Uncle Michuzi naomba uniwekee mada hii ili wadau wenzangu wachambue..
Kama mwanafizikia katika masuala ya kiatomiki-asilia (quantum) nimeweza kutambua umuhimu wa amani katika mfumo wa viasili ambapo kuna sheria maalum za kifizikia ambazo hufuatwa. Sheria hizo huhakikisha kuna kuwa na msawazo-suluhishi (homogeneity) kati ya viasili hivyo.
Utauliza kweli hayo mkuu? Jibu ni kweli kwasababu japo viasili havipendi kukaa pamoja (fermions) lakini kutokana hali halisi ya mazingira hufikia muafaka wa kuishi pamoja kwa amani hali ambayo hata sisi wanadamu ambao tumetengezwa kwa viasili hivyo tunakuwa katika mazingira ambayo hatuna chaguzi zaidi ya kuishi pamoja kwa amani japo tuna tofauti nyingi.
Kitu kinachotufanya tuishi pamoja ni uvumilivu kati yetu kwa kupuuza tofauti zetu na kuimarisha yale yanayotufanya tuwe kitu kimoja. Katika kuvumiliana ndipo tunapata AMANI lakini UVUMILIVU hutegemea mambo mengi hasa katika jamii yetu ni upatikanaji na ugawanywaji wa mahitaji muhimu ndio hupewa umuhimu mkuu. Kama viumbe wenye fikra tumegawa madaraka kwa kundi la wachache waweze kusimamia mambo hayo na kutuongoza katika kuendeleza hali zetu za maisha.
Uvumilivu ni kama mpira wa manati unapovutika huweza kufanya kazi iliyokusudiwa. Lakini UVUMILIVU unaweza kutafsiriwa kama WOGA katika hali Fulani kwani kama ni foleni basi nyuma ya Uvumilivu ni Woga na mbele yake ni Unyama. Kwa hiyo jamii yeyote lazima itazame kwa uangalifu mipaka ya AMANI inayotokana na uvumilivu. Nchi yetu inasifika kwa kuwa na amani inayotokana na uvumilivu wa hali nyingi hivyo kuifanya nchi yetu iwe ni yenye uvumilivu mkuu kati ya wanajamii na pia kuwa na hatari kuu mara mipaka ya uvumilivu huo ikivukwa.
Nchi yetu ina makabila zaidi ya mia moja na pia kuna wafuasi wa dini mbalimbali pia kuna watu wa rangi mbali mbali na pia upatikanaji wa mahitaji muhimu katika maisha pia yamegawanyika mara nyingi kufuata tofauti tulizonazo. Sitaki kunyoosha kidole kwa kabila, dini ama rangi yeyote lakini ukweli unabaki kuwa tofauti ya walionacho na wasionacho ni kubwa.
Hii inaonekana katika miji yetu mikubwa kuwa kuna tabaka la watu ambalo linaundwa na viongozi waliochaguliwa na wanajamii kuhakikisha kuna masawazo wa upatikanaji wa mahitaji muhimu lakini badala ya kutetea matakwa ya jamii wameelemea kutetea wazi wazi maslahi binafsi.
Hali hii ni hatari kwa uwe mvutiko (strain) wa uvumilivu kwa maana ukivuta sana mpira wa manati hukatika na mara nyingi matokeo ni majeraha kwa mvutaji. Hapa nataka kusema kuwa ile simenti inayoshikilia amani inayotokana na uvumilivu inaanza kumemenyuka. Hata katika viasili mvutiko (strain) unapozidi basi hufumka kwa kishindo kikuu ili amani ije ipatikane tena (relaxation to ground state).
Kwa sisi binaadamu ina maana uvumilivu ukipotea jamii itaingia kwenye eneo la unyama ambapo maisha na mali za wanajamii zitapotea kabla ya miaka kupita na kupata suluhu ya kuvumiliana tena. Tumeona hali hii ikitokea kwenye nchi nyingi kama Rwanda na Burundi, Sudani na kwengineko lakini ishara zake zimeanza kujitokeza nchini kwetu, mfano ni mauaji wa watu waliokwenda kuvunja nyumba pale Tegeta, mauaji ya Tarime na kwengineko.
AMANI inayotokana na uvumilivu inatoweka kila siku zinavyopita kiasi sasa naweza kusema sasa tunaingia kwenye amani inayotokana na WOGA. Na cha hatari zaidi WOGA ni hali tete (unstable state) ambayo si vyema kukaa nayo maana WOGA ukitutoka tunarukia kwenye UNYAMA ambao matokeo yake ni mauaji ya halaiki na upotevu wa mali na kurudisha nyuma hatua zote zilizotifikisha tulipo. Tujifunze hali iliyopo LIBYA na kwengineko ambako walikuwa na amani inayotokana na WOGA leo wameushinda WOGA wao na nchi imetumbukia kwenye vita kufuta maendeleo yote waliyopiga.
Sitabiri balaa lakini kwa mwenye akili ya kusoma nyakati atatambua kuwa tunaelekea huko kwenye balaa hali tunajua taathira yake. Leo hii vyama vya siasa vimekusanya ushawishi mkubwa kwa wananchi ambao hali zao ni duni badala ya kuweka maslahi ya wananchi mbele wameweka maslahi yao binafsi mbele zaidi kiasi maisha ya mwananchi wa wakaida yamekuwa magumu mara nyingi zaidi ya miaka iliyopita. Uchaguzi unaokuja 2015 utakuwa ni mtihani mkuu wa AMANI tuliyonayo.
Leo hii Wazazi wanashindwa kulea watoto wao hivyo watoto omba omba wanazidi kuongezeka. Wazazi wanashindwa kusomesha watoto. Vitendo vya kihalifu vinazidi kuongezeka na hivi ndivyo vitakavyoondoa WOGA na kututumbukiza katika janga.
Zamani wananchi hawakujua nini kinachoendelea lakini dunia ya leo yenye mitandao na njia nyingi za mawasiliani zimefumbuwa macho na masikio ya wengi na hivyo ni jukumu la viongozi wetu kujua kuwa matokeo huwa ni vitendo vilivyofanywa kabla (CAUSALITY).. ili tupate matokeo mema tubadilishe vitendo vyetu vya sasa na kutimiza majukumu yetu kwa faida ya TAIFA letu na Wananchi wetu. Hoja zenye kutetea wananchi zinaposhindwa bungeni kwa utashi wa siasa ujue ndio chachu ya kutokomeza WOGA uliopo na kulikurubisha taifa katika uvunjifu wa AMANI.
Ndimi Mdau Saidi Ally Saidi aka Mwanafunzi
Hii hoja hachangii mtu iko nje ya uwezo
ReplyDeleteHongera sana ndugu yangu kwa kutoa ukweli na jua watu wengi wataanza kuponda lakini siku ikifika wote watakubali.Mimi nilishatoa hiyo tahadhari miaka mitatu iliyopita na watu walikuja juu kuwa sisi hatuwezi kufanya hivyo ikabidi niachane nao kutokona na upeo wao wa kufikiri.Tatizo liko kwa viongozi kuwa na tamaa kupita kiasi na kutojali wananchi.Mfano,kukiwa na mradi wa kujenga au kutengeneza kitu fulani basi viongozi watakula pesa hadi mradi hautekelezwi.Unaweza kula 10% lakini wao wanakula 125%.Tatizo kubwa sasa hivi wananchi hawalioni ni kwa serikali kuuza ardhi yetu kwa watu wa nje,mali halisi(madini,dhahabu,mbuga za wanyama)kwa raia wa nje amabao hawana uchungu wakuzilinda na kuhifadhi kwa vizazi vya mbeleni.Angalieni mfano wa South Afrika wanavyochunga mbuga zao za wanyama,angalieni Bostwana wanavyochunga Almasi yao,nk Sisi tumekuwa ni shimo la kila mtu kuja na kuchuma mali na kujenda kwao.Mfano kampuni ya Barrick wanachimba gold lakini wananchi wa shemu hiyo hawafaidiki na kitu chochote, hakuna hospitali nzuri,hakuna shule nzuri, na huduma zozote zile muhimu kwa binadamu wa kawaida hakuna. Kuhusu wawekezaji sio kwamba nawapinga ila inabidi tuwe na sheria ambazo ziko wazi ili waweze kukubaliwa,kwamba baada ya miaka 5 bila ya kulipa kodi ikiisha na wakiwa hawataki tena kuendelea na uwezekaji basi lazima walipe kodi za nyuma,hawaruhusiwi kuuza mkataba kwa mtu yoyote yule ila kuurudisha kwa serikali,hawatalipwa fidia kwani wao ndio wamekatisha mkataba.Pia wakati wa kupewa mkataba lazima wawe na mtanzania mmoja katika kampuni yao ili yeyey awajibike iwapo watakiuka taratatibu za mkataba.Nimesema hivyo kwa sababau haya makampuni kila ikifka mwisho wa mwaka wa tano wa kuanza kulipa kodi wanasema tunaanmua kuuza mkataba kwa kampuni nyingine,ili wakwepe kulipa kodi na hiyo kampuni nyimgine ni wao wenyewe ila wanabdilisha jina.Tufungue macho na tuwaondoe viongozi wasio jali rasilimali zetu na sisi wananchi.
ReplyDeleteHii ni sahihi kabisa. Ila jambo moja la sisi watu weusi sio tabia yetu yakusoma nini kinataka kutokea na kifanyike nini kuzuia. Hilo halipo, kwani tunaamini kila kitu kinatokea kwa mipango ya MUNGU!!! Sasa mimi huwa najiuliza, huyu MUNGU mbona anamipango mibaya kwa watu weusi tu? Lakini nimegundua ya kwamba sisi ni wavivu wa kufikiri na huwa tukishiba leo hatufikiri mwakani tutashibaje. Mfano, tatizo la umeme halikuanza leo na data zote tunazo za muelekeo wa hali nchi siku za usoni tangu mid 1990's. hakuna kilichofanyika na kikubwa ni kuingia kwenye mikataba inayoweka nchi pabaya zaidi. Na tusubiri tukikesha kumwomba bwana kwani nchi inaendeshwa kisanii na madhara yake yanaweza kuwa jangwa. January wa Makamba unasoma haya?
ReplyDeleteAsante sana Said, Umenikuna sana hasa pale ulipotumia mfano wa mvuta manati akivuta sana na kuufanya mnati ukatike na yeye mwenyewe awe kwenye hatari.
ReplyDeleteNakumbuka zamani nikichunga ng'ombe malishoni tulitumia sana manati kuwindia ndege, na mara nyingi tulivuta sana manati ili kurusha mawe mbali zaidi kuwapata ndege,lakini kinyume chake manati yalipovutwa sana yalikatika na hatimaye kutuumiza wenyewe.
Said, naamini ulichosema ni sahihi kabisa.Kama ulivyosema kuwa hutabiri balaa litupate,nami nasema hakuna mtu anayejitabilia balaa limpate, ila ulichosema kinaendana sana na dalili ya mvua ni mawingu kama ulivyoainisha kwa mifano mbalimbali ya nchi za wenzetu wanaopitia makali hayo na wale waliopitia hali hizo na hatimaye yale yanayojiri kila kukicha nchini kwetu.
Sina ushauri wa nini kifanyike ila mimi kama mcha Mungu napeleka kilio cha maombi yangu kwa Mungu tu ndiye atakayetunusuru maana kizazi hiki hata useme ni kama unampigia mbuzi gitaa ambaye kamwe hatacheza. Kama ni kelele zimeishapigwa sana na kunyooshewa vidole watu,lakini utashangaa kuwa wote wanyoshaji vidole na wanyoshewa vidole wameoza. Kutoa kibanzi jichoni kwa mwenzio wakati wewe una boriti ni kama ndoto ya ndaria.
Labda kama Watanzania wataamka vizuri kuelewa haki zao za msingi na wakajua namna ya kizitetea pasipo kuangalia nani ni nani yangu, na nani ni muwajibikaji na nani ni mkombozi wao wa kweli na kuchukia mikumbo na mirungura labda tutapata mtu atakayetupigania na kuturudishia imani ya umoja na uvumilivu ulioutaja ambao ni kiungo muhimu sana katika kujenga amani na utulivu.Lakini dhiki na chuki na dhuruma zikikithiri uvumilivu utakoma na watu watachukua uamuzi usio wa busara.
Asante said, na nakuomba usikate tamaa kuleta maada kama hizi tena kwa lugha nzuri na yenye tija ambayo watanzania wahusika wengi wataielewa vema kwa kile unachotaka kuwapasha.
hii mada imeleta kigugumizi kwa wachangiaji kwasababu somo limeeleweka..hapa hakuna kuosha kinywa ukweli ndio huo..ahsante ndugu kwa kutuelimisha.
ReplyDelete