Rais Jakaya Kikwete, akiwa ameongozana na Mama Salma Kikwete, akitoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki alipowasili uwanja wa Maisara Zanzibar jana jioni kujiunga na Watanzania katika kuomboleza msiba huu mzito kwa Taifa la Tanzania
Rais Jakaya Kikwete akiwa msibani Zanzibar jana jioni pamoja na Rais wa Zaanzibar Dkt Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad, Rais Mstaafu wa Zanzibar Dkt Amani Abeid Karume na viongozi wengine.

Picha na Othman Mapara

Na Mwandishi Maalumu

KUFUATIA msiba mkubwa uliotokana na ajali ya kuzama kwa meli ya Spice Islander katika bahari ya Hindi usiku wa kuamkia  Jumamosi, Septemba 10, 2011, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ameamuru maombolezo ya kitaifa kwa muda wa siku tatu kuanzia leo tarehe 11 Septemba, 2011 ambapo bendera nchini zitapepea nusu mlingoti.
Aidha, kufuatia msiba huo, Mheshimiwa Rais, ameahirisha ziara rasmi ya kiserikali ya siku tatu nchini Canada ambako alikuwa amealikwa na Gavana Mkuu wa nchi hiyo, Mheshimiwa David Johnston.
Katika ziara hiyo iliyokuwa ifanyike kuanzia tarehe 14 – 16 Septemba, 2011, Mheshimiwa Rais angekutana pia na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Mheshimiwa Stephen Harper. Mheshimiwa Rais ameiomba Serikali ya Canada kupanga ziara hiyo kwa tarehe za baadaye.
Rais alitembelea majeruhi katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar, kuwajulia hali, baada ya ajali hiyo. Akiwa katika ziara hiyo ya majonzi aliarifiwa kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ilikuwa imechukua maamuzi kadhaa kukabiliana na hali ya ukoaji wa watu katika ajali hiyo.
Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuchangia kiasi cha sh. milioni 300 ili kusaidia zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kusaidia kusafirisha na kuzika miili ya watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo. SMZ imetoa sh milioni 100 kwa shughuli hiyo.
Serikali ya Muungano pia imeamua kukubali msaada wa wapigaji mbizi kutoka Afrika Kusini kwa ajili ya kusaidia kufanya tathmini ya jinsi meli ilivyozama na kuokoa maisha ya watu ambao watakuwa wamebanwa ndani ya meli hiyo.
Aidha leo, Septemba 11, 2011, Kamati ya Taifa ya Ulinzi na Usalama itafanya kikao chake mjini Zanzibar kuzungumzia hali ya ajali hiyo kwa maana ya kupata maelezo kamili kuhusu ajali hiyo, kupokea ripoti ya ajali, kufanya tathmini ya ripoti hiyo na kutoa maelekezo ya jinsi ya kukabiliana na hali ya sasa na hali ya baadaye ya usafiri wa maji nchini.
Hata hivyo kabla ya kikao hicho, tayari Rais Kikwete ameamua kufanyika kwa uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha ajili hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Hizo siku 3 za maombolezo ina maanisha jumatatu na jumanne kutakua hamna kufanya kazi Tanzania nzima?

    ReplyDelete
  2. Uchunguzi wa nini? Tunajua hiyo meli ilibeba abiria zaidi ya uwezo wake. Tunajua hiyo meli ilikuwa ya mizigo sio kubeba abiria. Uchunguzi wa nini kama sio KULA hela za walipa kodi bure?

    Kinachohitajika ni kuangalia taratibu na kanuni tulizonazo. Je, ilikuwaje meli ilikuwakuwa inauwezo wa kubeba chini ya abiria 500 ikaruhusiwa kuwa na zaidi ya abiria 800. Je ilikuwaje kama hii meli ni ya mizigo ikaruhusiwa kubeba abiria? Sheria zetu zinasemaje na wahusika walikuwa wapi?

    ReplyDelete
  3. You are our true leader Mr President. God bless Tanzania.

    ReplyDelete
  4. hata kama unajua chanzo kimoja, huenda kuna vyanzo vingine. Mfano kwani hii ni mara ya kwanza kubeba abiria wengi? kwani hii ni meri ya kwanza or chombo cha usafiri cha kwanza kubeba abiria wegi?
    Busara ambayo inajulikana kimataifa ni kufanya uchunguzi wa kina, wewe ambaye unadhani pesa za walipakodi zitaliwa pole. Ndio maisha yalivyo na ndio busara kwani gharama ambayo itatumika ni ndogo kuliko maisha yaliyopotea na yatakayopotea hapo baadae kama hatukuuondoa mzizi wa fitina.

    Salute to the president for your reactions!! wasio taka kukubali achana nao. ndio wingi ulivyo.

    G7
    Bongo

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...