Na Salama Njani - Habari Maelezo Zanzibar
Imeelezwa kuwa Zanzibar kama zilivyo nchi nyengine zinazoendelea duniani, inakabiliwa na changamoto mbali mbali katika juhudi za kutafuta mapato, na kukabiliana na mahitaji ya Bajeti ya mapato na matumizi kwa mwaka.
Akitoa mada kwa wanafunzi wa vyuo mbali mbali vya Zanzibar katika ukumbi wa American corner , Afisa Bajeti kutoka wizara ya nchi afisi ya Rais,fedha ,uchumi na mipango ya maendeleo bi Maryam Mohammed Othman amesema, kutokana na changamoto hizo Zanzibar inachukua hatua zaidi ili kukuza vyanzo vyake vya mapato na kuongeza pato la uchumi.
Akizitaja changamoto zinazoikabili Zanzibar katika kutafuta mapato amesema, ni pamoja na ukosefu wa utumiaji mzuri wa rasilimali zilizopo utakao hakikisha ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini pamoja na uimarishaji wa huduma za kijamii .
Nyengine ni vyanzo vidogo vya kodi, kasi ya ukuaji wa utalii usiolingana na kasi ya ukuaji wa mapato yatokanayo na utalii, ikilinganishwa na nchi nyengine ambapo utalii unakua na kasi ya mapato inaongezeka.
Mahitaji makubwa ya rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji MKUZA 2 kwa kuzingatia mahitaji ya MKUZA (1),kiwango kidogao cha fedha za ndani kwa matumizi ya miradi ya maendeleo, kiwango kikubwa cha utegemezi wa wahisani pamoja na shinikizo la ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Amesema kwa upande wa kutegema wahisani inaonekana kuwa miradi ya maendeleo kama ujenzi wa barabara, maji nk serikali inategemea sana wahisani kwa asilimia 60% au zaidi na kilichobaki ndio mchango wa serikali.
Amesema wakati wakati wa uandaaji wa Bajeti mambo muhimu kama mfumko wa bei na kupanda na kushuka kwa soko la fedha duniani huangaliwa kwa makini kabla ya kuanza kwa mwaka mpya wa Bajeti kwa lengo la kufikia mapato na matumizi ya Bajeti.
Aidha sekta mbali mbali za maendeleo kama afya, maji, elimu nk ziwe zinaenda sambamba na dira ya maendeleo katika kufanikisha mchakato wa bajeti
Nao washiriki wa mafunzo hayo walitaka kujua mambo mbali mbali katika uandaaji wa bajeti ikiwa ni pamoja na ushirikishwaji wa wananchi wa chini, mgao wa %4.5 kwa Zanzibar kutoka Tanzania bara, umuhimu wa kufufua viwanda vilivyokufa na tatizo la mfumko wa bei.
Akitolea ufafanuzi wa masuala hayo bi Maryam amesema Zanzibar bado haijafikia malengo ya maendeleo kutokana na kushindwa kufufua viwanda vilivyopo ili kukuza mapato kama ilivyo katika nchi nyingi ambapo maendeleo huja kutokana na viwanda na sio kilimo pekee.
Akizitaja sababu za kufa kwa viwanda amesema ni miongoni mwa kero za muungano kutokana na suala zima la kodi ambazo kwa sasa serikali zote mbili zinaendelea na mazungumzo ili kupata ufumbuzi .
Amesema kutokana na kuwa vyanzo vya mapato ni kidogo, kwa sasa serikali inalenga nguvu zake katika uwekezaji wa viwanda na utalii ili kuongeza mapato badala ya mfumo wa awali wa kutegemea kilimo pekee.
Suala la mgao wa %4.5 kwa Zanzibar kutoka Tanzania bara amesema, kwa sasa suala hilo lipo katika mazungumzo kwa kuona mgao huo ni mdogo sana ikilinganishwa na Tanzania bara kuwa na % 95.5 zanzibar iliomba kupatiwa %11 ya mgao ila kwa sasa inatajwa kuwa ni %6 ingawa bado haijathibitishwa.
Akizungumzia suala la utalii Maryam amesema,watalii wanaoingia ndani ya nchi ni wengi lakini mapato ni madogo hivyo ni lazima kuzingatia ukusanyaji mzuri wa mapato pamoja na usajili halali wa watalii wanapoingia nchini.
Hata hivyo watalii wanaangalia huduma muhimu ndani ya nchi, ikiwemo miundo mbinu ya Nyanja mbali mbali kama barabara, maji, umeme nk kutokana na hili serikali inaelekeza nguvu zake nyingi katika kuimarisha miundo mbinu, ili kukuza kasi ya mapato yatokanayo na utalii.
Aidha washiriki walishauri suala la bajeti kuingizwa katika mitaala ya shule ilikutoa uelewa mzuri kama ilivyo madhumuni yamafunzo hayo ni kueneza uelewa wa bajeti ya serikali ya Zanzibar pamoja na changamoto za uandaaji wa bajeti.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...