Kufuatia mafuriko yaliyokumba eneo la reli ya kati ya Stesheni za Gulwe na Godegode mkoani Dodoma usiku wa kuamkia Jumanne Desemba 20, 2011, Uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania -TRL ulisitisha huduma ya usafiri wa reli ya abiria iliyokuwa iondoke Dar es Salaam Jumanne Desemba 21 saa 11 jioni kwenda Kigoma.

Kwa vile kazi ya kukarabati njia ya reli katika maeneo hayo ilikadiriwa kuchukua wastani wa siku 2 Abiria wa treni ya hiyo walitakiwa kufika katika Stesheni husika ili warejeshewe nauli zao kuanzia Desemba 20, 2011.

Wakati huo huo Uongozi wa TRL umekodi mabasi yapatayo 29 kuwasafirisha abiria na wafanyakazi wapatao 1834 waliokuwa katika treni iliyokuwa inatoka Kigoma kuja Dar ambayo ilikuwa imekwama Dodoma wakati huo.

Basi la kwanza liliondoka stesheni ya reli Dodoma kuja Dar es Salaam Desemba 20 saa 11:50 jioni, hata hivyo kutokana na kipindi hiki kuwa cha Siku kuu upatikanaji wa mabasi ukawa wa shida sana, hadi usiku jana Desemba 21, 2011 kulikuwa ndio kumepatikana mabasi 22 tu!

Baada ya wahandisi na mafundi wa TRL kufanikiwa kurejesha mawasiliano kati ya maeneo ya stesheni za Gulwe na Godegode treni ya abiria kutoka Kigoma iliyokuwa imekwama Dodoma iliondoka na abiria wapatao 200 mnamo saa 7 usiku kuamkia leo Desemba 22, 2011 na kufanikiwa kupita salama eneo la mafuriko na imewasili mjini Morogoro saa 9:00 Alasiri ambako wamepanda mabasi matatu yaliyokuwa yakiwasubiri na tayari wako njiani kuja Dar.

Aidha imeshindikana abiria hao kuja moja kwa moja Dar es Salaam na treni kwa vile maeneo kati ya stesheni za Block Post Ilala na Puga –Mpiji yako katika matengenezo

Wahanga hao waliokuwa wapatao 1834 kwa muda wote waliokuwa Dodoma wakisubiri huduma ya usafiri mbadala walilipwa fedha za kujikimu kununulia chakula na TRL.

Hivi sasa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TRL Mhandisi Kipallo Aman Kisamfu yuko eneo la stesheni za linalokarabatiwa la Gulwe na Godegode ili kufanya tathmini ya mwisho pamoja na Wahandisi na Mafundi wanaomalizia ukarabati wa eneo hilo lililoathirika na mafuriko..

Imetolewa na Afisi ya Uhusiano

Kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji -TRL Mhandisi Kipallo Aman Kisamfu

MIDLADJY MAEZ
Meneja Uhusiano
TRL -Makao Makuu
Dar es Salaam
Desemba 22, 2011

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. Safi sana TRL kwa kazi nzuri na kujali wasafiri....Tutafika tu hakuna shaka kazeni buti, inawezekana kabisa bila hata ya wahindi wala wazungu sisi wenyewe tukijali na kuweka maslahi ya taifa mbele!!!

    ReplyDelete
  2. Uwezekano upo zaidi ya hii TRL, upasuaji wa panya hauna tofauti na upasuaji wa binaadamu, misingi mikuu ya uendeshaji wa genge la dagaa hauna tofauti sana na uendeshaji wa kiwanda cha chuma!

    Tujiamini na tuwe wafanisi ili kuendesha mambo yetu menyewe bila kuwa tegemezi kwa Wageni wezi!

    ReplyDelete
  3. Suala la Ufanisi ktk uendeshaji Mdau wa pili hapo juu umetoa mwangaza!

    Mfano tuliona Bosi wa zamani wa Shirika letu la ndege ATCL lilipokuwa na ndege 3 tena za kukodi na yeye akaajiri wafanyakazi zaidi ya 300!

    Sasa kwa misingi ya kushindwa kuliendesha shirika hili kubwa kwa tija ina maana yule Bosi wa zamani wa ATCL hawezi hata kuendesha Genge la Dagaa!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...