Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi leo jioni wameuaga mwili wa marehemu Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mussa Khamis Silima (pichani) baada ya kufikishwa katika ukumbi wa Baraza hilo Visiwani Zanzibar.

Kwa mujibu wa kanuni za Baraza la Wawakilishi kuanzia sasa Mjumbe yoyote atakayefariki atalazimika kufikishwa katika Baraza hilo kwa kuombewa dua na jeneza kufunikwa Bendera ya Baraza la Wawakilishi.

Mwili wa marehemu uliwasili uwanja wa ndege wa zamani saa 11:30 jioni kwa ndege ya kukodi ya Shirika la TANZAIR ambapo katika uwanja huo viongozi mbalimbali wa Serikali walikuwepo pamoja na wananchi.

Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho alishughulikia taratibu za kuusafisha mwili wa marehemu kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dar es Salaam.

Mbunge wa viti Maalum(CCM), Maua Abeid Daftari alikuwa miongoni mwa viongozi walioleta mwili wa marehemu Visiwani hapa.

Katika taarifa ya Serikali ya Mapinnduzi Zanzibar  kwa vyombo vya habari iliyotolewa jioni hii na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed ilisema marehemu anatarajiwa kuzikwa kesho Kijijini kwao Kiboje Wilaya ya Kati  Mkoa wa Kusini Unguja.

Katika taarifa hiyo, Waziri Aboud  alimtaja marehemu Mussa kuwa ni miongoni mwa watu waliotoa mchango katika shughuli za kisiasa pamoja na utumishi wa muda mrefu Serikalini akiwa mwalimu ambaye amechangia maendeleo ya vijana wengi Visiwani Zanzibar.

Kabla ya kifo chake, marehemu Silima alipata ajali ya gari ambapo katika ajali hiyo, mke wa marehemu alifariki papo hapo na hali ya dereva wake bado anaendelea kutibiwa hospitalini.

Mwakilishi huyo aliumia ya sehemu ya miguu pamoja na kiuno kutokana na ajali iliyotokea eneo la Nzuguni Dodoma juzi na kulazimika kupelekwa Hospitali ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Viongozi mbalimbali wa Serikali wanatarajiwa kuhudhuria katika mazishi hayo.

23/08/2011
IMETOLEWA NA:
IDARA YA HABARI(MAELEZO) ZANZIBAR

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. MWENYEZI MUNGU AMLAZE MAHALA PEMA PEPONI AMIN, NA AKUSAMEHE MAKOSA YAKO NA AKUPE WEPESI ISHALLAH

    ReplyDelete
  2. Inna lillahi wainna ilayhi Rajiun-Mwenyeenzi Mungu awalaze mahali pema peponi,Ameen

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...