Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo Joel Bendera (katikati) akisisitiza jambo kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari- MAELEZO (Kushoto) Clement Mshana na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) Elishilia Kaya mara baada ya ufunguzi wa mkutano wa tano wa Maofisa Habari ,Elimu na Mawasiliano wa Wizara,Taasisi,Idara zinazijitegemea na Wakala wa serikali leo jijini Arusha. Picha/Habari na Aron Msigwa/Veronica KAzimito - MAELEZO.

Serikali imesema itaendelea kulinda na kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata haki ya kupata na kutoa habari kwa mujibu wa sheria .

Hayo yamesemwa leo na naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Joel Bendera wakati akifungua mkutano wa tano wa maofisa Habari, Elimu na Mawasiliano unaofanyika katika kituo cha kimataifa cha mikutano cha Arusha (AICC).

Amesema Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo inalo jukumu kubwa la kusimamia sekta ya habari nchini pamoja na kuratibu Vitengo vya Habari, Elimu na Mawasiliano kwa kuhakikisha kuwa masuala yote ya Habari yanafuata miongozo na kanuni kwa mujibu wa sheria za nchi.

Awali akizitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta ya habari nchini amesema kuwa kukosekana kwa weledi katika ukusanyaji na usambazaji wa habari moja ya tatizo linalorudisha nyuma maendeleo ya habari na kuwataka maofisa habari wa elimu na mawasiliano kwa umma kuwa mstari wa mbele katika kuzingatia weledi katika kutekeleza majukumu yao.

“Sio siri taaluma yenu hivi sasa imeingiliwa na kundi la watu ambao kwa kutofahamu sawasawa majukumu yao kitaaluma wanapotosha umma kwa kuandika na kutoa habari zisizo sahihi, habari ambazo hazijafanyiwa utafiti na kwa upande mmoja au mwingine zimeshapitwa na wakati.”

Ameendelea kufafanua kuwa katika fani waliyonayo maofisa hao, wajibu wao sio tu kuandaa majibu ya kero na hoja zinazotolewa na wananchi dhidi ya Serikali au kuandaa taarifa mbalimbali bali kuelimisha jamii kuhusu sera ya nchi na mabadiliko mbalimbali yanayotokea nchini.

Kwa upande wa utoaji wa habari kwa wananchi amesema sekta ya habari inalo jukukumu kubwa kuwaelimisha kwani wamegawanyika katika matabaka mbalimali kielimu, kijinsia na makazi hivyo ni wajibu wa maofisa hao kutambua mlengwa wa ujumbe wanaotarajia kuuwasilisha, chombo wanachotakiwa kupitishia ujumbe huo na lugha wanayotumia ili kuwafikia walengwa.

Aidha kuhusu kujiendeleza kielimu Naibu waziri Bendera amewaambia maofisa hao kuongeza elimu ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Akizungumzia suala zima la tovuti ya wananchi, naibu waziri amesema Serikali imetekeleza kwa vitendo dhana ya uwazi na uwajibikaji ambapo inaweza kuzungumza na wananchi wake, kujua kero zao na kutafuta njia za kuzipatia ufumbuzi.

Naibu waziri amesema kuwa tangu tovuti ya wananchi ianze kazi mnamo mwaka 2008 Serikali imepokea zaidi ya hoja 67,874 na kati ya hoja hizo 40,500 zimejibiwa ikiwa ni sawa na asilimia 60, hoja nyingine ambazo hazijajibiwa hazihusu utendaji wa Serikali.

Mkutano huu wa siku sita, unafanyika wakati Serikali imeamua Vitengo vya Habari, Elimu na Mawasiliano viratibiwe na Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo kwa mujibu wa hati ya mgawanyo wa majukumu ya wizara hiyo iliyotolewa tarehe 13 februari, 2008.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Hongera mwl Joel nasikia raha sana nikikuona Kama hivi, good luck, you're such a good man, I wish you all the best in the world, couldn't happen to a nicer bloke! HM

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...