Mama Maria Nyerere akimkaribisha JK muda mfupi baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Musoma jioni jioni hii. JK yupo mkoani Mara kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo pamoja na shughuli nyingine atakuwa mgeni rasmi katika kilele cha mbio za mwenge siku ya Jumatano ambayo pia itakuwa ni kuadhimisha siku ya Nyerere.
JK akibonyeza kitufe wakati akizindua mradi wa umeme katika kijiji cha Kisamwene kata ya Butuguri,wilaya ya Musoma vijijijni leo jioni
JK akiteta jambo na Meneja wa TANESCO kanda ya Ziwa Bwana Makala Kingu muda mfupi baada ya kuzindua mradi wa umeme katika kijiji cha Kisamwene, kata ya Butuguri wilaya ya Musoma vijijini jioni hii ya leo
JK akifunua kitambaa kuzindua rasmi Shule ya sekondari mchepuo wa Sayansi ya Chifu Oswald Mang’ombe iliyopo wilaya ya Musoma vijijini.Pembeni ni Mbunge wa Musoma vijijini Mheshimiwa Nimrod Mkono ambaye ndiye mfadhili mkuu wa shule hiyo
JK akimpongeza mbunge wa Musoma vijijini Nimrod Mkono kwa kujenga shule ya kisasa ya mchepuo wa Sayansi ya chifu Oswald Mang’ombe na hatimaye kuikabidhi kwa serikali katika hafla fupi iliyofanyika shuleni hapo jana jioni.Mheshimiwa Mkono aliijenga shule hiyo kwa kutumia mapato yake mwenyewe akisaidiwa na marafiki na wafadhili mbalimbali.
Mwanafunzi Godbless Buluhya wa shule mpya ya sekondari ya Chifu Oswald Man’gombe iliyopo musoma vijijini akifanya jaribio la kisayansi wakati JK alipokagua maabara ya shule hiyo jana jioni.Wengine katika kutoka kushoto ni Mama Salma Kikwete, Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Mstaafu Enos Mfuru(wapili kushoto) na wanne kulia ni Mbunge wa Musoma vijijini Mh. Nimrod Mkono.
JK akiongea na mwanafunzi Ezekiel James wakati alipokagua darasa la mfano muda mfupi baada ya kufungua shule ya Sekondari ya Chifu Oswald Mang’ombe leo jioni wilaya ya Musoma vijijini.
Picha zote na mdau Freddy Maro wa Ikulu
JK akanusha kuwapo
mgawanyiko ndani ya CCM

Na Mwandishi Maalum, Musoma
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa hakuna mgawanyiko ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), bali kuna makundi mawili ya wanachama wa chama hicho yanayovutana Bungeni.

Aidha, Rais Kikwete amesisitiza kuwa Serikali yake haitasita kumfikisha kortini Mtanzania yoyote atakayethibitisha kuwa ameshiriki vitendo vya rushwa, bali kazi hiyo haitafanyika kwa kuongozwa na misingi ya hisia tu za watu.
Rais Kikwete ameyasema hayo jioni ya leo, Jumatatu, Oktoba 12, 2009, wakati anazungumza na viongozi wa CCM wa Mkoa wa Mara nyumbani kwa Mkuu wa Mkoa huo, wakati alipokutana nao, ili kubadilishana mawazo juu ya hali ya chama hicho.

“CCM haina mgawanyiko. Hivi hapa Mara kuna mgawanyiko? Mwanza kuna mgawanyiko? Hivi Tanga kuna mgawanyiko? Singida umesikia kuna mgawanyiko? Mgawanyiko uko kwenye magazetini na ndani ya Bunge,” Rais Kikwete amewaambia wanachama hao.

Amesisitiza Rais Kikwete: “Ukweli ni kwamba wale wanachama wetu tuliowapeleka pale Bungeni kutuwakilisha, wanagombana. Ugomvi uko pale pale Bungeni. Wakiondoka wanauacha pale, wakirudi Bungeni wanaendelea nao. Mgawanyiko huu tunaoambiwa hauko Musoma wala Bagamoyo”

Rais Kikwete amesema kuwa wabunge hao wa CCM “wanagombana wao kwa wao na wakati mwingine wanaonyesha kuwa na ugomvi na Serikali yao. Mimi nimekaa Bungeni pale kwa vipindi vinne kama mbunge na wala sijapata kuona hali ya namna ile.”

“Watu wa chama kimoja hawawezi hata kukaa meza moja na kunywa maji. Kila wakikutana ni mti na macho. Lakini tutayamaliza haya. Lile jopo la wazee wetu linafanya kazi na tuna hakika kuwa hili nalo tutaondokana nalo,” amewahakikishia wanachama hao Rais Kikwete.

Katika kikao chake cha karibuni, Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM iliteua Kamati Maalum ya Wazee wa Busara ikiongozwa na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi kutafakari hali hiyo ya mvutano kati ya makundi hayo mawili na kutafuta mwafaka.

Kuhusu madai ya rushwa, Rais Kikwete amewaambia viongozi hao kuwaeleza wananchi ukweli kuwa kama kuna Serikali ya CCM imepata kuchukua hatua kubwa zaidi za kupambana na rushwa, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha kortini viongozi waandamizi, basi ni Serikali ya Awamu ya Nne.

“Mkiulizwa kwenye kampeni za sasa za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, waambie kuwa haijapata kutokea katika historia ya nchi yetu zikachukuliwa hatua kubwa zaidi za kupambana na rushwa kuliko katika kipindi cha miaka minne iliyopita.”

Amesisitiza kuwa Serikali yake itaendelea kukamata na kumfikisha kortini yoyote ambaye ushahidi utathibitisha anahusika na tuhuma za rushwa, lakini Serikali haitakamata watu tu kwa sababu ya matakwa na hisia za watu tu mitaani.

“Kwenye mazingira ya sasa ya Utawala Bora, hatuwezi kukamata watu kwa hisia na mapenzi tu ya watu. Ni lazima tufanye hivyo kama upo ushahidi wa kuiwezesha Serikali kuwafikisha kortini watu wanaotuhumiwa kwa rushwa.”
Kuhusu kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Rais Kikwete amewaambia viongozi hao wa CCM: “Fanyeni kampeni kifua mbele. Tumefanya mengi. Tuliahidi na tumetekeleza, na tunaendelea kutekeleza. Ni kweli shida za binadamu haziishi, lakini ukweli ni kwamba yaliyoahidiwa yametelezwa kwa kiasi kikubwa.”

Viongozi hao wa CCM wa Mkoa wa Mara wamemwiambia Rais Kikwete kuhusu jinsi kampeni za uchaguzi huo zinavyokwenda.

Katika vitongoji vyote 2,417 vya mkoa huo, CCM haikupingwa katika vitongoji 1, 029.
Katika vijiji 445, CCM haikupingwa katika vijiji 160 na katika mitaa 71, CCM ina wapinzani katika mitaa 69.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. Mambo aliyoyafanya JK huko kwa mfano kuzindua mradi wa umeme na kufungua shule yana sura ya kiserikali. Vipi anaongea mambo ya kichamachama tuuu? JK akumbuke ni rais wa Watanzania wote, sio wa chama.
    "Mgawanyiko" maana yake ni nini?
    "CCM haina mgawanyiko..."
    "Watu wa chama kimoja hawawezi hata kukaa meza moja na kunywa maji...".
    Kama sio kugawanyika huko ni nini? Watu bwana.

    ReplyDelete
  2. HIVI AFYA YA JK INAHITAJI MAELEZO KIASI HICHO? JK HUYU ANAYETOLEWA UFAFANUZI WA AFYA YAKE NI TOFAUTI NA YULE ALIYEJITOLEA UFAFANUZI KUHUSU AFYA YAKE WAKATI WA KAMPENI ZA URAISI KWA KILICHO SABABISHA AANGUKE PALE JANGWANI? HA BM TULIAMBIWA ALITEGUKA MGUU AKIWA MTOTO. UFAFANUZI WA MARAMBILIMBILI HULETA MASWALI MENGI.

    ReplyDelete
  3. ni kweli kabisa mkuu ulivyongea nathan ni sahihi,hotuba haikuwa na malengo hasa katika kuchochea nguvu kazi na maslahi ya nchi na wananchi wake has hususani hapo mara.nachoweza kusema unajua kila mtu anahaha kutafuta kura ndo maana kila sehemu raisi au wabunge watakapoenda ni kuongelea vyama vyao na nini wamefikia.
    natoa pongezi kwa huyo mzee aliyejenga shule,katika mkoa huo.nathani ni jambo jema la kujivunia na kuigwa kwa watu wote wenye uwezo.tunahitaji watu kama mkono.
    Mungu akubariki mzee.
    huyo rais nimemchoka mimi hamna ktu hapo..

    ReplyDelete
  4. Nampongeza Mkono kwa kujenga shule ambayo watoto wa masikini wataweza kusoma na kujipatia elimu ambao itawapa msingi mzuri wa maendeleo.

    Hela kapata wapi hilo ni swala lingine.Watu watasema ahaa mihela ya kesi za bioti hiyo.

    Sisi tunafurahi tumeona shule.

    ReplyDelete
  5. mbona wanafunzi ni wakubwa??au ni a level?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...