Spika wa Bunge Mhe. Samuel Sitta (Mb) akiwahutubia wahitimu wa chuo Kikuu cha Mt. Augustino. (SAUT) katika wa mahafali ya 11 ya chuo hicho ambapo Spika alikuwa mgeni rasmi leo hii huko Nyegezi jijini Mwanza.
Mpiga Picha wa Rais, fred Maro akitunukiwa nondozzz yake ya uzamili katika mawasiliano ya umma ( Master of Mass Communication) na Askofu Thadeus Ruwa’inchi katika wa mahafali ya 11 ya chuo kikuu cha Mt. Augustino (SAUT).
Spika wa Bunge Mhe. Samuel Sitta (Mb) akimpongeza mpiga picha wa Rais Fred Maro mara baada ya kula nondozzz yake ya uzamili katika mawasiliano ya umma ( Master of Mass Communication) katika wa mahafali ya 11 ya chuo kikuu cha Mt. Augustino. (SAUT) ambapo Spika alikuwa Mgeni rasmi. Picha na Owen Mwandumbya wa Bunge


Maafisa habari toka kushoto Nadhifa omari ( wizara ya Ulinzi), mary mwanjelwa (PSI), Cosmas Mwaisobwa (Bodi ya Mikopo), Titus Kaguo (EWURA) na Everine Mpasha ( chuo cha kumbukumbu ya mwl. Nyerere) katika picha ya pamoja mara baada ya kula nondozzz zao za uzamili katika mawasiliano ya umma ( Master of Mass Communication) katika wa mahafali ya 11 ya chuo kikuu cha Mt. Augustino. (SAUT) ambapo Spika alikuwa Mgeni rasmi katika mahafali hayo. Picha na Owen Mwandumbya wa Bunge
Kutoka shoto ni Abdul Njaidi, fred Maro na Eveline Mpasha katika picha ya pamoja mara baada ya kula nondozzz zao za uzamili katika mawasiliano ya umma ( Master of Mass Communication) katika wa mahafali ya 11 ya chuo kikuu cha Mt. Augustino (SAUT) ambapo Spika alikuwa Mgeni rasmi katika mahafali hayo. Picha zote na Owen Mwandumbya wa Bunge



HOTUBA YA MHE. SAMUEL J. SITTA (MB), SPIKA WA BUNGE KWENYE MAHAFALI YA KUMI NA MOJA YA CHUO KIKUU CHA MT. AGUSTINO,
28 NOVEMBA, 2009
NYEGEZI MWANZA
_____________________________________

Mheshimiwa Baba Askofu Thaddeus Ruwa’ichi;
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino;

Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Chuo;

Askofu Severine Niwemugizi
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu;

Wajumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino;

Mheshimiwa Dr. Charles H. Kitima;
Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu,

Waheshimiwa Viongozi wa Serikali na wa Vyama Vya Siasa;

Watumishi na Wahadhiri wa Chuo Kikuu;

Wanajumuiya wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino;

Wahitimu wa mwaka 2009;

Wazazi na Walezi mliopo hapa;

Wanahabari;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana:

Baada ya kupokea barua yenu ya kuniomba kuwa Mgeni Rasmi kwenye mahafali ya 11 ya Chuo Kikuu hiki nilifanya utafiti mdogo ili kufahamu sababu iliyowasukuma kukiita Chuo chenu Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino. Nimejifunza kupitia vyanzo mbalimbali kuwa Mtakatifu Agustino ni miongoni mwa viongozi wanaoheshimika sana duniani kutokana na mchango wake mkubwa wa kitaaluma na falsafa katika historia ya Kanisa Katoliki. Tarehe 20 Februari, 2008 huko Vatican Baba Mtakatifu Benedict wa XVI alimwelezea Mtakatifu Agustino kama ifuatavyo: -

“St. Augustine was a great witness of Christ, much loved by my predecessors and whom I also have studied and meditated upon often. He is the faith of the Church who left us the most works … of vital importance for the history of Christianity. St. Augustine lives through his works and is present among us. As we live, we see the lasting vitality of the faith for which he spent his entire life.”


Wengi wetu tunazitambua jitihada za Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino kuhakikisha kuwa chuo hiki kinatoa matunda mema yatakayolingana na sifa ya urithi tajiri wa umakini, uadilifu, na maadili mema ya Mtakatifu Augustino.

Mhashamu Baba Askofu,

Kwa unyenyekevu nimepokea heshima hii kubwa ya kuwa Mgeni Rasmi katika mahafali ya 11 ya Chuo hiki. Naushukuru Uongozi wa SAUT kwa kunialika kuja kujumuika nanyi kwenye sherehe hii ya Mahafali.

Vile vile, nawapongeza wahitimu wote na wakufunzi ambao kwa juhudi zao za pamoja katika masomo na mwenendo mtulivu hapa chuoni, wametuwezesha kusherehekea siku ya leo. Natoa shukrani maalum kwa Wahadhiri na Watumishi wote wa Chuo kwa jitihada zenu ambazo leo hii tunashuhudia matunda yake.

Nimefahamishwa kwamba dira ya maendeleo ya SAUT imewekwa katika Mpango wa Miaka mitatu 2005/06 hadi 2007/2008 na mpango wa miaka mitano 2009/2010 hadi 2013/2014. Ni kutokana na mipango hii mizuri, Chuo Kikuu hiki kimehimili ongezeko kubwa la wanafunzi pasipo kuathiri ubora wa elimu. Hii ni tofauti kabisa na hali ilivyo kwenye baadhi ya Vyuo Vikuu vingine hapa nchini. Hongera sana kwa kazi hii nzuri.


Mheshimiwa Baba Askofu,

Kuna mambo mawili ya maendeleo ya Chuo ambayo yamenivutia. Kwanza, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino mwaka huu wa masomo kimeanzisha kitivo cha Uhandisi. Hii ni hatua kubwa itakayowezesha upatikanaji wa watalaam katika nyanja ya Teknolojia ambayo ni msingi muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yoyote. Pili, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino mwaka huu wa masomo, kimefungua Kituo chake mjini Mtwara (Mtwara Centre). Kwa mujibu wa taarifa ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu, Kituo cha SAUT Mtwara tayari kimesajili wanafunzi 1200 wa shahada ya Ualimu. Hatua hii sio tu itatuwezesha kupunguza kwa haraka zaidi uhaba mkubwa wa walimu kwenye Shule za Sekondari bali pia itawasaidia Watanzania wengi zaidi kupata elimu ya chuo kikuu. Naupongeza uongozi wa Chuo hiki pamoja na Kanisa Katoliki kwa hatua hizi muhimu.

Ndugu Wahitimu,

Mnahitimu elimu yenu ya Chuo Kikuu katika mazingira tofauti na yale yaliyokuwepo miaka 10 au zaidi iliyopita. Dunia tuliyonayo hivi sasa ni dunia ya utandawazi (globalization). Hiki ni kipindi ambacho kinaifanya dunia kuwa kijiji kimoja. Hivyo, mipaka iliyokuwa imezitenganisha nchi zetu imebaki ni alama tu (symbolic). Hizi ni zama za mawasiliano bila kujali mipaka. Vile vile, teknolojia ya mawasiliano ya upashanaji habari kupitia internet, simu za mkononi, tovuti na luninga imefupisha masafa na kuongeza kasi ya kuwasiliana.

Ndugu Wahitimu,

Utandawazi unaopanuka umetoa fursa mbalimbali za manufaa lakini pia umezaa athari kadhaa. Mojawapo ya fursa zitokanazo na utandawazi ni ukuaji wa teknolojia ya mawasiliano na upashanaji habari, hali ambayo imeleta ufanisi na kasi katika utendaji kazi, biashara na kukuza uchumi. Hata hivyo pamoja na fursa hizo, utandawazi umeharakisha mmomonyoko wa maadili miongoni mwa wanajamii hususan vijana. Imekuwa ni vyepesi mno kuiga mila, desturi na tamaduni zisizoendana na mazingira yetu. Aidha, katika nyanja za uchumi, utandawazi umewezesha ushindani mkubwa katika biashara, ufanisi wa uzalishaji wa bidhaa, ubora wa bidhaa na kukua haraka kwa masoko ya bidhaa hizo. Hali hiyo imezifanya nchi zenye uchumi duni kama ilivyo Tanzania kupuuzwa (marginalized) katika uchumi wa Dunia.

Vile vile, katika soko la ajira, utandawazi umesababisha changamoto kwa Serikali na wadau wa elimu wakiwemo wamiliki wa Vyuo na Wanafunzi, kuinua ubora wa elimu katika ngazi zote ili kushindana kwenye soko hilo.

Ndugu Wahitimu,

Kulingana na changamoto za utandawazi nawaomba wahitimu wa 2009 kutafakari yafuatayo:

(i) Taaluma bila nidhamu na kumtii Mungu haileti mafanikio.

(ii) Njia za mkato katika maisha zina athari kubwa;

(iii) Ni wajibu wenu kusimamia haki na kupinga dhuluma katika jamii.

Nidhamu na Kumtii Mungu:

Mimi naamini kuwa, nyenzo muhimu itakayowasaidia wahitimu katika maisha yenu huko muendako ni nidhamu na maadili mema. Ukiwa na maadili mema utaheshimiwa na kuthaminiwa na watu kama usemi wa Kiswahili usemavyo “Jiheshimu nawe utaheshimiwa.”

Ndugu Wahitimu,

Tunasoma ndani ya Biblia Katika kitabu cha Mithali sura ya kwanza, aya ya 7 kwamba: “Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, bali wapumbavu hudharau hekima na adabu.” Napenda kuwaasa kuwa msingi mzuri wa elimu mliojiwekea hautakuwa na maana yoyote iwapo hamtamtanguliza Mungu katika maisha yenu ya kila siku. Nidhamu na maadili mema ni matunda yatokanayo na kumheshimu Mungu. Bila hivyo, ni sawa na mtu aliyejenga nyumba bila kuiwekea msingi imara. Hivyo, ni dhahiri kuwa nyumba hiyo haitastahimili mafuriko au upepo mkali. Kwa mantiki hiyo, silaha pekee itakayowawezesha kufanikiwa zaidi katika maisha yenu ni kumtanguliza Mungu katika kila jambo mlitendalo kwa kulishika neno lake kwa dhati. Aidha, katika kitabu hicho hicho cha Mithali sura ya tatu, aya ya tano tunasoma: “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, wala usizitegemee akili zako mwenyewe.”

Nchi yetu inahitaji kwa wingi wasomi walio na Nidhamu, Uzalendo na Maadili mema. Hao ndio watakaochangia kuijenga Nchi yetu katika misingi endelevu ya Utu, Upendo, na kutanguliza maslahi ya wengi – hususan wanyonge na maskini.

Njia za mkato na athari zake:

Tatizo jingine linaloikabili jamii yetu hivi sasa hususan miongoni mwa vijana, ni kutawaliwa na hisia potofu kuwa unaweza kufanikiwa haraka katika maisha kwa njia za utapeli, ujanja ujanja na za mkato. Kibaya zaidi, jamii yetu imekuwa na tabia ya kusifia na kuenzi mafanikio yanayotokana na njia hizo. Ukiajiriwa Benki, unafikiria njama za kuiba Mamilioni, ukiajiriwa kutoa huduma za kutoa haki, kutoza kodi au hata kutibu wagonjwa unafikiria namna ya kujipatia Rushwa kwa ufanisi. Bila shaka wengi wenu mmesikia na baadhi yenu mnatumia msamiati wenye maneno kama ameukata, ameula, ameuchinja au kasevu. Nawatahadharisha kuwa, njia kama hizo si tu sio endelevu, bali pia huwapotosha vijana wengi kujiingiza kwenye vitendo viovu kama vile ujambazi, wizi, wizi wa kalamu, utapeli, ngono-uzembe, umalaya, kutumia au kuuza dawa za kulevya nk, ambavyo matokeo yake sisi sote tunayafahamu.

Ndugu Wahitimu,

Napenda kuwaasa kuwa njia pekee na endelevu itakayowaletea maisha bora ni ile mliyoichagua ninyi­, nayo ni elimu inayoambatana na maadili mema. Mtalaam mmoja wa masuala ya elimu alitumia maneno yafuatayo kuelezea maana ya elimu: “Education is the process of instruction aimed at the all round development of mankind. Education dispels ignorance. It is the only wealth that can not be robbed. Education includes the moral values and the improvement of character and the methods to increase the strength of mind.” Anayetumia vipaji na elimu yake kutenda maovu, hatasamehewa na jamii bali mtenda mema atakumbukwa vizazi na vizazi kama tunavyomkumbuka Mt. Augustino.

Ndugu Wahitimu,
Wajibu wa kutetea haki na kupinga dhuluma.
Migogoro na machafuko katika nchi mbalimbali hutokana na tabia ya baadhi ya viongozi kupuuza sauti na mahitaji ya wananchi walio wengi na kukumbatia maslahi yao binafsi na ya marafiki zao. Hali hii ikiachwa iendelee huwafanya wananchi kukosa imani kwa utawala uliopo. Hatimaye wananchi, baada ya kuchoshwa na mfumo huo, hujiingiza katika vitendo vya kuupinga waziwazi mfumo huo. Matokeo yake ni chuki ndani ya jamii na hata umwagaji damu. Vijana, hususan, ninyi mliobahatika kupata elimu nzuri mna nguvu kubwa ya kuizuia hali hii kwa kusimama kidete kupinga dhuluma, maonevu na rushwa katika jamii yetu.

Ndugu Wahitimu,

Mwanaharakati maarufu wa Kimarekani, Hayati Martin Luther King (Jr) aliwahi kuasa kuwa: “There is nothing more dangerous than to build a society with a large segment of people in that society, who feel that they have no stake in it, who feel that they have nothing to lose. People, who have a stake in their society, protect that society, but when they feel they don’t have it they unconsciously want to destroy it.” Kwa hiyo, wahitimu msiwe watazamaji. Jipangeni ndani ya jamii mtetee utawala bora na kukataa uonevu.

Nchi yetu imebahatika kuwa na misingi ya kuheshimu utu, umoja na usawa iliyowekwa na Muasisi wa Taifa letu Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere. Misingi hiyo inazingatia utu wa mtu bila kujali kabila, rangi, utajiri, jinsia au eneo analotoka mtu. Misingi hiyo imeendelea kuifanya Tanzania kuwa kisiwa cha amani na utulivu ndani ya bahari iliyochafuka. Hivyo, hatuna budi kuidumisha misingi hiyo kwa nguvu zetu zote ili kulinda maslahi ya Taifa letu na ya vizazi vijavyo. Kwa mantiki hiyo, naamini na ninashauri kuwa wasomi wetu mnalo jukumu maalum kuutumia uelewa wenu kukemea waziwazi na bila woga vitendo vyote vyenye mwelekeo wa kuivunja misingi hiyo. Kwa pamoja jamii ivikatae vitendo vya ubabe katika utawala, upendeleo na uonevu, wizi, rushwa na aina zote za matumizi mabaya ya madaraka.

Margareth Chase Smith, Mwanasaikolojia wa Kiingereza aliwahi kuasa kuwa: “Moral cowardice that keeps us from speaking our minds is as dangerous to this country as irresponsible talk. The right way is not always the popular and easy way. Standing for right when it is unpopular to do so is a true test of moral character.” Kwa kifupi, kipimo cha utu wako ni kutokuwa mwoga katika kupigania haki zako na haki za jamii.

Ndugu Wahitimu,

Rais wa zamani wa Marekani Hayati John F. Kennedy katika hotuba yake mara baada ya kuapishwa kuwa Rais wa 35 wa Marekani tarehe 20 Januari, 1961 aliwahi kuwaasa Wamarekani wenzake kujiuliza wameifanyia nini nchi yao na sio nchi yao imewafanyia nini. Maneno hayo ingawa aliyatamka yapata miaka 48 iliyopita, bado yana maana kubwa sana, sio tu miongoni mwa Wamarekani, bali hata miongoni mwetu Watanzania.

Ndugu Wahitimu,

Ni dhahiri kuwa matatizo na kero nyingi tunazozishuhudia hivi sasa kama vile rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma nk, yanatokana na kupungua kwa uthabiti wa uzalendo miongoni mwa wanajamii. Kwa upande mmoja kuna woga wa kupambana na nguvu za dhuluma na rushwa lakini pia kuna tamaa inayotufanya tusalimu amri na kujiunga na himaya za walarushwa.

Kama nilivyosema hapo awali, imefikia mahali ambapo wanajamii huwasifu watumishi na viongozi wa umma ambao hujilimbikizia mali nyingi kwa njia za rushwa, udangayifu na ubadhirifu. Aidha, wanajamii hao hao huwasuta na kuwabeza wale watumishi na viongozi wachache ambao baada ya utumishi wao wa uaminifu wamestaafu bila kujilimbikizia mali!

Ndugu Wahitimu, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge la Tisa aliyoitoa mnamo tarehe 30 Desemba, 2005 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alisema, “kadhalika hatuna budi kuchukua hatua thabiti kuzuia Watumishi wa Umma kutumia nafasi zao kujitajirisha na kujilimbikizia mali. Sisemi kwamba ni haramu mtu kuwa tajiri au kuwa na mali, hapana. Ninachosema mimi kuwa ni haramu ni kutumia nafasi ya utumishi na uongozi wa umma kujipatia manufaa, kujitajirisha au kujilimbikizia mali”.

Ndugu Wahitimu, wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Ni dhahiri kuwa elimu peke yake haiwezi kukidhi kiu na ari waliyo nayo Wananchi katika kuondoa umaskini na kuinua hali zao za maisha. Elimu yenye tija kwa jamii haina budi iendane na maadili mema. Aidha, elimu inayoambatana na maadili mema italeta uaminifu katika kazi na uadilifu katika utumishi wa Umma. Kuna nchi kadhaa leo hii katika bara la Afrika zenye Wasomi wengi na vyuo vikuu vingi, lakini nchi hizo zinachekwa kwa kudhihirika kuwa ni vinara wa Wizi na rushwa.

Kwa kiasi kikubwa wasomi wa Nchi hizo wamechangia kudumaza maendeleo ya nchi hizo. Badala ya kutafuta majawabu ya matatizo na kuwakwamua wananchi kwenye lindi la umaskini na kukata tamaa, wasomi hao wameusaliti umma kwa kujiingiza kwenye tamaa ya kujilimbikizia mali kwa njia za ujanja na kuendekeza rushwa, uzembe, ubadhirifu n.k. Licha ya kudharauliwa, Nchi za aina hiyo huvutia wawekezaji matapeli na hivyo kujenga duara jeuri ya rushwa na utapeli huku Nchi ikizama katika lindi la umasikini na kukosa maendeleo. Hatuna budi kuhahakisha kuwa Taifa letu halitumbukii katika orodha ya nchi kama hizo zenye sifa mbaya na maendeleo yaliyokwama.

Hitimisho la waraka wa kanisa Katoliki kuhusu mapendekezo ya vipaumbele vya kitaifa ukurasa wa 23 limeweka vizuri azma ya wenye kulitakia mema taifa letu kwa maneno yafuatayo:-

‘Tunahitaji kufufua maadili, kurudi katika tunu msingi za kimaadili na matashi ya kujenga maelewano, mshikamano, kujali manufaa kwa wote na kumpatia kila mmoja mali, nafasi, fursa na wajibu’ Wito huu unastahili kuungwa mkono kwa vitendo na sisi sote Watanzania.

Binafsi naziunga mkono jitihada zilizotangazwa na Mheshimiwa Rais wetu za kuleta mabadiliko katika sheria za maadili na uchaguzi kwa lengo la kuwabana viongozi wote wanotumia mianya iliyopo kujitajirisha kwa mikataba mibovu, kutupatia viongozi wabovu kwa kutumia fedha, rushwa za aina mabalimbali na matumizi mabaya ya madaraka.

Bunge ninaloliongoza linasubiri kwa hamu miswada yoyote ya Serikali itakayoimarisha uwazi na uwajibikaji wa viongozi wa ngazi zote nchini katika masuala ya maadili.

Kwa kuhitimisha nasaha zangu kwa wahitimu nawaomba mlikumbuke neno hili lililopo katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia sura ya 5 aya ya 16 na sehemu ya aya ya 17 kama ifuatavyo:

16Basi nasema, enendeni kwa Roho wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. 17 Kwa maana mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili;

Wapendwa wahitimu wa SAUT 2009 nawatakia mafanikio mema katika maisha na daima muwezeshe Roho aushinde mwili.

Ahsanteni kwa kunivumilia na kwa kunisikiliza.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 9 mpaka sasa

  1. Candid ScopeNovember 28, 2009

    Mheshinmiwa saba Kaka Nichuzi nashukutu kutuletea hii hotuba ya speaker wa Bunge la Tanzania Mheshimiwa Samwel Sitta.

    Ama kwa hakika tunao viongozi wanaostahili kuheshimika kwa kuenzi umma wa watanzania kimaadili na utashi kamili. Kama wengi wetu tukiwa tunaishi kwa misingi hii miwili determination and self awareness na imani tutachagua viongozi wanaojali maslahi ya taifa na wananchi kwa jumla badala ya kujilimbikizia mali.

    Mheshimiwa Speaker wa Bunge Samweli sitta katika mahafali ya Nyegezi kaonyesha ukweli wa mengi yanayo wakera watanzania wapenda haki na maendeleo ya taifa

    ReplyDelete
  2. Wengi wetu wapenzi wa Glob hii nikiwemo mimi binafsi, huwa tunakawaida ya ku ignore posts zenye maandishi mengi sana ya kusoma, na kuishia kusoma Headings tu, lakini leo kwa kuona ni hotuba ya nani, sikuona uvivu au kusita kuisoma, na hakika sijutii kuisoma,maana imenipa ari na nguvu mpya ndani yangu km mtanzania kuona na kutafakari upya umakini wa ninayoyafanya kwa nchi yangu, hakika Speeker6 umesema kinachotakiwa kusikilizwa na watanzania wengi-Ujumbe mzuri sana.
    Hongera Maro kwa kunyaka nondo...., na ahsante sn Michuzi kwa post hii

    ReplyDelete
  3. Good, SAUT in making! Napakumbuka sana hapo Raila Odinga Ground, natamani nirudi toka huku Trinidad Tobago wasela wangu kuungana nanyi kuserebuka, vipi Beach ya kule chini kwa Mheshimiwa Diwani ilikosa shughuli kweli? haya wahitimu chakalikeni, kazi mtapata sasa maana mna vyeti.

    ReplyDelete
  4. ALIWAHAMASISHA KUWA WASIULIZE NCHI YAO ITAWAFANYIA NINI, ILA WAO WATAIFANYIA NINI NCHI YAO IN FUTURE, SI NCHI YAO IMEWAFANYIA NINI. ALIKUWA ANAONGELEA TO UNKNOWN FUTURE ASINGEWEZA KUONGELA PAST AMBAYO WAMESHAIPITA NA WANAJUWA NCHI IMEWAFANYIA NINI. IPO TOFAUTI KUBWA KATI YA IMEWAFANIA NINI NA ITAWAFANYIA NINI. ALIKUWA ANAWAHAMISHISHA FOR THE FUTURE.

    ReplyDelete
  5. And part of that speach is here under, and he did not say WHAT THE COUNTRY HAS DONE FOR THEM, AND THEM WHAT HAVE THEY DONE FOR THE COUNTRY, WHAT HE SAID IS HERE BELOW CHECK BY YOURSELF.


    "In the long history of the world, only a few generations have been granted the role of defending freedom in its hour of maximum danger. I do not shank from this responsibility - I welcome it. I do not believe that any of us would exchange places with any other people or any other generation. The energy, the faith, the devotion which we bring to this endeavour will light our country and all who serve it -- and the glow from that fire can truly light the world.

    And so, my fellow Americans: ask not what your country can do for you - ask what you can do for your country.

    My fellow citizens of the world: ask not what America will do for you, but what together we can do for the freedom of man.

    Finally, whether you are citizens of America or citizens of the world, ask of us the same high standards of strength and sacrifice which we ask of you"
    J F KENNEDY INAUGRAL SPEECH, 1961

    ReplyDelete
  6. Mtoto wa CoastNovember 29, 2009

    Wahitimu wote hongereni sana.

    Huko Nyegezi kero kubwa ni baadhi ya wananchi wenye nyumba zao kuzunguka au katika viunga vya karibu na eneo la chuo.

    Wanapandisha pango kila wakati bila hata taarifa ya muda wa kutosha wakati hata hivyo vyumba havina kiwango kinacholingana na kodi wanazotoza.

    Jamani hata kama tuko katika soko huria, je hakuna haki za walaji/wateja?

    TRA, Wakala wa Majengo na Ushirika wa Walaji (kama upo) fuatilieni (sio kuomba rushwa) kuhakikisha kuwa hao watu wanalipa kodi inayostahili tokana na wanachokusanya kwa kichwa na pia mnaweza kuwashauri juu ya gharama za kutoza.
    Wanafanya uhuni huu baada ya kugundua kuwa utashi (demand) ya mahala pa kuishi Wanafunzi eneo la karibu na Chuo ni kubwa hapo mahala.

    Haijalishi hata kama kwingine kokote kuko hivyo; suala hapa ni kuwa;
    'Dai malipo zaidi baada ya kutoa notisi muafaka kwa huduma bora zaidi!'

    ReplyDelete
  7. Mheshimiwa Michuzi najaribu kutuma wazo!

    Ni nini umuhimu wa kuwa na wabunge wengi wa kuteuliwa? labda wadau waweza toa mawazo

    Mimi nilikuwa nashauri wabunge wawe ni wale waliochaguliwa moja kwa moja na wananchi na kusiwe na viti maalum vya upendeleo, hivi husababisha kuwa na wabunge wengi ambao hawawajibiki moja kwa moja kwa wananchi bali kwa waliowateua ambao asilimia kubwa ni raisi na vyama vyao

    Wadau mnakaribishwa kutoa mawazo!

    ReplyDelete
  8. Hotuba imetulia kweli! Hongera Mh. Spika kwa nasaha zako nzuri!

    Hongera Fred and Mpasha kwa kulamba nondozz! Ni hatua muhimu sana katika maisha!

    Nikikumbuka SAUT enzi hizo ikiitwa NSTI mambo yalikuwa mswano kweli! Watu walikuwa wanapishana kwenye corridors za Mikumi, Serengeti, etc!!!! Palikuwa hapatoshi!

    Malimbe Campus kulikuwa poa ile mbaya! Maisha yalikuwa mswano watu walikuwa busy na kuku wa kienyeji!!!!!!!!!!!!!

    SAUT/NSTI Alumni

    ReplyDelete
  9. Michuzi kwanini umebania comment yangu? Nimeuliza Godfrey Baluah yupo wapi siku hizi manake yeye ndio alikuwa mpiga picha wa Raisi na Fred Maro alikuwa pia yupo ikulu ila mpiga wa picha wa Raisi alikuwa Baluah. Je ameteuliwa sehemu ingine? amestaafu?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...