MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu leo imemfutia mashitaka na kumuachia huru mshitakiwa wa sita Joseph Rutto, aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya kutapeli na kutakatisha fedha haramu.

Rutto na wenzake watano wakiwamo aliyekuwa Mhasibu wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) Justice Katiti, Fortunatus Muganzi, Robert Mbetwa, Gidion Otullo na Godwin Paula, walikuwa wakikabiliwa na mashitaka 10 yakiwemo kujipatia Sh 338,935,337.46 kwa njia ya udanganyifu, mawili yakiwa ya kutakatisha fedha na mawili kumdanganya mwajiri wake na kusababisha hasara ya fedha hizo.

Mwendesha mashitaka Wakili wa Serikali Fredrick Manyanda alidai mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Aloyce Katemana kuwa upande wa mashitaka unaondoa mashitaka dhidi ya mshitakiwa huyo kwa kupitia kifungu cha sheria namba 91 (1) ya mwenendo wa mashauri ya jinai.

Kupitia kifungu hicho cha sheria inampa madaraka Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuondoa shitaka au mashitaka dhidi ya mshitakiwa kwa sababu hana nia ya kuendelea na mashitaka dhidi yake (Nolle Prosequi).

Hakimu Katemana alisema shitaka hilo limeondolewa kupitia kifungu hicho cha sheria hiyo.

Wakati huo huo baada ya kuachiwa kwa mshitakiwa huyo Wakili Manyanda aliomba kubadilisha hati ya mashitaka dhidi ya washitakiwa watano waliobaki ambapo walisomewa mashitaka hayo 10 yanayowakabili.

Wakisomewa mashitaka yao mapya washitakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo katika vipindi tofauti kati ya Septemba na Oktoba mwaka 2008.

Katika mashitaka ya kwanza na pili, wote kwa pamoja wanadaiwa kula njama na kuitapeli Barclays kwa kughushi baadhi fomu zinazoonesha kuwa Kampuni ya Tourism Promotion Services inaitaka benki hiyo kuilipa Kampuni ya East Africa Procurement Services Limited Sh 338,935,337.46 wakidai kuisambazia kampuni hiyo vifaa vya hoteli.

Katika mashitaka ya tatu yanayowakabili mshitakiwa wa nne na wa tano ambao wanadaiwa katika tarehe hizo, waliwasilisha nyaraka za kughushi katika Makao Makuu ya Barclays ili benki hiyo itoe malipo kwa Kampuni ya Tourism Promotion Services kutoka kwa East Africa Procurement Services Limited Sh 338,935,337.46 wakidai kuisambazia kampuni hiyo vifaa vya hoteli.

Katika mashitaka ya nne, wote wanne wanadaiwa kujipatia Sh 338,935,337.46, ambapo inadaiwa kati ya Oktoba 6 hadi 30, kwa makusudi walijipatia fedha hizo kutoka Barclays kwa kudanganya kuwa East Africa Procurement Services inatakiwa kulipwa na Tourism Promotion Services.

Katika mashitaka ya tano na sita, Katiti anadaiwa kutumia nyaraka kumpotosha mwajiri wake zilizoonesha kuwa Kampuni ya Tourism Promotion Services imelipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya Agosti mwaka juzi; jambo ambalo si sahihi.

Washitakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kutakatisha fedha haramu katika mashitaka mawili tofauti ya saba na nane na kudaiwa kuchota fedha kutoka Benki ya CRDB, Tawi la Holland kwenye Akaunti Namba 0121186000 ya East Africa Procurement Services na kuzihamishia Barclays na Kenya Commercial Bank huku wakishirikiana na watu wengine ambao hawajafahamika.

Katika mashitaka ya tisa na 10, ni mbadala wa mashitaka ya saba na nane ambayo ni zao la rushwa au yanayohusiana nayo kutokana na kuhamisha fedha kutoka Benki ya CRDB na kuhamishia katika akaunti nyingine ili kuficha asili ya fedha hizo.

Washitakiwa wote walikana mashitaka hayo na walirudishwa rumande na kesi hiyo itasikilizwa tena mahakamni hapo Februari 23, mwaka huu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. What is kutakatisha fedha wadau embu nielekezeni hilo!

    I cant get it!

    ReplyDelete
  2. Kutakatisha hela ni Money laundering kwa kidhungu...

    mfano umeshaona dinner au kirestaurant hakina hata wateja wengi kwa siku lakini hakifi na kinalipa bills zake bila matatizo kabisa na mwisho wa mwaka wanafile tax na kusema wamepata mapato kadhaa kumbe hiyo hela ilipatikana kwa kuuza unga au kwa nji nyingine isiyo ya halali...sasa hapo wametumia hiyo restaurant kusafisha hela saas sijuihao watu bongo walipata vipi hiyo hela na walitumia nini kuisafisha hela yao....ITH

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...