Baadhi ya wananfunzi wa shule za sekondari waliofanya vizuri katika mtihani wa kidato cha sita wakiingia kwenye ukumbi wa Bunge Mjini Dodoma kukabidhiwa vyeti na kutambulishwa kwa wabunge leo.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwa wananfunzi wa shule za sekondari waliofanya vizuri katika mtihani wa kidato cha sita baada ya kuwakabidhi vyeti na kuwatambulisha kwa wabunge mjini Dodoma leo.Kulia kwake ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Capt, George Mkuchika na Kushoto kwake Waziri wa Elimu, Utamaduni na Mafunzo ya Ufundi, Dr. Shukuru Kawambwa.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB.), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA HAFLA YA KUWAPONGEZA WANAFUNZI WALIOFANYA VIZURI KATIKA MTIHANI WA KUMALIZA KIDATO CHA SITA MWAKA 2011 ITAKAYOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA BUNGE – DODOMA TAREHE 1 JUNI 2011

Mheshimiwa Spika;
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri;
Waheshimiwa Wabunge;
Wageni Waalikwa; na
Mabibi na Mabwana.

Awali ya yote napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Waandaaji  wa Hafla hii kwa kunipa fursa ya kuzungumza katika tukio hili la kuwapongeza Wanafunzi waliofanya vizuri katika Mtihani wa kumaliza Kidato cha Sita mwaka 2011. Naomba nikushukuru Mheshimiwa Spika pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwa
kukubali Vijana wetu 20 kuingia ndani ya Ukumbi huu wa Bunge ili wapongezwe
na wakati tukio hilo likifanyika, washuhudiwe na Waheshimiwa Wabunge pamoja
na Wananchi Nchini kote.

Mheshimiwa Spika,
Katika matokeo ya mtihani wa Kidato cha Sita uliofanyika Nchi nzima Mwezi Februari 2011, mambo ya kutia moyo ni kuwa Wanafunzi walifanya vizuri katika Masomo ya Sayansi ikilinganishwa na miaka ya nyuma hasa mwaka 2010. Masomo hayo ni Advanced Mathematics, Physics, Chemistry na Basic Mathematics”.
Hii ni hatua nzuri katika maendeleo ya Sayansi hapa Nchini ikizingatiwa kuwa Masomo ya Sayansi yamekuwa na ufaulu usioridhisha kwa muda mrefu. Napenda kutoa pongezi kwa Wadau wote waliohusika katika kuleta mafanikio haya.

Mheshimiwa Spika,
Baada ya kuona matokeo na hasa viwango vya ufaulu, Serikali kwa kushirikiana na Bunge tuliona ni vyema kuonyesha kuridhishwa kwetu na juhudi za Wanafunzi hawa. Tuliona ni vema kuwepo na jambo litakaloonyesha kuridhishwa kwetu na mafanikio yao na kuamsha ari na ushindani kwa Wanafunzi ambao bado wako Mashuleni ili nao waweze kuyafikia mafanikio haya na ikiwezekana kufanya vizuri zaidi. Tukaamua Waje Bungeni ili tuwapongeze mbele ya Waheshimiwa Wabunge na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika,
Wanafunzi tuliowaalika ni 20. Majina yao ni kama ifuatavyo:

1. Muhagachi P. Chacha - Kibaha, Pwani
2. Samwel Katwale - Mzumbe, Morogoro
3. Amir Abdallah - Feza Boys, Dar es Salaam
4. Aron Gerson - Tabora Boys, Tabora
5. Shaban Omary - Tabora Boys, Tabora
6. Kudra H. Baruti - Feza Boys, Dar es Salaam
7. George V. Assenga - Majengo, Kilimanjaro
8. Comman Nduru - Feza Boys, Dar es Salaam
9. Francis Joseph - Tabora Boys, Tabora
10. George M. Felix - Mzumbe, Morogoro
11. Doreen Kabuche - Benjamin W. Mkapa, Dar es Salaam
12. Rahabu Mwang’amba - Kilakala, Morogoro
13. Mary C. Moshi - Kifungilo Girls, Tanga
14. Nuru N. Kipato - Marian Girls, Pwani
15. Zainabu Hassan - Al-Muntazir Islamic, Dar es Salaam
16. Catherine E. Temu - Ashira Girls, Kilimanjaro
17. Anthonia J. Lugomo - Usongwe, Mbeya
18. Cecilia A. Mviile - Kifungilo Girls, Tanga
19. Mariam Matovolwa - Kilakala, Morogoro
20. Suzan J. Makoi - Tarakea, Kilimanjaro

Mheshimiwa Spika,
Mtaona kuwa tumealika Wasichana 10 waliofanya vizuri miongoni mwa Wasichana
wote waliofanya mtihani huo wa Kidato cha Sita mwaka 2011. Uchambuzi
unaonyesha kuwa, Wasichana hao walifaulu kutoka Shule za Sekondari za
Benjamin W. Mkapa (1), Kilakala (2), Kifungilo Girls (2), Marian Girls (1),
Al-Muntazir Islamic (1), Ashira Girls (1), Usongwe (1), na Tarakea (1).

Aidha, tumealika Wavulana 10 waliofanya vizuri kuliko Wavulana wote
waliofanya mtihani huo. Wavulana hao wamefaulu kutoka Shule za Kibaha (1),
Mzumbe (2), Feza Boys (3), Tabora Boys (3) na Majengo (1).

Hapa tunachokiona ni kwamba, Shule za Tabora Boys na Feza Boys ndizo zenye
idadi kubwa ya Wanafunzi kati ya 20 walioongoza katika mtihani wa Kidato cha
Sita mwaka huu. Shule hizi mbili zinastahili pongezi nyingi.

Mheshimiwa Spika,
Jambo la kutia moyo kwenye matokeo haya ni kuwa, miongoni mwa Wanafunzi hawa
20, Wanafunzi 7 walijiunga na Kidato cha Tano baada ya kumaliza Kidato cha
Nne katika Shule za Kata. Wanafunzi hao ni Samweli Katwale kutoka Sekondari
ya Bukwande (Magu), Francis Josephat kutoka Sekondari ya Inchugu (Tarime),
Rahabu Mwang’amba kutoka Sekondari ya Vwawa (Mbeya), Zainabu Hassan kutoka
Sekondari ya Uhuru (Shinyanga), Mariam Matovolwa kutoka Sekondari ya Kikuyu
(Dodoma), Suzana J. Makoi kutoka Sekondari ya Tarakea (Rombo) na Anthonia J.
Lugomo kutoka Sekondari ya Usongwe (Mbozi).

Kati ya Wanafunzi hao saba, watano ni Wasichana na wawili ni Wavulana.

Napenda niwapongeze Wanafunzi hawa 7 kwa kuwa wamethibitisha kuwa uamuzi wa
Serikali wa kujenga Shule za Kata ulikuwa na utabaki kuwa uamuzi sahihi.
Kama Shule hizi zisingekuwepo huenda Vijana hawa wasingeweza kuonesha uwezo
wao kitaaluma kama walivyofanya hususan Wasichana. Wanafunzi hao pia,
wameonesha kuwa Shule hizi zikiwezeshwa zaidi zitafanya vizuri zaidi kuliko
Shule nyingine. Kwa mara nyingine, niwaombe Viongozi na Wananchi ambao
hubeza Shule hizi, wakubali kiungwana kuwa, ni heri kuwa na Shule hizo
kuliko kutokuwa nazo kabisa. Jukumu letu ni kuendelea kuziboresha Shule hizo
na kuwatia moyo Walimu na Wanafunzi wao ili waendelee kufundisha na
kujifunza kwa bidii.

Mheshimiwa Spika,
Wanafunzi hawa hawakufikia mafanikio haya bila malezi na msaada kutoka kwa
Wazazi na Walimu wao. Tumealika Mzazi mmoja mmoja kwa kila Mwanafunzi ili
ashuhudie Mwanae anavyopongezwa siku ya leo. Nawaomba Wazazi hawa na wale
waliobaki nyumbani wapokee pongezi zangu kwa malezi na miongozo yao kwa
Wanafunzi hawa iliyochangia mafanikio yao.

Mheshimiwa Spika,
Serikali inatambua na inathamini kazi zinazofanywa na Walimu Nchini. Ni kwa
mtizamo huo tumewaalika Walimu waliowafundisha Wanafunzi hawa. Bila shaka,
kufaulu kwa Wanafunzi kumechangiwa na juhudi za Walimu wao. Nao tumetaka
washuhudie matokeo ya kazi zao siku ya leo. Vilevile, hii itakuwa ni fursa
ya  kutoa ujumbe kwa Walimu wengine kuongeza bidii katika kuwawezesha
Wanafunzi wao kufikia malengo yao. Nawaomba Walimu waliochangia mafanikio ya
Wanafunzi hawa wapokee shukurani zangu binafsi pamoja na Serikali kwa kazi
kubwa na yenye heshima waliyofanya.

Kwa pamoja nawapongeza Wazazi na Walimu wote kwa kutimiza wajibu wenu
vizuri. Wajibu wa kuwalea watoto hawa katika maadili mema na kuwaongoza
kwenye njia nzuri zilizowawezesha kukaribishwa hapa Bungeni.

Mheshimiwa Spika,

Pamoja na kuwaalika Wanafunzi hawa pamoja na Walimu na Wazazi wao Bungeni,
tumeona tusiishie hapo. Tumepanga kutoa zawadi kwa Wanafunzi Bora 20, Walimu
wao na Shule zao ikiwa ni ishara ya kuthamini kazi kubwa iliyofanywa. Zawadi
hizo ni kama ifuatavyo:

  - Kompyuta ndogo (Lap Top) na Shilingi 150,000 pamoja na Cheti cha Ubora
  kwa kila Mwanafunzi aliyealikwa;
  - Shilingi 500,000 pamoja na Cheti kwa Walimu 31 wa A-level
  waliowafundisha Wanafunzi hao;
  - Shilingi 1,000,000 pamoja na Cheti kwa kila Shule walikosoma Wanafunzi
  hao;
  - Meza ya Maabara yenye thamani ya Shilingi 5,000,000 pamoja na Cheti kwa
  kila Shule ya Kata ambako walisoma Wanafunzi 7 kati ya 20 waliofanya vizuri
  Kidato cha Sita.

Zawadi zitakazotolewa hapa Bungeni ni zile za Wanafunzi 20 tu. Zawadi
nyingine zitatolewa kwenye hafla itakayofanyika leo jioni.

Mheshimiwa Spika,
Nina imani kuwa utaratibu huu wa kutambua na kutoa motisha kwa Wanafunzi
bora utaongeza ari ya Wanafunzi na Walimu kujifunza na kufundisha kwa bidii
na hivyo kuinua kiwango cha Ubora wa Elimu Nchini. Ni vema ukawepo utaratibu
bora na endelevu wa utoaji wa motisha kwa Wanafunzi na Walimu wao. Natarajia
Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi watafanyia kazi suala hili.

Napenda kuwaasa Vijana wetu kuwa baada ya kumaliza Elimu ya Sekondari
watajiunga na Vyuo vya Elimu ya Juu. Huko kuna uhuru zaidi ya mlivyozoea.
Uhuru huo sio tatizo, bali tatizo ni jinsi unavyotumia uhuru huo. Nawashauri
msijiingize kwenye Migomo isiyo na tija na Maandamano kinyume na Sheria.

Mheshimiwa Spika,
Nimalizie kwa kuwashukuru Wanafunzi, Walimu na Wazazi, kwa kukubali mwaliko
wetu. Niwaombe Wanafunzi waongeze  bidii kwenye masomo yao. Aidha, wadumishe
nidhamu kwa Walimu na Wazazi ili waweze kupata mafanikio zaidi. Nawashukuru
pia Walimu kwa juhudi zao na niwaombe waongeze bidii katika kazi zao ili
yapatikane mafanikio makubwa zaidi hasa katika Masomo ya Sayansi.
Nawashukuru Wazazi kwa malezi yao na kuwaomba kuendelea kuwaongoza Vijana
wao kwenye maadili mema.

Mwisho, nawatakiwa wote hafla njema jioni, safari njema kurudi nyumbani na
maisha mema kwa ujumla.

Baada ya kuyasema hayo, naomba mniruhusu niwape zawadi Wanafunzi 20
waliofanya vizuri katika mtihani wa Kidato cha Sita mwaka 2011.

*Nashukuru kwa kunisikiliza.*


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Kibaya ni pale wanapoangalia aliyefanya vizuri kwa kupata As ama Division one. Wanasahau kuwa kunawengine wanadivision three lakini wamefaulu kuzidi huyo wa division one ukizingatia mazingira mabaya ya kusoma (Teaching and learning environment) waliyopitia. Dhambi hii ni kubwa na inawafanya watanzania wengi waonekana hawana akili kumbe mazingira mabaya ya kusomea yamewafanya wawe hivyo. Hapa nimekumbuka msemo wa kiingereza nilowahi kuusikia kuwa "I was born intelligent but education ruined me" tafsri isiyorasmi ni "Nilizaliwa na akili lakini mfumo wa elimu ndo uloniharibu". Mambo yaleyale ndo yalimfanya hata Rais wa nchi awatangazie watanzania kuwa mikopo itatolewa kwa wanafunzi watakao pata daraja la kwanza na la pili tu. Nilishangaa kuona kuwa Rais amesahau kuwa wengine wanasoma katika mazingira ambayo kupata daraja la kwanza ama la pili ni ndoto kwao na haina maaana kuwa hawana akili 'natural intelligence'. kazi kweli kweli.

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 01, 2011

    wanatokea shule gani na majina yao mbona hawajulikani

    ReplyDelete
  3. AnonymousJuly 02, 2011

    mafataki msiwamezee mate watoto wa watu

    ReplyDelete
  4. AnonymousJuly 02, 2011

    Napenda kumpokeza sana Muhagachi Peter Chacha kwa kazi nzuri aliyoifanya. Huyu kijana anastahili pongezi kutokana na kuelewa ugumu wa maisha katika familia yake na kujua anatakiwa kufanya nini ili kuinua familia yake. Huyu kijana sio kwamba ni juhudi za walimu pale alipomalizia High School ni kutokana na juhudi za wazake wake wawili. Wanaenda shambani wakirudi wanakaa chini kufundisha watoto wao hesabu, kusoma na kuandika pale Chamoto/Banana-Ukonga. Mdogo wangu Muhagachi kuendelee kufanya hivyo hadi PhD yako. Nakukaribisha sana Havard University or Duke University. Naomba serikali ya Tanzania imsaidie huyu Kijana familia yake haina kabisa uwezo wa kumsaidia kijana wao, inahitaji msaada wenu wa hali na mali. Mkisaidia huyu kijana naye atawasidia wengine. Nawashukuru sana watakaojitolea kumsaidia.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...