Rais Jakaya Kikwete akimshukuru binti aliyempa maua mara alipowasili kwenye uwanja wa ndege mjini Addis Ababa kuhudhuria kikao cha wakuu wa nchi za afrika, AU, kinachoanza leo.


Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameondoka nchini asubuhi yuko Addis Ababa, Ethiopia, kuhudhuria Mkutano wa 12 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa AU.

Mkutano huo wa 12 utafanyika kwa siku mbili kuanzia keshokutwa, Jumatatu, Januari 2, 2009, kwenye Ukumbi wa UNCC-EAC mjini Addis Ababa.Mkutano huo utatanguliwa na Kikao Maalum cha wakuu hao wa nchi wanachama wa AU kitakachofanyika leo Jumapili, kujadili maendeleo ya kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa Afrika.

Kikao hicho maalum kitafanyika chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete, katika nafasi yake kama Mwenyekiti wa AU, na ni mwendelezo wa majadiliano ya suala hilo kama ilivyoamuliwa katika kikao kilichopita cha AU kilichofanyika Sharm El Sheikh, Misri, Juni, mwaka jana.

Kikao hicho maalum kitapokea na kujadili ripoti ya Kamisheni ya AU juu ya mapendekezo ya jinsi ya kuanzishwa kwa Serikali hiyo.Kikao hicho kitafuatiwa na Mkutano wenyewe wa 12 wa wakuu wa nchi hizo utakaofanyika kwenye ukumbi huo huo wa UNCC-ECA.

Rais Kikwete ataufungua Mkutano huo ambao pia utamchagua mwenyekiti mpya wa AU, ambaye atachukua nafasi ya Rais Kikwete, anayemaliza muda wake kwenye nafasi hiyo.

Miongoni mwa wazungumzaji kwenye ufunguzi huo, mbali na Rais Kikwete mwenyewe, watakuwa ni pamoja na Waziri Mkuu wa Ethiopia Ato Meles Zenawi, Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Jean Ping, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, na Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu (Arab League) Amr Moussa.

Kwenye siku ya pili ya Mkutano huo, Jumanne, Februari 3, 2009, wakuu hao watajadili zahama ya kifedha inayoikabili dunia baada ya kuwa wamewasikiliza wataalam mbalimbali wa masuala ya fedha katika Afrika na duniani.

Kwenye siku hiyo ya pili na ya mwisho ya Mkutano huo, Tanzania inatarajiwa kuwasilisha mapendekezo ya mfumo wa kisheria wa kuwalinda masikini katika Afrika.

Mbali na mkutano huo, Rais Kikwete pia amehudhuria Mkutano wa 20 wa Kamati ya Utekelezaji ya Wakuu wa Nchi za NEPAD Jumamosi, Januari 31, 2009. Baadaye mchana, Rais Kikwete amehudhuria mkutano maalum wa eneo la Maziwa Makuu ambao umepokea na kujadili ripoti kuhusu hali ilivyo katika Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Ripoti hiyo imewasilishwa na marais wa zamani, Olusegun Obasanjo wa Nigeria na Benjamin Mkapa wa Tanzania ambao wameombwa na Umoja wa Mataifa na Wakuu wa Nchi za Maziwa Makuu kuongoza jitihada za kuleta amani Mashariki mwa DRC.




Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. hi!picha!hilinistua kidogo!lakini
    any way !JK wetu ni mtu mwaminifu na mzazi mwenye kujua uchungu wa mwana,sio kama Jackob Zuma wa bondeni.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...