Na Idara ya Habari Maelezo,Pemba.
Wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba wamesikitishwa na kitendo wanachodai kufanyiwa na Masheha wa Mkoa huo kwa kupandisha bei ya vibali vya kuuzia Mazao mbali mbali likiwemo zao la Karafuu kwa kutozwa shillingi elfu moja wakati Mkoa wa Kusinui Pemba hutoza shillingi mia tano tu.
Wamesema kiwango hicho wanachotozwa Wananchi wa Mkoa huo ni kikubwa mno na kinaweza kusababisha wananchi wa mkoa huo wenye Karafuu kidogo kuzirundika nyumbani hadi kuwa nyingi jambo ambalo Serikali hailipendelei hata kidogo.
Wananchi hao wameyaeleza hayo leo wakati walipokutana na wajumbe wa Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Fedha Biashara na Kilimo katika ziara yao walipokuwa wakivitembelea Vituo mbali mbali vya Ununuzi wa Karafuu vya Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar (ZSTC).
Wamesema kuwa bei inayotozwa na Masheha hao katika uuzaji wa vyeti vya Mazao sio sahihi ikilinganishwa na bei inayotolewa naWilaya ya Mkoani na Chake Chake zilizopo Mkoa wa Kusini Pemba ambapo kila Wilaya hutoza Shillingi mia tano tu.
Wananchi hao wamesikitishwa sana kuona Fedha hizo zinakusanywa na Masheha hao na wamedai hazitumiki kwa lengo lililokusudiwa la kuzichangia Halmashauri za Wilaya mapato yake na badala yake wamedai kuwa huingia katika mikono ya watu wachache.
Masheha wa Mkoa wa Kaskazini Pemba wamewaelezea wajumbe wa kamati hiyo iliopo chini ya Mwenyekiti wake Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni Salmin Awadh Salmin kuwa wao hununua vitabu hivyo vya Risiti kwa kila kimoja chenye kurasa mia moja kwa bei ya shillingi sitini elfu wakati wenzao wa Mkoa wa Kusini Pemba hununua kitabu kama hicho kwa shillingi elfu thelathin tu..
Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Baraza la Wawakilishi Fedha, Biashara na Kilimo Salmini Awadh Salmin amewaagiza wakuu wa Wilaya ya Wete na Micheweni katika Mkoa wa Kaskazini Pemba kulisimamia suala hilo nakulipatia ufumbuzi wa haraka iwezekavyo ili azma ya Serikali ya ununuzi wa Karafuu Katika Vituo vya ZSTC ifanyike bila ya matatizo yoyote yale
Amesema katika kipindi hiki Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejikita katika uokoaji wa zao hilo la Karafuu hivyo malalamiko ya Wananchi yasiposhughulikiwa yanaweza kusababisha LENGO la Serikali lisifikiwe.
Afisa Mdhamini wa Wizara ya Biasahara Viwanda na Masoko Pemba Hemed Suleiman nae ameahidi kulichukuwa nakulifanyia kazi tatizo hilo ili lengo na azma ya Serikali yakulifufuwa zao hilo lifikiwe.
Hata hivyo Kamati ya Fedha Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi kwa ujumla imeridhishwa nakazi nzuri inayofanywa na ZSTC katika harakati za ununuzi wa zao hilo katika Vituo mbali mbali kisiwani Pemba.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...