Mengi wanayosema na kuyaamini wa-Tanzania kumhusu Mwalimu Nyerere ni majungu. Hayo nimeyafahamu kwa muda mrefu. Ni wajibu wetu kuandika habari sahihi kuhusu Mwalimu Nyerere kama ilivyo kwa masuala mengine yoyote. Nami, kwa kuanzia, nimechapisha kitabu kiitwacho CHANGAMOTO, ambamo, pamoja na mengine yote, kuna makala na dondoo mbali mbali kuhusu Mwalimu Nyerere.

Kati ya majungu ambayo yanavuma sana ni kwamba Mwalimu Nyerere hatimaye alikiri kuwa Ujamaa umeshindwa. Madai haya yanasikika vijiweni, na nimewahi kuyaona kwenye maandishi pia, kama vile blogu, na gazeti la An Nuur, ambamo kauli alizozitoa Mwalimu Nyerere katika mahojiano na CNN zimenukuliwa, lakini sio kwa usahihi.

Ninavyojua, Mwalimu Nyerere hakuwahi kusema kuwa Ujamaa umeshindwa. Ninajiamini kabisa kwa hilo. Napenda kutangaza kuwa yeyote atakayeleta ushahidi kuthibitisha kuwa Mwalimu Nyerere alikiri kuwa Ujamaa umeshindwa aulete ushahidi huu hapa kwenye blogu yangu. Ikidhihirika kuwa ushahidi umetolewa, nitampelekea mhusika dola 100 kama kifuta jasho na shukrani yangu, kwani atakuwa amenielimisha kwa jambo ambalo sikulijua. Ninathamini sana elimu.

Tangu nilipoanzisha blogu hii, nilitamka kuwa shughuli yake mojawapo itakuwa nikumwenzi Mwalimu Nyerere. Kuyaanika hadharani majungu dhidi ya Mwalimu Nyerere ni sehemu ya kazi hiyo. Naanza na majungu niliyoyataja hapa juu. Kazi kwenu.



Kupata chanzo BOFYA HAPA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 28 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 02, 2011

    Umekuwa creative sana kwani watu wanamdhihaki mzee wa watu wakati alijaribu ndoto zake kwa nia njema na alionesha moyo wa uzalendo. Kitu ambacho wengine wameshindwa. Tumebaki kukopi tu bila hata kupest. Manake tunpest hivyo tulivyokopi maendeleo yangeonekana.

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 02, 2011

    Baada ya kustaafu, Mwl. Nyerere alipata kuhojiwa na TVZ au Televisheni Zanzibar. Alipoulizwa juu ya sera za uchumi za Ujamaa na Kujitegemea alizokuwa akiziendesha wakati akiwa Rais, akajibu kwa kukubali kuwa sera hizo "zilishindwa". Interview hii niliishuhudia mimi mwenyewe. Ukitaka waulize TVZ kama wana kumbukumbu. Ila hizo dola zako 100 kaa nazo tu. Alhamdulilah, Mola ameniruzuku za kutosha. Ukipenda toa sadaka.

    ReplyDelete
  3. AnonymousJuly 02, 2011

    Unataka kutuambia kwamba sera za ujamaa na kujitegemea zilifaulu? Au cha muhimu kwako ni kwamba Nyerere hakuwa na ushujaa wa kukubali zilifeli?

    Prof. Mbele, ukitoa ushahidi kwamba watanzania hawakula Unga wa Yanga, hawakupiga mswaki kwa kutumia vijiti na mkaa, hawakusimama foleni ndefu kwa ajili ya nusu kilo ya sukari na hawakuvaa malapa ya tairi za gari nitakupa zawadi ya Wembe! (Ulikuwa shida wakati wake!)

    ReplyDelete
  4. AnonymousJuly 02, 2011

    Nyerere ni kiongozi imara.Yeye akushindwa ujamaa ila wanaompinga ndiyo wameshindwa na wanaishi sasa.
    Nchi zote tajiri duniani zinaumoja na umoja ni moja ya viungo vya ujamaa.
    Wa TZ tunatakiwa tuwe na ujamaa na upendo ili tusonge mbele.
    Tupendane ,bila ya hivyo hakuna cha maendeleo kamwe.
    Ujamaa aliokuwa anausema JK ndio huo,na yeye hakushindwa.
    Ndiyo maana Tanzania ni nchi ya kwanza kwenye hatua ya kufuta ukabila barani Afrika.
    Anayepinga aende LIberia aone kunaendelea nini kule.
    Tumebakisha hatua mbili tu tunaweza kufikia kwenye kile mwanadamu anaita maisha bora na maendeleo (UPENDO)UJAMAA kama amkumwelewa mzee mzima.
    Pia mkumbuke nyerere alikuwa anawekewa vikwazo vya misaadandiyo maana tulikuwa na shida kwa kiwango fulani na hii ilitokana na Tanzania kusaidia ukombozi wa Kusini mwa Afrika,kitu ambacho tunatakiwa tujivunie.
    Tokea lini watanzania tukawa na tabia ya kuwasimanga wazazi wetu?Huyu ni moja wa wa zazi wa Taifa letu.
    BABA WA TAIFA ´LA TANZANIA NI JK NYERERE.

    ReplyDelete
  5. AnonymousJuly 02, 2011

    Mzee umesema sawa, Ujamaa haukushindwa. Ila Mwalimu alizungukwa na walaji, na watu ambao kwa kweli hawakuwa na kiwango cha kumuelewa. Ilikuwa ni: kikulachi ki-nguoni mwako. Zaidi ya hapo TZ kama nchi maskini au changa ilijihusisha sana na jambo jema la ukombozi wa nchi zote zilizokuwa zinapigania uhuru wakati huo, hasa zile za kusini mwa bara la Afrika. Kwa maana hii Mwalimu hakuwa mu-binafsi, kama kiongozi shujaa na mashuhuri alitufanya waTZ pia kama Taifa moja tutupilie mbali ubinafsi. Hili liliwafanya wakubwa wa dunia hii kutoipenda TZ. Hivyo kuyumbisha uchumi wa nchi na mipango mingine mingi ya kimaendeleo ya nchi maskini, na TZ ikiwa moja wapo. Enzi za Mwalimu watanzania wote tulijuwa muelekeo wa nchi ulikuwa ni upi. Zilikuwepo sela zilizokuwa zinaweza kutathiminiwa, kulikuwa na misemo ya kuwatia moyo wananchi na kuwachochea katika kuipenda nchi, wananchi walijisikia kama watoto wanaotoka kwenye familia ya baba na mama mmoja. Familia iliyosimama imara. Awamu ya kwanza ilibuni miradi mingi ya kimaendeleo iliyo kuwa inamilikiwa na wananchi wenyewe. Yeye mwenyewe Mwalimu kama kiongozi mkuu alijuwa wazi kuwa kasi ya maendeleo kwa kipindi cha miaka kumi tangu TZ ilipopata uhuru ilikuwa kubwa, kwa hivyo basi aliwaalika wakoloni na marafiki wa TZ kuja kuona tulipokuwa tumefikia katika miaka kumi baada ya uhuru. Hakuwaita wakoloni waje kukaguwa, kutegeza au kuwaomba misaada na mikopo. Sisemi kuwa misaada na mikopo haikuwepo. Ila alitaka kuwaonyesha ukweli kuwa TUNAWEZA. Baada ya kumaliza ziara, wakoloni walirudi makwao wakiwa wamejaa hiana, na wakatuvuruga zaidi. Tukumbuke kuwa maendeleo yanaletwa na ushirikiano kati ya mataifa mbalimbali, ushirikiano huu lazima uwe wa haki. Mkubwa awe na wajibu wa kumtendea haki mdogo. Bila haki toka kwa mkubwa basi mdogo hawezi kwenda popote, au kwa kifupi mkubwa asimhujumu mdogo. Hii inaeleweka hata kwenye maisha yetu ya kila siku: kazini, biashara, mashuleni, michezoni, ndoa, familia, makanisani, misikitini, vyama n.k.
    Shule na matibabu, Taifa lilibeba majukumu pamoja na uchanga wake! Kweli mtu mwenye akili zake hawezi kuthubutu kusema Ujamaa ulishindwa. Enzi za awamu ya kwanza nakumbuka majila ya asubuhi na jioni kuanzia saa kumi na kuendalea, Dar ilikuwa inapambwa na mabasi ya usafiri wa wafanyakazi wa mashirika ya umma kama: Benki kuu, NBC, THB, Nasaco, TRDB, TRC, Sigara, Bora, Urafiki, Sungura, Posta, Wazo, Kizaku, Keko madawa, Chibuku, Bima, Tanesco,Orodha inaendelea......Leo wapi? Mimi nanyamaza.

    ReplyDelete
  6. AnonymousJuly 02, 2011

    Hawa watu wengine wanamfanya huyu Nyerere kama Mungu mtu wakati si kama kafanya kitu cha ajabu mpaka kikapigiwa mfano ni kiongozi tu wa kawaida ambae alikuwa anaongoza watu anavyotaka yeye, usiangalie mazuri mawili aliyoyfanya angalia pia na mabaya mangapi aliyoyafanya. Utashangaa hivyo watu wanavyomsifu wakati kwa mtazamo wangu namuona mtu wa kawaida tu manaake tangu nimezaliwa mpaka leo sijawahi kuona Tanzania ina maendeleo mpaka hivi ninavyozungumza wakati tuna rasilimali za kutosha. Mnk Tanzania tusijilinganishe na nchi nyengine za kiafrica hata kidogo, sijawahi kusikia Tanzania tukapigana vita, isipokuwa vya Uganda ambavyo tulivitaka wenyewe lakini hakuna vita vya wenyewe kwa wenyewe hata uchumi wetu ukaenda chini, kwa hivyo hakuna sababu hata moja tukawa maskini Tanzania isipokuwa hatujawahi kupata kiongozi wa maana tu, kuko kusifu lakini si mpaka tena mtu tukawa tunamuabudu. Nyerere ni kiongozi kama viongozi wengine tu

    ReplyDelete
  7. AnonymousJuly 02, 2011

    Ndg Mwandishi, shida yako ni kutaka kusikia kauli ya Nyerere mwenyewe kwamba ujamaa ulishindwa au ni kutaka kupata maoni ya watu kuwa ujamaa ulishindwa? Mimni binafsi naona ujamaa ulishindwa hata kama mwalimu mwenyewe hakukiri hivyo. Na sababau za kushindwa sio mwalimu ni watu waliopewa madaraka wakayatumia vibaya. Ama wengine hawakumuelewa alichokuwa anataka ama waliona ni kitu kigumu kwao. Ujamaa unahitaji uvumilivu na ushirikiano baina ya wadau mbalimbali. Kama hakuna mambo hayo ni wazi tu ujamaa ungeshindwa. Lakini kwa wale wanaomlaumu mwalimu kwamba sera hizi ndizo zimesababisha nchi ama wao kuwa na uchumi duni, wanapaswa wajiulize nchi zingine za Afrika zilizofuata sera zingine kama vile ubepari zina maendeleo ya kutisha kiasi cha kujivunia sera hizo? Mfano mzuri ni Kenya waliofuata uchumi wa kibepari na wakwekeza sana lakini uchumi ukamilikiwa na wageni kwa asilimia 90. Ambapo Tanzania uchumi ulimilikiwa na wananchi kwa zaidi ya 90%. Matokeo yake ni kwamba wanachi wa kenya walikuwa masikini kuliko wa Tanzania. Ni hivi karibuni tu ambapo wamefanya mabadiliko ndipo wananchi wa kawaida wakapata ahueni. Na kwa takwimu za UNDP 2005 zinaonesha kwamba asilimia 50 ya wananchi wa Kenya wanaishi chini ya dola 1 kwa siku ambapo tanzania ilikuwa 36%. Kwa hiyo mimi naona hata tungefuata huo ubepari mnaoutaka pengine watu waili watatu wangekuwa na pesa sana lakini walio wengi tungenyanyasika. Mimi nampongeza Nyerere kwa kujaribu kama ambavyo JK amekuwa akijaribu japo hajafanikiwa.

    ReplyDelete
  8. AnonymousJuly 02, 2011

    hehe dola 100 zako kazitoe sadaka ila mwalimu alichemsha ukweli ndio huo tusisahau kuwa watu walikula yanga na sukari ya maji ya miwa na mafuta ya nazi

    ReplyDelete
  9. AnonymousJuly 02, 2011

    Anony unayesema nyerere alichemsha unaruhusiwa kutoa maoni yako kadiri utakavyo. Lakini naomba nikuulize vijiswali vifuatavyo. Hivi ulitarajia Nyerere ajenge uchumi kwa pesa ipi wakati wakoloni hawakuacha kitu? Mkoloni wa kwanza alikuwa Mwarabu, alifanyia nini Tz zaidi ya kujitajirisha kwa kuchukua watu wetu tumwani. Mkoloni wa pili alikuwa Mjerumani, huyu alijaribu japo na yeye nia yake ilikuwa kupora tu na kupeleka kwao. Mkoloni wa tatu alikuwa mwingereza, huyu alikuwa n na nyumba mbili za kuhudumia kwa rasilimali za Tz, ya kwanza ilikuwa nchi yake ya Uk kwa mama yake, ya pili ilikuwa makao makuu yake akiwa East Africa ambayo ilikuwa Kenya. Kwa uporaji huo Tz ilibakishwa haina kitu. Sasa ulitaka Mwalimu aanze kwa pesa ipi? Kumbuka alikuwa ni mtu asiyependa kupewa misaada yenye masharti. Pili alikuwa hataki ukoloni wa aina yoyote uendelee. Ndio maana alimkataa Muisraeli kwa kuwa na sera zake za kumbagua Mpalestina. Kwa mtaji huo ilikuwa lazima tule kilichopatikana wakati huo. Mnaolaumu hiyo hali ndio ninyi baba zenu walifilisi viwanda na mashirika ya umma wakapeleka kwenye matumbo yenu. Ninyi ndio mlichngia hali kuwa ngumu zaidi.

    ReplyDelete
  10. AnonymousJuly 02, 2011

    Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. huyu marehemu alijaribu na alikuwa na nia ya dhati katika kuleta maendeleo ya tanzania. Leo hii wako wapi wenye nia ya dhati ya kuleta maendeleo ya tz kama sio Jakaya Kikwete, Zitto Kabwe, Dr. Slaa na Tundu Lissu?

    ReplyDelete
  11. AnonymousJuly 02, 2011

    Tatiazo la Prof Mbele ni ukatoliki wake, wenzetu hawa hata panya mradi ni wakikatoliki watakata kuwa hali nafaka. Aidha prof alikuwa mtoto sana au alikuwa kwa kipindi hicho yuko kwenye koma, sie tuliowengi tulimsikia kwa masikio yetu akisema kuwa ujamaa umshindwa kama ulivyo ukatolika shindwa, hii ni kweli kwa maneno yake binafsi. Hata hivyo tafuta kwenye archives kwa vianzo vilivyotajwa hapo chini, huenda wao waka hitaji hiyo dola 100 yako!


    Mkuu, kuna nukuu za gazeti la Msemakweli toleo nambari 013 la Jumapili Juni 7-13, 1998 yenye kichwa cha habari,"Nyerere adai Ujamaa na Ukristo vimeshindwa" likinukuu mahojiano yaliyofanyika katika kipindi cha maswali na majibu katika television ya CNN.

    ReplyDelete
  12. Kwa watu makini, suala la umuhimu wa kuhifadhi historia halina ubishi. Suala la kuhifadhi kumbukumbu kwa usahihi kabisa halina ubishi. Suala nililoleta linahusu kauli za Mwalimu Nyerere. Tunawajibika kuzihifadhi kwa usahihi kabisa. Lakini, kwa suala hili la Mwalimu Nyerere, na masuala mengine, Tanzania tunaaibisha, kwa kupuuzia elimu makini na badala yake tunaendekeza majungu.

    Nitoe mfano mmoja. Wiki hii, wenzetu Afrika Kusini wamechapisha kitabu cha kauli za Mzee Mandela tangu miaka ya zamani hadi ya hivi karibuni. Wahariri wamefanya kila juhudi kuthibitisha kuwa maneno ya Mandela yamenukuliwa kwa usahihi kabisa. Ni mfano wa kuigwa. Soma hapa.

    ReplyDelete
  13. AnonymousJuly 02, 2011

    Ann wa sat Jul 0201:37:00pm2011 Umesema "Nyerere alichemsha" Kama Nyerere alichemsha, basi wewe umepooza kabisa.

    ReplyDelete
  14. AnonymousJuly 02, 2011

    Profesa, hivi unataka ushahidi wa "Mnyamwezi" (oooops samahani!) ndiyo uelewe kwamba Mwalimu alishindwa sera zake? Na kuna ubaya gani watu wakisema ameshindwa wakati ni kweli (labda kama umezaliwa baada ya mwaka 1980 kwa hivyo hukumbuki hizo shida). Unaweza kuongezea kwa kusoma kitabu cha Profesa Omari.

    Mbali ya ushahidi aliyokuanikia namba mbili, vile vile jaribu kutafuta clip ambayo alifanya interview katika nchi za Scandinavia (anza na Sweden) kwenye mwaka 86-87 (baada ya kustaafu). Hapo kwa kumbukumbu zangu alikiri kushindwa kwa sera za ujamaa na kuzitolea sababu nyingi, na vile vile kukiri kuchemsha kwa kuondoa vyama vya ushirika.

    Yeye ni binaadamu kama wengine na mengine hufanikiwa na mengine kushindwa siyo vibaya.

    ReplyDelete
  15. AnonymousJuly 02, 2011

    Namuennzi mwalimu na namsifu kwa kutulisha yanga kwani alifanya hivyo ili wananchi wawe wanajilimia chakula chao wenyewe. Naomba mkumbuke ile kampeni ya mvua za kwanza ni za kupandia. Alikataa kwenda kuomba chakula cha mifugo iliwalishwe watanzania. Na baada ya hapo watanzania walianza kulima hata Dar badala ya watu kupanda maua walikua wanapanda mahindi pembezoni mwanyumba. Hii ya watu kula sukari ya miwa sinahaja ya kuijengea hoja. Kwani hata sukari tunayo nunua dukani imetokana na miwa. Mafuta ya nazi ndio mafuta bora kuliko yote katika ngozi na nywele za binadamu. Wengi mnaponunua vipodozi ghali hamfahamu kua mna nunua mafuta ya nazi,maparachichi,mawese,maziwa ya ng`ombe pamoja na kokoa. Tofauti ni kwamba vimeongezwa vikorombwezo, ambavyo mimi naviita danganya toto jinga. Kama huamini angalia kopo la lotion unayotumia ujicheke ujinga wako.

    ReplyDelete
  16. AnonymousJuly 02, 2011

    Ujamaa Nyerere ulimshinda, kama una akili huna haja ya kutafuta ushahidi wa mahojiano kati yake na vyombo vya habari, kama angekuwa ameuweza Tanzania leo hii isingekuwa hapa, wajamaa wa ukweli wote wamefanikiwa na ndio utazame nchi za ASIA nyingi zimefanikiwa kwa kufuata sera hii. LABDA NIKUWEKE SAWA KIDOGO NI KWAMBA NYERERE ALICHOFANIKIWA KATIKA SERA YA UJAMAA NI KUTUUNGANISHA WATANZANIA LAKINI SI KIUCHUMI, NA AMEKAA MADARAKANI MIAKA ISHIRINI NA..... SASA UJAMAA NI MPANA, UNAPOSEMA UJAMAA KUNA MAMBO MENGI SI TU KUUNGANA KWA KUONGEA KISWAHILI, NA KUWA NA NIDHAMU YA UWOGA......THINK BIG HOMMIE

    ReplyDelete
  17. AnonymousJuly 02, 2011

    hata kama walikula miwa na mafuta ya nazi ipi bora kula wali wa kuku kyk vita au kula kula miwa ktk amani

    ReplyDelete
  18. AnonymousJuly 02, 2011

    Hata kama Mwalimu aliwahi kukili kuwa ujamaa ulishindwa, alikuwa anamaanisha kuwa yeye hakuwa na uwezo wa kuwa mahali pote (omnipresent) yaani awe mjumbe wa mtaa (miji kumi) mpaka raisi wa nchi. Yeye alikuwa kiongozi wa nchi nzima, na alikuwa na viongozi wengine chini yake ambao walizembea. Lakini yeye kama mtu aliyekuwa wa kujishusha alikuwa na tabia ya kubeba makosa ya waliokuwa chini yake. Katika mjadala mzima huu, ninapoangalia au kukumbuka sere za Mwalimu na watu waliokuwa wamemzunguka, ninawalinganisha na Yesu wa Nazareti na wanafunzi wake, hasa juu ya hotuba ya mlimani, ambayo wanafunzi wake kumi na wawili hawakuielewa kabisa! Anony wa tisa (9) umesema wazi wanaomulaumu Mwl. ndiyo wale wale babazao walimuhujumu Mwl. Maana ndiyo walikuwa na dhamana ya kuhifadhi rasilimali za taifa na siku zote walitaka kuiba, na kila Mwl. alipowakemea walimuona kama nduli. Hata hivyo diyo hao hao kwa sasa wanatawala, wanakula kile Mwl. alichohifadhi kwa ajili ya taifa zima. Hawajiulizi kuwa kama Mwl. angeamuwa kuwa mwizi leo hii wangekula wapi wao?!Kwa hiyo nyinyi wote mulioko juu mshukuruni Mwl. maana aliwawekea bila yeye kujuwa na muendelee kula kimya. Sawa?

    ReplyDelete
  19. AnonymousJuly 03, 2011

    Anayesema Baba yetu wa Taifa alichemsha anahitaji kutoka au kununuliwa Tv aone hata Kenya walivyo wabaguzi wa kabila hadi leo hii sayansi na technologia hajaweza kujua alichofanya our Mwalimu Nyerere, na pia aminini kuwa hadi leo kuna wananchi wa Tz chakula hawana na Nyerere hayupo nasi. Imagine Nyerere angekuwa ndo Kikwete na Kikwete awe Nyerere? Sasa hivi tu akili za watu zimefunguka na mambo anayoyafanya Rais wetu si haki nchi iko mikononi mwa watu wachache na akili zenu zipo tu alichofanya Nyerere badala ya kusaidia watoto wanaokufa kwa kukosa chakula,matibabu katika nchi iliyopata uhuru 50 yrs ago, eti wamachinga wanafukuzwa wanapewa wachina kuwa wamachinga mnadhani nyerere angefanya hivyo? Huku niliko ukiomba kazi hata kama unavyeti na mzungu hana anapewa kwanza mzungu je haya yapo Tz au mzungu akionekana mnadhani Mungu wenu hata kama alikuwa anafagia kwao Tz itampa kuwa Manager.Kama Nyerere aliweza udini na ukabili haya mengine yangekuja tu.Angalieni mnavyochangia mada zenu kama ulizaliwa juzi hutajua THAMANI YA NYERERE REAL, SO is better to shut up rather than kutueleza uongo. Nchi zingine zinatamani msingi tulioupata kwake. Watanzania tutabakia kuongelea tu vitendo hatuwezi.
    I WILL ALWAYS DO MY BEST TO LOVE HIM. REST IN PEACE MY LOVE ,

    ReplyDelete
  20. AnonymousJuly 03, 2011

    Nilichogundua humu kwenye huu mjadala kuna uislamu na ukristo. Wanampinga Nyerere wengi wanatoka Zanzibar na baadhi ya waislamu wa Tz. Hapo juu kuna mmoja amesema mambo ya ukatoliki. Nadhani kwa fikra kama hii hatutakaa tupate maendeleo ya kweli. Uswahili umetujaa. Fikra za ajabuajabu. Mtu yuko interested na dini badala ya ukweli wenyewe. Jambo likifanywa na Mkristo basi kwa waislamu ni kosa hata kama alikuwa sahihi. Hii si sawa kabisa katika harakati za kutafuta maendeleo.

    Kumbukeni pia kwamba Prof. ameleta mada hii kwa nia ya kutafuta kumbukumbu za Nyerere ili azihifadhi. Ninyi mnaanza kuleta mabezo.

    Jingine mnatakiwa mfahamu kuwa mafanikio ya kimaendeleo hayapimwi katika uchumi tu. Ndio maana kuna social, Economic and Environmental.
    Je katika haya hakuna hata moja lililofanikiwa kwa sababau ya Ujamaa? Kama lipo basi si sahihi kusema ujamaa ulifeli kabisa.

    ReplyDelete
  21. AnonymousJuly 03, 2011

    Ndg yng au mtz mwenzangu mwl nyerere km binaadam kuna mazuri mengi pamoja na mabaya alitoyatenda namsifu sana kwa mema yake na namsamehe kwahayo mabaya kuhusu ujamaa kweli alishindwa ndio maana awamu ya pili ya alhaj mwinyi ikaja na Ruksa kuonyesha kwamba mfumo wa ujamaa umeshindwa

    ReplyDelete
  22. AnonymousJuly 03, 2011

    Hizi mada za nyerere zimeanzia kule kwenye blog ya mjengwa. Huyu profesa mbele akajifanya kumtetea nyerere kule akakutana na "political analysts" wakamtoa "knock-out" hakupost tena na akatoka mkuku bila kuaga. Ndiyo maana amekimbilia huku kwenye wadau wengi wa malavidavi na makamuzi.

    Mbele, onea buzi..., gombe ogopa eenh???

    ReplyDelete
  23. AnonymousJuly 03, 2011

    Huyu Professor Mbele ni utani mtupu. Sasa anajifanya kuwa ujamaa hajakufaa duniani kote walipoujaribu?! Nenda kawaulize Warusi na jamaa zao. China ujamaa uliobakia ni wa chama cha kikomunisti tu kwa jina lakini mfumo mzima wa uzalishaji na uchumi ni wa kibepari.

    Sasa wewe kweli ni Professor wa majungu. Sasa unataka kulete ubishi wa kijinga tu. Kama Nyerere alikiri au hakukiri si muhimu cha muhimu ni kuwa ujamaa wa Nyerere umeizamisha Tanzania katika umasiki na ulikuwa janga kwa nchi.

    ReplyDelete
  24. AnonymousJuly 03, 2011

    ankal na wasomaji wenzangu.

    1. Kwanza nampongeza Profesa kwa juhudi za za kutaka kuuweka ukweli hadharani. Hakika hilo ni jambo jema. Aidha, ningependa wachangia hoja katika hili wapende kuweka maoni yatakayotuelimisha, na sio maneno ya mkato mkato.

    2. Mimi siwezi kukubali au kukataa kama Mwalimu alisema ujamaa umeshindwa. Ingawa nimesikia hayo kwenye vyombo vya habari mfano 'Julius Nyerere, the elder statesman of post-colonial Africa, dies, aged 77' Indipendent Newspaper 15th October 1999. Maelezo hayo yako hata kwenye You Tube, ingawa sio kutoka kinywa cha Mwalimu; lakini imeripotiwa kuwa Mwalimu alikiri Kushindwa kwa mfumo wa Ujamaa na kujitegemea.

    3. Wakati wa 'Operation Vijiji', itakumbukwa kuwa watu walihamishwa maeneo ya mijini kupelekwa kwenye 'vijiji vya ujamaa'. Mafanikio ya vijiji vya ujamaa kwa kweli na msingi ni kwamba hayakuwepo. Wengine waliuwawa na wanyama pori kwa kuhamishiwa katika 'vijiji' vilivyopangwa katika maeneo ya hatari.

    4. MSINGI WA UJAMAA WA TANZANIA UNATOKANA NA AZIMIO LA ARUSHA. Mali za 'mabepari' zilitaifishwa na mihimili yote ya uchumi ikapewa serikali. Tukaingia kwenye ushirikiano wa Afrika Mashariki na kupata hasara kubwa 1977. Cha msingi ni kwamba katika hio mihimili ya uchumi,Serikali iliyoongozwa na Azimio la Arusha haikufanikiwa katika kuwaondolea watanzania maadui watatu (Umaskini, Ujinga na elimu)kama alivyolenga mwalimu.

    5. ikumbukwe kwamba tumepewa misaada ya udugu katika ujamaa na jamhuri ya china ikiwemo TAZARA na Mradi wa Mpunga Rujewa, Mbarali ambao una kinu cha kuzalishia umeme na ni shamba la kipekee. misaada hiyo ilikuwa na ufanisi ilipokuwa inasimamiwa na wachina, Serikali ilipokabidhiwa; ilidorora! Ujamaa na Azimio la Arusha kinadharia ni muafakamzuri wa usawa na kutafuta maendeleo. Leo tunalalamikia mgao wa umeme, kama mdau aliyechangia anaesema anaitamani $100 anunulie mishumaa. Wakati wa kilele cha ujamaa na azimio la Arusha ilikuwa kuna mgao wa chakula --- DONA. Watu walikuwa wanaoga kwa harita na wanakunywa uji wa chumvi. Sasa kama hayo ndio mafanikio ya Ujamaa na Azimio la Arusha tuambizane.

    6. Jambo la busara alilolifanya Julius Nyerere ni kung'atuka 1985, ingawa kwa kuwa alikuwa bado anapenda madaraka; akaendelea kuwa mwenyekiti wa CCM mpaka 1992. Aling'atuka kwa kuwa alishaamini kuwa hana tena mchango wa kuinasua nchi katika mgogoro wa uchumi aliokuwa ameshaiingiza kwa miaka 18 mfululizo tangu alipotangazia taifa azimio la arusha. Ali Hassan Mwinyi, licha ya kubughudhiwa katika utawala wake (Kwa sababu Mwenyekiti wa Chama aliendelea kuwa Mwalimu); alifanikiwa kuleta mageuzi ya Uchumi, kufungulia vyombo vya habari na vyama vingi. Watanzania leo wanapayuka watakavyo, hii imetokana na 'liberal' policies za Mzee Mwinyi. La msingi kabisa, ni baada ya Mwalimu tu kuachia uenyekiti na Azimio la Zanzibar likapitishwa.

    7.Mwalimu alifanikiwa sana katika uongozi wake, lakini Sera ya Ujamaa na Azimio la Arusha vilishindwa. La kustaajabisha Sasa Tanzania sijui tujiite mabepari au? maana sielewielewi.

    8. samahani kwa mchango mrefu, naamini hapa nitazua mjadala.

    ReplyDelete
  25. AnonymousJuly 03, 2011

    Umewatuhumu watu kusema majungu lakini article yako imetaja 'jungu' sio 'majungu'. Ninavyosikia wewe ni professor wa Kiswahili correct me if I am wrong, singular na plural la neno majungu. Kwa wewe kutumia majungu nilitegemea list ya majungu sio moja kama ulivyosema.

    Zaidi, Nyerere kukiri au kuto kukiri ni diversion tactics ya ukweli kama siasa sake zilikuwa successful au la. Majaji wa hilo sio yeye Nyerere bali ni wananchi. Mfano wa court scenario, mshitakiwa anaweza kusema yeye hajafanya kosa, kwa hiyo haiminishi kauli yake ndio itakayofatwa kwasababu amekiri kutofanya kosa.

    Professor based on maandishi yako I conclude that you are mbumbumbu.

    ReplyDelete
  26. AnonymousJuly 03, 2011

    Ninatangulia kusema kuwa kwanza Nyerere alikuwa ni binadamu mwenye hulka na mambo yoote ya kibinadamu ukiwemo udhaifu. Hivyo pamoja na nia yake njema kwa taifa hili bado alikuwa ni binadamu wa kawaida na kwa kweli ujamaa kama sera haukufanikiwa kwa 100% Labda tuziangalia hizi % na kulinganisha malengo na tuzipe kiwango cha ufaulu halafu tuhitimishe kwamba kwa kuwa kiwango chetu cha ufaulu ni labda 55% basi ulifeli au la ila kama mwenyewe alikwishakiri kufeli kwa hakika umefeli lakini kufeli haimaanishi kwamba ulikuwa mbaya.

    Katika jambo linalonikera kuhusu Nyerere ni watu kumtukuza na kuwatukana wale walioshiriana nae kwa karibu. Kwa mfano kuna kejeli nyingi sana kuhusu Mzee R M Kawawa na kama ni majungu yanayomuhusu mzee huyu pengine ni mengi kuliko ya Nyerere mwenyewe. Kusema Nyerere alikuwa safi na kuwaponda hadharani waliomsaidia kufikisha nchi pale ilipofika ni dosari kwa Nyerere mwenyewe.

    ReplyDelete
  27. AnonymousJuly 03, 2011

    Ujamaa umeweka msingi ambao wengi wetu ndipo tulipojengea maisha yetu. Wengine tusingeweza kupenya kwenye mifumo ya kibepari.

    Kuna Anony mmoja amesema maendeleo hayapimwi kwa uchumi tu, kuna mambo mengine ambayo Ujamaa ulifanikiwa. Na hata hivyo ujamaa ungeweza kufanikisha uchumi kama watu waliopewa madaraka wasingeiba na kuuwa misingi ya uchumi iliyowekwa.

    Sasa kinyume cha ujamaa ni ubepari. Haya mmefunguliwa milango. Mbona mnawalalmikia viongozi wakifisadi nchi? Si mnautaka ubepari, kaeni kimya mnyolewe. Mwenye ubavu atashindana nao asiyekuwa nao mtakuja endeleeni kulalamika.

    ReplyDelete
  28. Ankal, sijapenda kauli iliyotolewa na anyonymous contributor anayetuita sisi wa 'Malavidavi' na 'Makamuzi'; yaani sisi wana globu ya jamii ni watu wa malavidavi na makamuzi. waambiwe wachangia mada watoe mada na sio lugha za kuchefua

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...