Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ben Christiaanse (kushoto), akiongea na wanahisa wa benki hiyo kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa benki uliofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NMB, Misheck Ngatunga.

NA MWANDISHI WETU


WANAHISA wa Benki ya NMB watapata gawio la jumla ya Shilingi 15.7 bilioni kwa mwaka 2009, ikiwa ni ongezeko la asilimia 4.7 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NMB, Misheck Ngatunga, amesema mgawo wa kila hisa kwa mwaka utakuwa Shilingi 31.40, ikilinganishwa na Shilingi 30 kwa mwaka 2008.

Alikuwa anawasilisha ripoti ya mwaka 2009 kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa NMB uliofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Ngatunga alisema mwaka 2009 ulikuwa wa changamoto nyingi kutokana na kuongezeza kwa ushindani katika sekta za benki pamoja na mtikisiko wa uchumi duniani, ambao ulikuwa na madhara makubwa katika uchumi wa Tanzania kama kwingineko duniani.

Aliisifu serikali kwa kuandaa mkakati wa kukabiliana na mtikisiko wa uchumi kwa kuendeleza mfuko wa kuokoa na kusaidia sekta na taasisi zilizoathirika na mtikisiko huo.


“Sekta ya fedha ya Tanzania kwa ujumla haikuathirika na mtikisiko huo, na iliendelea kuwa na mtaji wa kutosha na yenye faida. Ingawa athari hizo zilikuwa tofauti kwa kila benki.”Hata hivyo, alisema hali ya uchumi na kushuka kwa viwango vya riba vilichangia kushuka kidogo kwa mapato na faida mwaka 2009, ambapo benki hiyo ilipata faida ya Shilingi 68.04 bilioni (kabla ya kodi), ikilinganishwa na Shilingi 70.94 bilioni mwaka uliotangulia.


Upungufu huo wa faida ni kwa asilimia nne.Wakati huo huo, NMB imedhamiria kuboresha huduma zake na kupunguza msongamo wa wateja katika matawi yake nchini na kuwafikia Watanzania wengi zaidi wanaoshi vijijini.

Katika taarifa yake ya mwaka 2009, benki hiyo yenye mtandao mkubwa nchini imesisitiza kuwa itazingatia zaidi kupunguza muda wa wateja kusubiri katika matawi na ATM, pamoja na kuboresha mikopo.

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi alisema pamoja na mafanikio mengi yaliyopatikana katika kipindi kipindi cha mwaka uliopita, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa matawi na mtandao wa ATM kutoka 167 mwaka 2008 hadi 281 mwishoni mwa mwaka 2009, bado wanakabiliwa na changa moto nyingi, ikiwemo tatizo la msongamano wa wateja.

“Nina uhakika kwamba uongozi na wafanyakazi wa NMB watafanikiwa kukabiliana na changamoto hizo,” alisema Ngatunga.Alisema NMB inakusudia kupanua zaidi mtandao wa matawi nchini ili kuweza kujikita zaidi katika msukumo wa ‘Kilimo Kwanza’, mpango wa kuboresha uzalishaji wa kilimo na sekta ya mabadiliko kwa nia ya mapinduzi ya kilimo.

Akizungumza katika mkutano huo, Mtendaji Mkuu wa NMB, Bern Christiaanse, alisema mtandao wa matawi ya NMB uliongezeka kufikia 133 mwaka 2009, huku matawi mapya nane yakifunguliwa mwaka huo.

Alisema ongezeko hilo ni matokeo ya mkakati wa benki hiyo wa kutoa huduma za kifedha kwa watanzania wengi iwezekanavyo.Kwa mujibu wa taarifa ya mwaka 2009, jumla ya raslimali za benki hiyo zilikua kwa asilimia 20.6 kutoka Shilingi 1,384.3 bilioni hadi 1,669.3 bilioni, wakati ambapo mtaji wa benki ulikua kwa asilimia 20.4 kutoka Shilingi 159,689 milioni hadi Shilingi 192,239 milioni.

Taarifa hiyo iliyowasilishwa kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa NMB ni ya pili tangu benki hiyo iwe kampuni ya umma baada ya kuorodheshwa kwenye soka la hisa la Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 30, 2010

    4.13% yield is better than kuweka pesa zako kwenye saving account. Good job NMB.

    btw, Sikujua Dividend kwa kiswahili ni Gawio.

    Faraja

    ReplyDelete
  2. AnonymousMay 31, 2010

    HII NI NJIA NYINGINE YA KUHAMISHA HELA ZA WATANZANIA.

    KWANZA NI VIZURI TUKAFAHAMU KUWA WATEJA WAKUBWA WA HII BENKI NI SERIKALI.

    PILI HII BENKI INACHAGI SERIKALI COMMISSION KUBWA SANA KWENYE HUDUMA ZAKE,HIVYO FAIDA KUBWA INAYOPATIKANA INATOKA KWENYE FEDHA ZA SERIKALI( WALIPA KODI)

    TATU WAWAKEZAJI WAKUBWA KWENYE HII
    BENKI NI ROBOBANK YA UHOLANZI. HIVYO BASI PESA NYINGI YA HII FAIDA INAAMISHWA NCHINI KWA NJIA YA DIVIDEND.

    NASHANGAA UTAONA WAZIRI WA FEDHA AKIFURAHIA ATAKAPOPEWA HUNDI YA DIVIDEND. KUMBE HAJUI KWAMBA NI SAWA TU NA MTU ALIYETOA FEDHA NYINGI MFUKO WA KULIA NA KUWEKA MFUKO WA KUSHOTO. NA ZIPOINGIA KWENYE MFUKO WA KUSHOTO ZINAKUWA ZIMESHAPUNGUA SANA.

    HAWA WAWEKAZAJI WA NCHI WANATAKIWA KUWEKEWA SHERIA ITAKAYOWALAZIMU KUWAKEZE SEHEMU YA DIVIDEND YAO HAPA NCHINI LA SIVYO HELA ZA NCHI HII ZITAAMISHWA TU KIRAHISI KWENYE NJE.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...