Barrick inachangia kwa kiasi kikubwa kwenye sekta hii muhimu ya madini nchini Tanzania, huongeza nafasi za ajira, ukuaji uchumi na kuboresha huduma ya elimu na afya kupitia miradi inayobaki kuwa endelevu.

Kampuni ya Barrick ni mchangiaji mkubwa katika hazina ya Serikali, kupitia mishahara, mrahaba na kodi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 13 mpaka sasa

  1. Nasikia Mpakanjia yu hoi bin taaban. Michu hebu tueleze. Ila Michu nasikitika sana kuna siku nilituma msg ambayo ingeweza kumsaidia mtu au watu lakini wewe ikaibania. tena wala sikuandika lugha mbaya ya kuudhi au matusi. Sawa kaka! ulinifanya mpaka nikate tamaa yakuwa narusha mawazo yangu.nilijua blog hii ni ya kuelimisha na kuburudisha lakini vingine unabania. Poa tu. Nisamehe kama nitakuwa nimekukwaza. Tueleze Mpakaroad vipi?

    ReplyDelete
  2. Kaenda Buzwagi kupoza machungu ya wananchi, baada ya Kabwe kufumua madudu ya mgodi huo. Tunashukuru Bw Mwanyika alikiri kuwa mkataba ulisainiwa hotelini, vinginevyo Kabwe angeonekana mwaongo.
    Kwa kweli JK ni msanii sijapata kuona. Anyway, yetu macho.

    ReplyDelete
  3. AAH NGOJA UONE COMMENTS ZA AISAAC-US, HAHAHAHA JAMAA ANACHEKESHA KISHENZI DAH

    ReplyDelete
  4. Is it true MPAKANJIA AMEVUTA?? MIchu tupe news bwana.

    ReplyDelete
  5. ni furaha iliyoje kuona wakazi wa Buzwagi wanafaidika kwa kujengewa nyumba,ambazo natumai zitakua za kisasa,mimi ni kijukuu cha mmoja walio nyang'anywa mashamba yao ambayo yalikua yakiingiza kula yetu ya kila siku nanikisema kula simaanishi mazao yanauzwa halafu pesa ikanunue chakula chetu laa ni tunakula tunacho kipanda, kuanzia mahindi,mipunga,matango,viazi yaani karibu kila chakula cha kitanzania unachokijua tumelima na ndio kimenikuza mie na ndugu zangu sasa mtu kumnyang'anya shamba lake ambalo ndio kila kitu kwake ina maana umtafutie ufumbuzi mwingine wa vipi ajiendeleze sio mkabidhi pesa.Kwahiyo ina furahisha kuona wanajengewa nyumba na kupewa shamba hata kama ni dogo ni afadhali kuliko awe hana kabisa cha kuletea chakula.

    ReplyDelete
  6. Kwa dhati kabisa nazipongeza juhudi za serikali na za mwekezaji kuboresha hali ya maisha ya mtanzania hasa wana vijiji walioko katika maeneo ya MRADI wa Buzwagi.
    Hongera Mh Rais na hongera Mh. Karamagi, tunaona matokeo ya kazi mnayofanya na kujituma kwenu kwa ajili ya wananchi wanaohitaji.

    ReplyDelete
  7. NAOMBA KUULIZA HIVI CALCULATOR ZA BONGO NI TOFAUTI AU WAMEENGEZA UKUBWA AU DIGITAL NUMBER? SERIOUS NIKIJARIBU KUWEKA MABILLION KWENYE CALCULATOR NILIYONAYO INANIPA ERROR.

    UMASIKINI WETU WALA HAUHITAJI HELA NYINGI. TUTAFIKA TU. YAANI HIZO HELA 1,700,000,000 ZINAJENGA NYUMBA 207 WAKATI NCHI ZA WATU NI JUMBA LA MTU MMOJA HILO.

    MUNGU IBARIKI TANZANIA

    ReplyDelete
  8. Anon wa August 25, 2007 11:26:00 PM hapo ukigawanya inakua wastani Tshs 8.2 Millioni kwa kila nyumba. Yes, kwa Mtanzania wa kawaida hata mji kama wa Dar es Salaam anaweza kujenga kwa hela hiyo. Kwa eneo la porini kama huko Buzwagi hizo zitakuwa nyumba kali sana.

    Si unajua tena ni gesture ya kuwatuliza raia waliosogezwa kupisha mradi. Wenyewe wanaita "Corporate Social Responsibility".

    ReplyDelete
  9. Wadaueee NYERERE anageuka kaburini JAMANI JAMANI!!!!

    ReplyDelete
  10. mbona mpakanjia kashughulisha watu sana?...nyani haoni makalio yake wajameni_ mzizi mibamiba

    ReplyDelete
  11. Jamani hizo nyumba zituzuge hiki ni kiini macho au mazingaombwe.Je kampuni ya barrick katika mradi huo inategemea kupata faida ya mabilioni mangapi?ili kutafuta uwiano walichokitoa na wanachokipata hii naweza kufananisha wakati ule mababu zetu kule Shinyanga walipobadirishana almasi kwa shanga na biskuti.Pili ni utaratibu wa makampuni au serikali inapowahamisha wakazi kutoka eneo moja kwenda lingine ili kutoa nafasi kwa mradi fulani hivyo hizo nyumba sio zawadi ni haki yao.Tatu ziara ya Rais katika mradi huo wakati sakata la buzwagi limepamba moto sio wakati muafaka.Hii inaweza ikatafsiriwa kama kumuunga mkono Waziri wa madini mh.Karamangi au ni jitihada za Rais kujaribu kuwatuliza wananchi HAYA NIMAZINGAOBWEEEEEEE

    ReplyDelete
  12. Kweli waTZ hatuna akili. Yaani nani anaweza kujenga nyuma kwa sh. 8.2M? Hata iwe porini..! Mfuko mmoja wa cement ni sh. 15,000. Hapo unaweza piga hesabu na kujua ni mifuko mingapi ya saruji inapatikana, plus mabati, mchanga, kokoto, etc. Kwa Dar hiyo ni ya plot tuu, tena nje ya mji kabisa, kwa taarifa wa wale walio nje ya chi kwa muda mrefu.

    Ni kwamba hiyo 8.2M inajenga vibanda vya low quality tuu. Wanajua wabongo wako soo cheap, kuanzia kwa JK na Karamagi wake, hadi wananchi.

    Hivi tujiulize kama tungeenda huko ulaya tumwambie mtu tunahitaji plot yake (ambayo haina tones of gold chini yake kama buzwagi) angedai kiasi gani kuhama? Sasa kwa nini sisi tunahamisha watu wetu kwa sh. 8.2M na kusifia eti ni mradi mzuri kupita kiasi? Are we mad?

    Kwanza ingebidi kila familia ilipwe si chini ya 200M za eneo lake lenye dhahabu, hapo ndo tuanze kuongelea gharama za usumbufu and re-settlement!

    JK wacha kutuzuga. Semeni mmevuta kitu kidogo mkiwa London, yaishe...

    ReplyDelete
  13. an 8.2m house and a piece of land...how long is the mkataba?..100 years?....iare we worth this kweli?...there was williamson diamonds sisi wengine tangu hatujazaliwa mpaka sasa theoretically tuna wajukuu but nchi bado masikini...kwani haya mahesabu huwa yanapigwa vipi?...state nayo inapata nini?...kama vipi tuachwe na vijumba vyetu vya udongo na vimiembe vyetu mpaka hapo hii mikataba itakapo sainiwa sehemu ambazo hazitaleta utata...siyo mpaka wengine wafungwe gavana dodoma...

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...