Jumuiya ya watanzania waishio nchini Switzerland (TAS-Tanzanian Association in Switzerland) usiku wa tarehe 30 mwezi April 2011 waliandaa harambee kwa ajili ya kutunisha mfuko wa chama ili kupata uwezo wa shughuli mbalimbali kama ilivyoanishwa katika katiba ya Umoja wao, ikiwemo elimu kwa ajili ya wasiojiweza. Sherehe hiyo ilifana sana kwani ilihudhuriwa na watu zaidi ya 200 wa rika tofauti kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Wageni waliohudhuria walipata nafasi ya kujionea na kununua vitu mbalimbali kutoka Tanzania vikiwemo khanga, vitenge, vinyago, tingatinga na vitu vingine vinavyoonyesha utamaduni wetu wa kitanzania. Pia waliweza kula chakula kizuri cha kitanzania kilichoandaliwa na wana-TAS. Sherehe ilinoga zaidi kutokana na dansi la nguvu lililoonyesha staili ya ‘’mduara’’ iliyowavutia sana wageni kutoa mabara mengine.
Kama mdau niliyehudhuria nilifurahishwa sana jinsi sherehe hiyo ilivyoandaliwa na utaratibu mzima wa shughuli ulivyokuwa. Napenda kuchukua nafasi hii kuushukuru Uongozi wa TAS, wanaTAS wote pamoja na wote waliohudhuria kwa umoja na ushirikiano wao kuweza kufanikisha harambee hiyo. Mungu ambariki kila mmoja wenu . Ni wazi kuwa watu wanapenda kuweka vikwazo vingi katika uanzishwaji na ustawi wa jumuiya za kitanzania huku ughaibuni na wanasahau matunda mazuri ya kuwa na umoja.
Napenda kutoa changamoto kwa watanzania walioko Uswiss kuendeleza mshikamano huu kwani kutokana na matukio kama haya watu wanazidi kufahamiana na ndipo wanaweza kusaidiana na pia kuwaachia urithi mzuri vijana na watoto wao wanaokulia ughaibuni. Pia napenda kuwashauri watanzania ambao wako popote pale nje ya nchi waendeleze mshikamano ambao utaweza kuwaweka karibu zaidi na kuweza kusaidiana katika mambo mbalimbali ya kijamii. Nina imani kipato kitakachotokana na harambee hii kitawasaidia kufikia malengo yao na kwamba kidogo watakachotoa kusaidia kule nyumbani kitaamsha ari ya wengine kuiga mfano huu mwema.
MUNGU IBARIKI TAS, MUNGU IBARIKI TANZANIA.
Mdau Uswiss.
haya ndo mambo tunapenda kuona. Hongereni wabongo uswiss.
ReplyDeleteHongereni sana, haya ndo mambo siyo yanayoendelea huku niliko, mnaonekana mko so organised. I love it, mmenikumbusha mbali sana enzi nikiwa Tz na huu wimbo
ReplyDelete