Jumuiya ya Watanzania Jimbo la Michigan imepokea kwa masikitiko makubwa habari za msiba wa kitaifa ambapo watu zaidi ya 200 wamepoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa kufuatia kuzama kwa meli ya Mv. Spice Islanders usiku wa kuamkia Jumamosi ya tarehe 10 Septemba, 2011.
Tunaungana na Watanzania wengine kutoa pole na rambirambi za dhati kwa wale wote waliopoteza ndugu, jamaa na familia katika tukio hili la kushtua na kusikitisha. Tunawaombea faraja wale wote ambao wamepoteza ndugu na jamaa zao na wale wote ambao hadi hivi sasa hawana uhakika wa walipo ndugu zao na hivyo kuwa katika hali kubwa ya wasiwasi.
Tunatoa pole na rambirambi kwa Rais wa Zanzibar na kupitia kwake kwa wananchi wote wa Zanzibar pamoja na serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa Msiba huu mkubwa wa kitaifa.
Tunaungana na wale wote ambao wanaombea hali ya utulivu na mshikamano katika muda huu wa majonzi. Pamoja nao tunaamini kuwa wakati muafaka utakapofika uchunguzi huru na wa wazi utaonesha kwa kina sababu ya ajali hii kubwa ikizingatiwa kuwa ajali kama hii imewahi kutokea nchini Mei 21, 1996 kwa kuzama kwa Mv. Bukoba kwenye Ziwa Victoria.
Tunaamini kuwa uchunguzi huo utasababisha mabadiliko yenye kuhakikisha usalama na uwajibikaji ili kulinda maisha ya watumiaji wa vyombo mbalimbali vya usafiri nchini na kuliepusha taifa na athari za majanga makubwa kama haya.
Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu pema peponi. Amen!
Ayub Mfinanga
Mwenyekiti Wa TAMI.
(Tanzania Association Michigan)
Detroit, Michigan.
U.S.A


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...