Na Thomas Ludovick
MOJA ya changamoto kubwa inayoikabili Sekta ya Afya katika maeneo mengi nchini hususan vijijini kwa sasa ni upungufu mkubwa wa watoa huduma wa afya pamoja na uchache wa vifaa vya tiba, hivyo kupelekea wananchi kutopata huduma bora za afya.
Sababu kubwa inayopelekea wahudumu wa afya kukwepa kufanya kazi vijijini ni pamoja na ukosekanaji wa vitendea kazi vya kutolea huduma, ukosefu wa huduma muhimu za kijamii katika maeneo ya vijijini, miundombinu duni na waudumu wa afya kutopata fursa ya kujiendeleza kitaaluma.
Pia inatubidi kufahamu kuwa zaidi ya asilimia 70 ya watu nchini Tanzania wanaishi katika maeneo ya vijijini ambapo ndipo kwenye kiungo muhimu katika kuinua uchumi wa taifa letu. Kama watu hawa watakuwa hawapati huduma bora za afya ni wazi kwamba matokeo yake watapoteza maisha na vilevile taifa litakuwa limepungukiwa na nguvu kazi katika jamii na hivyo kupelekea uchumi wa nchi pia kushuka.
Kutokana na suala hili, hivi karibuni shirika lisilo la kiserikali la Sikika lilitembelea Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, na kugundua kuwa Wilaya hiyo ina upungufu wa asilimia 62 ya watoa huduma wa afya. Hivyo kusababisha wananchi waishio vijijini kuendelea kukosa huduma bora za afya. Kutokana na upungufu huo umesababisha watoa huduma wachache waliopo kufanya kazi zaidi ya saa 8 kwa siku kinyume cha sheria za kazi.
Mbali na wafanyakazi wachache wa afya waliopo kufanya kazi zaidi ya muda unaoruhusiwa kisheria, hupelekea wagonjwa kupata kero ya kukaa foleni ndefu wakisubiri huduma. Maeneo mengine wauguzi hulazimika kufanya kazi zisizokuwa za taaluma zao.
Katika ziara hiyo, Sikika pia waligundua kuwa katika kituo cha afya kinachojulikana kwa jina la Busi, kilichopo umbali wa kilomita 70 kutoka wilayani Kondoa, kina Afisa Tabibu mmoja. Hii ni sawa na kituo cha Makorongo ambacho kina Wauguzi wawili na Afisa Tabibu mmoja huku kukiwa wanahitaji wahudumu 15. Pia katika vituo vya afya Busi na Hamai suala la usafi hufanywa na wauguzi wenyewe ambao huenda mapema katika vituo vyao kufanya usafi na baadae kurudi nyumbani kwa ajili ya kujiandaa kwa kazi ya kuwahudumia wagojwa.
Aidha, katika ziara hiyo Sikika walibaini kuwa Zahanati ya Chase katika kata ya Makorongo ilikuwa imefungwa kabisa kwa takribani wiki mbili kutokana na Mganga Mfawidhi mmoja kufariki dunia na kusababisha wananchi kutopata huduma. Hali kadhalika vituo viwili vya afya (Khubunko na Maziwa) vimefungwa kwa kukosa watumishi wa afya. Hali hii inapelekea wakazi wa maeneo husika kutopata huduma za afya kabisa.
Afya bora ni haki ya msingi ya binaadamu. Pia wananchi wakiwa na afya bora hushiriki kikamilifu katika kuinua uchumi binafsi na wa nchi. Jamii yenye wananchi dhaifu uchumi wake pia huwa dhaifu na maendeleo ya kipato duni. Mbaya zaidi, ukosefu wa huduma bora huweza kupelekea vifo hivyo kuvunja haki ya msingi ya kuishi.
Katika Bajeti ya mwaka wa fedha wa 2011/2012 Sekta ya Afya imepangiwa bajeti ya Sh. billioni 1,209.1 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 0.3 ikilinganishwa na sh. bilioni 1,205.9 mwaka 2010/2011, japokuwa bajeti imeongezeka kwa asilimia hiyo lakini bado huduma za afya zinazidi kuwa duni.
Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ichukua hatua za haraka kukabiliana na uhaba mkubwa wa wafanyakazi wa afya katika maeneo ya vijijini na hasa wilaya ya Kondoa.
Hata hivyo, naipongeza Serikali kwani kupitia mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM), imepanga kujenga zahanati katika kila Kijiji na kituo cha afya katika kila Kata ili kupunguza umbali wa upatikanaji wa huduma ya afya. Hadi sasa ni miaka minne ya utekelezaji wa mpango huu ikiwa imeshapita lakini bado kuna changamoto kubwa ya uwepo wa majengo mapya yasiyo na watoa huduma.
Lakini ni vizuri kufahamu kuwa watoa huduma wa afya ni watu muhimu sana mahali popote pale duniani. Kama kutatokea upungufu wa wataalam hawa sehemu husika, basi ile sera ya kutoa huduma bora za afya kwa kila mwananchi itabaki kuwa nadharia tu.
Hivyo, naamini kuwa ufumbuzi wa tatizo hili upo ndani ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Ili kukabiliana na tatizo hili serikali inabidi ichukue hatua za haraka zaidi kupeleka watumishi na vifaa vya tiba vya kutosha katika maeneo ya vijijini ili kutimiza adhma yake ya kutoa huduma bora. Hata hivyo Kondoa ni moja kati ya sehemu inayotoa picha halisi ya utoaji wa huduma za afya katika maeneo mengi ya vijijini nchini Tanzania, japokuwa kuna maeneo mengi zaidi yanayokabiliwa na matatizo hayo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...