Meneja wa benki ya KCB Tanzania tawi la Morogoro, Carlos Msigwa akimkabidhi mti Kaimu Afisa Elimu mkoa wa Morogoro, Bakari Hamis wakati wa zoezi la upandati miti 600 kwa shule ya msingi Msamvu B kati ya 21,000 iliyotolewa na benki ikiwa ni muendelezo wa kampeni ya upandaji iliyozinduliwa na benki hiyo hivi karibuni Chanika Msongola jijini Dar es Salaam.
Mjumbe wa Kamati ya shule ya Msingi Msamvu B, Nassoro Korwe akisisitiza jambo mara baada ya kukamilika kwa zoezi la upandaji miti 600 iliyotolewa na Benki ya KCB Tanzania tawi la Morogoro. Kushoto ni Kaimu Afisa Elimu mkoa wa Morogoro, Bakari Hamis na kulia ni Meneja Muendeshaji wa benki hiyo Hogla Laiser.
Na Mwandishi Wetu
Katika kuunga mkono juhudi za serikali kwa kuhifadhi mazingira na kulinda vyanzo vya miti ya asili Benki ya KCB Tanzania Tawi la Morogoro imeitikia wito huo kwa kupanda miti 1,350 yenye thamani ya shilingi Milioni 3.5/-.
Miti hiyo imepandwa katika shule za Msingi Kiegea, Mibulasi na Msamvu B zote za mkoani Morogoro zoezi lililoendeshwa kwa ushirikiano wa Wafanyakazi wa benki hiyo, Walimu, Wajumbe wa kamati za shule, wanafunzi, wazazi na Kaimu Afisa Elimu mkoa wa Morogoro, Bakari Hamis na Watendaji wa Wakala wa Mbegu za Miti TSA Morogoro.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa zoezi la upandaji miti, Meneja wa Benki ya KCB Tanzania tawi la Morogoro Carlos Msigwa amesema kuwa benki yake imejikita kwenye upandaji miti kutokana na baadhi ya watu kuona mazingira sio jambo la msingi kwao.
Msigwa amefafanua kwamba mabadiliko ya tabia nchi yanayochangiwa na kukua kwa shughuli za kibinadamu jamii isipopambana na kuidhibiti hali hiyo kwa kupanda miti na kuacha kuharibu maziungira jangwa na maafa vitazidi kutokea.
“Kupanda miti katika maeneo ya shule sio tu kunalinda mazingira, bali pia kunaepusha shule kuezuliwa mapaa na vimbunga ama upepo mkali. Vilevile wanafunzi mbali ya kujipatia matunda wanaweza kujipumzisha chini ya miti kwa ajili ya kujisomea,” alisema Meneja Msigwa.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya shule ya Msingi Msamvu B, Nassoro Korwe ameziomba taasisi zingine kuiga mfano huo kwa kuisaidia shule hiyo kukabiliana na changamoto zingine zinazojitokeza.
Akitaja baadhi ya changamoto Mjumbe Korwa amesema licha ya Benki ya KCB Tanzania kuwapandia miti wanakabiliwa na ukosefu wa maji kwa ajili ya kumwagilia miti hiyo ili isife kwa ukame.
“KCB Morogoro tayari wametupandia miti, tunaomba wahisani wengine wajitokeze kutusaidia upatikanaji wa maji kwa kipindi cha mwanzoni ili wanafunzi wayatumie kumwagilia miti. Hilo lisipofanyika mchango huu wa wahisani utakuwa umepotea bure.
Katika hatua nyingine Kiranja mkuu wa shule hiyo Hadija Maganga ameishukuru benki hiyo kwa msaada huo na kusema sasa watakuwa katika mazingira safi na salama kwa ajili yak masomo.
Mbali na hilo alitumia fursa hiyo kuuomba uongozi wa benki hiyo kuangalia namna ya kuisaidia shule hiyo madawati ili kukabiliana na tatizo la baadhi ya wanafunzi kubanana ama kukaa kutokana na upungufu wa vifaa hivyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...