Na Dixon Busagaga,Arusha.
CHUO kikuu kishiriki cha Ushirika na Biashara(MUCCOBS) cha mjini Moshi kimekiadhibu chuo cha IAA cha mjini Arusha katika michezo ya kirafiki iliyofanyika katika viwanja vya IAA mjini Arusha.
Katika michezo ya aina tatu iliyochezwa chuoni hapo MUCCOBS ilichomoza na ushindi mkubwa katika michezo ya mpira wa mikono na mpira wa kikapu huku IAA wakifanikiwa kujinasua na aibu ya uwanja wa nyumbani kwa kuchomoza na ushindi katika mchezo wa mpira wa miguu.
Katika mchezo wa mpira wa mikono timu ya MUCCOBS ikiongozwa na Deusdedith Doto,Losivu Molel ,Gosbeth Maro na Jimmy ilifanikiwa kuichapa IAA seti tatu kwa moja.
Kwa upande wa mpira wa kikapu ,licha ya IAA kuchezesha vikosi viwili,vijana wa Muccobs wakiongozwa na wachezaji wake tegemezi Deo,Kilaza na K waliweza kuifunga IAA kwa jumla ya vikapu 40 kwa 34.
Hata hivyo hali ilikuwa tofauti kwa upande wa mpira wa miguu ambapo timu ya IAA waliweza kuutumia vyema uwanja wake baada ya kuchomoza na ushindi wa mabao 2 kwa 1.mabao ya washindi yakipachikwa kimiani na mshambuliaji wake hatari Meshaki huku lile la kufutia machozi kwa upande wa Muccobs likifungwa na Yahaya.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa michezo hiyo naibu waziri wa michezo na burudani wa serikali ya wanafunzi wa chuo kikuu kishiriki cha ushirika na biashara(MUCSO),Omary Sambiga alisema lengo la michezo hiyo ni kuendeleza ujirani mwema kati ya vyuo hivyo.
Alisema mbali na ujirani mwema pia michezo hiyo ilikuwa na lengo kuzipatia timu za mpira wa mikono,kikapu na mpira wa miguu michezo ya nje ya chuo kutokana na kucheza michezo mingi katika uwanja wake wa Ushirika kwa takribani miaka minne sasa.
“Tumeamua kuja kucheza na wenzetu IAA kutokana na kwamba timu zetu hizi kwa zaidi ya miaka minne zimekuwa zikicheza michezo ya ndani ya chuo pekee,tukaona ni vyema tutoke na sisi”alisema Sambiga.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...