Na Mohamed Mhina na Tamimu Adam wa Jeshi la Polisi - Moshi
IGP Mwema amesema kuwa, Jeshi la Polisi halitaweza kuvumilia vitendo kama hivyo viendelee kutokea mahala pengine popote hapa nchini.
Hata hivyo IGP Mwema, amepongeza juhudi za wananchi wa mkoa wa Shinyanga na mikoa mingine jirani kwa ushirikiano wao uliofanikisha kukamatwa kwa majambazi sita kati ya kumi yaliyopora silaha ya Polisi na kuwaua Askari Polisi wawili katika kituo kidogo cha Kagongwa wilayani Kahama na kukimbia.
IGP Mwema alikua akifunga mkutano Mkuu wa Mwaka kwa Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi uliokuwa ukifanyika katika Chuo cha Taaluma za Polisi Moshi mkoani Kilimanjaro.
Amesema ushirikiano huo ukidumishwa katika maeneo mbalimbali, utaliwezesha Jeshi la Polisi kuendeleza bila kuchoka mapambano dhidi ya uhalifu hapa nchini.
IGP amesema kuwa, juhudi za kuyatafuta majambazi mengine manne zinaendelea na kwamba tayari zimeonyesha dalili za mafanikio na muda si mrefu watuhmiwa hao watakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria kujibu tuhuma zao.
Wakati wa Mkutano huo, Maafisa hao Wakuu wakiwemo Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi pamoja na Watumishi raia wa Jeshi hilo, wameweka Maazimio manane ambayo yanalenga katika kusimamia nidhamu na maadili ndani ya Jeshi hilo.
Miongoni mwa maazimio hayo pia ni kuimalisha usimamizi wa rasilimali za Jeshi la Polisi pamoja na kubaini Matishio ya Usalama wa Taifa letu.
Aidha wamependekeza kuimarisha matumizi ya mifumo ya mtandao wa Kompyuta katika utendaji wa kazi za Polisi hasa kwenye nyanja za Upelelezi wa Makosa ya Mitandao na kuboresha mawasiliano.
Aidha amesema kuwa mifumo hiyo itasaidia kujenga uwezo kwa wapelelezi watendaji katika kufanikisha masuala ya upelelezi na usimamizi wa kesi na upatikanaji wa taarifa za wahalifu.
Amewaambia Makamanda hao kuwa ni muhimu kwa kila kiongozi katika ngazi zote kuanzia ngazi ya kituo, Wilaya, Mkoa hadi Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kwenda kutoa elimu ya utekelezaji wa maazimio ya mkutano huo.
IGP Mwema amesema kuanzia leo kila Askari, Mkaguzi na Afisa ni lazima awe ni sehemu ya suluhisho la matatizo yanayowakabili katika himaya zao na kinyume cha hivyo basi mtendaji huyo ndiye atakuwa sehemu ya tatizo husika.
Wakati wa mkutano huu pia, washiriki wamepata fursa ya kutambua matishio ya usalama na kuibuka kwa aina mpya za uhalifu hapa nchini.
Naye Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini Kamishna Robert Manumba, amewataka Makamanda hao wa Polisi wa Mikoa, mara warudipo katika vituo va vya kazi, wakahakikishe kuwa, wanapata nafasi ya kuwasikiliza wananchi na kupokea mawazo na ushauri wao ili kuwawezesha kupata kukabiliana na uhalifu ukiwemo wa majambazi wenye silaha.
Kamishna Manumba amesema kuwa kama kila Kamanda atakuwa karibu na wananchi, itakuwa rahisi kwao kupata taarifa za kihalifu pamoja na nyendo za watenda makosa.
Mkutano huo wa siku tatu ambao ulifunguliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani Mh. Shamsi Vuai Nahodha, uliwashiirikisha Maafisa Wakuu wa Jeshi la Polisi pamoja na Watumishi Raia wa Wizara ya Mambo ya Ndani ambapo pia walikuwa wakiangalia changamoto na mafanikio kwa mwaka uliopita na kupanga mikakati mipya ya kukabiliana na wimbi la uhalifu hapa nchini.
hawakuiva hao, ongeza ukali wa mafunzo na pata wanafunzi bora siyo form 7 au div 5.
ReplyDelete