Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA Mama Salma Kikwete akipokea hundi ya shilingi milioni tano (5m/-) kutoka kwa Mkurugenzi wa Masoko wa Benki Bank ya CRDB Bi  Tully Mwambapa (kulia)kwa ajili ya kuchangia tamasha la wajasiriamali wanawake (MOWE) 2011 usiku wa kuamkia leo jijini Dar es Salaam, Zaidi ya shiligi 55 milioni zimechangwa.(55,368,500/-)
 Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani nchini Alexio Musindo akizungumza katika hafla  ya uzinduzi wa uchangishaji wa fedha kwaajili ya Tamasha la wajasiriamali (MOWE) yaani Month of Women Enterprenuers
 Mwenyekiti wa Taasisi wa WAMA pia Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiongea na Wajasiriamali wakati wa hafla ya uzinduzi wa uchangishaji wa fedha kwaajili ya Tamasha la Wajasiriamali (MOWE) 2011 litalofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo mwaka huu Taasisi ya WAMA ndio mratibu wa Tamasha hilo.Jumla ya zaidi milioni 55 zimechangwa katika hafla hiyo na kauli mbiu ya mwka huu ya MOWE ( MIAKA 50 WANAWAKE WAJASIRIAMALI TUNAWEZA-TUTUMIE FURSA),(kulia ni Mwenyekiti wa MOWE Tanzania Elihaika Mrema,na (kushoto) ni Mwakilishi wa Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Consolata
 Baadhi ya Wanawake wajasiriamali wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA Mama Slama Kikwete (Aug 26,2011) katika hafla ya  uzinduzi wa uchangishaji wa fedha kwaajili ya Tamasha la wajasiriamali (MOWE) jijini Dar es Salaam
Michango ikiendelea. Picha zote na Mwanakombo Jumaa-MAELEZO


Na Anna Nkinda – Maelezo
Wadau wa maendeleo hapa nchini wametakiwa kuwasaidia wanawake wajasiriamali kwa kuwapa fursa zilizopo ndani ya uwezo wao kwani wanawake hao huzalisha bidhaa za asili ya kitanzania ambazo hutumika ndani na nje ya nchi na kwa kufanya hivyo huchangia kuongeza fursa za ajira na kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa juzi na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akizindua uchangishaji wa fedha kwa ajili ya kufanikisha maadhimisho ya Tamasha la Wanawake Wajasiriamali Tanzania kwa mwaka 2011 lijulikanalo kama Mwezi wa Wanawake Wajasiriamali (Month of Women Entrepreneurs – MOWE)  katika Hoteli ya New Afrika  jijini Dar es Salaam.
Zaidi ya shilingi milioni 55 pamoja na vifaa mbalimbali zilichangwa na wadau hao kwa ajili ya kufanikisha tamasha hilo ambalo linatarajia kufanyika tarehe 30/10/2011 – 4/11/2011 katika viwanja wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema  kuwa kumuwezesha mwanamke kunasaidia jamii na taifa kupunguza umaskini wa kipato cha watu hivyo inachangia utekelezaji wa lengo la kwanza katika  malengo ya millennia linalohusu kupunguza umaskini kwa nusu ifikapo mwaka 2015.
“Mimi binafsi nimeshiriki mara kadhaa katia shughuli za kuendeleza ujasiriamali kwa wanawake na nimejionea jinsi wanawake wakiwemo wenye ulemavu na waishio na Virusi Vya Ukimwi (VVU) wanavyotambua umuhimu wa kuongeza kasi katika juhudi za kuleta maendeleo kwao na kwa kila Mtanzania. Napenda kuwahakikishia kuwa jukwaa la MOWE ni mfano bora sana wa kuendeleza wanawake wajasiriamali”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa WAMA pia aliwataka viongozi wa makampuni waliohudhuria katika hafla hiyo kupanga utaratibu wa kudumu wa kuchangia tamasha hilo ambalo Shirika la Kazi Duniani (ILO) limekuwa likisimamia kwa muda mrefu ili ILO itakapomaliza muda wake wa kusimamia tamasha hilo liendelee kufanyika.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa ILO nchini Alexio Musindo alisema kuwa wameshafadhili matamasha manne kama hayo na wataendelea kufadhili mengine kwani ukimuunga mkono mwanamke utakuwa umemuandalia maisha mazuri ya hapo baadaye pia wanawake wajasiriamali wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa wanapambana na umaskini na hivyo kuinua kipato cha familia zao.
Musindo alisema, “Moja ya malengo ya ILO ni kutoa nafsi  kwa wanawake na wanaume  ili waweze kufanya kazi kubwa, za kati na ndogo ambazo zitawaongezea kipato katika mazingira ya uhuru, usawa na ubinadamu kwani ujasiriamali ni chanzo kikubwa cha mapato, ajira na uzalishaji mali”.
Aliendelea kusema kuwa tamasha hilo litawakusanya maelfu ya wanawake wajasiriamali ambao wataweza kubadilishana mawazo, ujuzi pamoja na kujifunza teknolojia mbalimbali za kuzalisha bidhaa zao pia wataweza kupata masoko ya kuuza bidhaa zao na kujipatia fedha.
Naye Mwenyekiti wa kamati ya MOWE Elihaika Mrema alisema kuwa tukio hilo  limekuwa likiadhimishwa hapa nchini tangu mwaka 2006 baada ya kujifunza kutoka nchi za Ethiopia mwaka 2004 na Zambia mwaka 2005.
Mrema alisema kuwa sababu za kuanzishwa kwa MOWE ni baada ya kutambua changamoto zilizokuwa zinawakabili wajasiriamali wanawake wakiwemo wenye ulemavu na waishio na VVU. Changamoto hizo ni uwezo mdogo wa kuyafikia masoko ya uhakika, ukosefu wa mitaji, maeneo bora ya kuzalishia bidhaa au kufanyia biashara, kushindwa kumudu gharama za utangazaji wa bidhaa au huduma wazalishazo na ugumu wa upatikanaji wa habari.
“Matokeo ya MOWE ni kutangaza kwa vitendo mafanikio ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii yaliyotokana na juhudi za wanawake wa rika zote, mijini na vijijini wakiwemo wenye ulemavu na waishio na VVU”, alisema Mrema.
Tamasha hilo ambalo hufanyika kila mwaka kwa mwaka huu linaratibiwa na Taasisi ya WAMA na litakusanya  wadau kutoka mikoa yote nchini hasa wanawake wa rika zote wakiwemo wenye ulemavu na waishio na VVU huku kauli mbiu ikiwa ni “miaka 50 wanawake wajasiriamali tunaweza tutumie Fursa”.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...