WEKUNDU WA MSIMBAZI SIMBA SC.
KATIKA PICHA RASMI YA MWAKA 2010


Vinara wa ligi kuu ya kandanda ya Vodacom Simba SC leo wamevunja mwiko kwa kuibanjua Toto Africa ya Mwanza bao 2-0 kwenye uwanja wa nyumbani wa vijana hao wa Kishamapendo wa CCM Kirumba na kuendelea kuongoza ligi wakiwa hawajapoteza mchezo hata mmoja hadi sasa.
Simba walikuwa hawajawahi kuifunga Toto Africa toka ipande daraja misimu miwili iliyopita, na mchezo wao wa mwisho Simba ilibugia 4-1 walipotia mguu Kirumba mwaka jana. Lakini leo kibao kiligeuka na kukuta wenyeji wakisalimu amri katika mchezo uliojaa visa kiedekede.

Kisa kimojawapo ni Simba kugoma kuingia kwenye chumba chao cha kuvalia kwa madai kwamba walikuta matone kama ya damu yametapakaa kila sehemu chumbani humo. Kwa mujibu wa meneja wa wekundu hao wa msimbazi, Innocent Njovu, walimwita kamisaa na waamuzi ambao baada ya kuona hali hiyo waliwaruhusu wafanye maandalizi yao uwanjani.
Meneja wa uwanja wa Kirumba, John Tegete, ameruka kimanga alipoulizw kuhusu matone hayo yanayosadikiwa kuwa ndumba-nangai, na kusema yeye alichofanya ni kukabidhi funguo kila timu baada ya kuhakikisha viko safi, na kwamba hayo mengine hayamhusu na wala hakuwa na habari nayo.
Hata hivyo gemu lilianza kama ada na Simba walifungua hesabu dakika ya tano ya kipindi cha pili kupitia kwa mshambualiaji wake Mussa Hassan Mgosi ambaye alitumbukiza kimiani goli la kwanza kwa timu yake na la 11 kwake binafsi baada ya kupokea majalo toka kwa Nicco Nyagawa.

Dakika nne baadaye Mgosi alichachafya ngome ya Toto Africa kwa chenga zaa mwili kabla ya kumtangulizia kiungo mshambuliaji Ramadhani Chambo ambaye alikata nyasi kwa shuti kimo cha kuku iliyoenda nyavuni moja kwa moja, baada ya kumpita kipa Mohamed Azizi.

Ushindi huo umeipa Simba pointi 42 dhidi ya 30 za watani wao wa jadi Yanga inayokamata nafasi ya pili. Toto Africa wamezidi kwenda chini kuelekea mstari wa hatari wakiwa na pointi 7 kutoka michezo 14.

Huko Morogoro Mtibwa Sukari wana tam-tam wameendelea kuogelea katika nafasi ya nne kwa kuifunga JKT Ruvu iliyo nnafasi ya tano kwa bao bao 1-0, na kujikita na pointi 25.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...