Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,Bernard Membe akishiriki utiaji saini Mkataba wa Makubaliano ya Mpaka wa Bahari wa Tanzania, Comoro na Ushelisheli. Katikati ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Ushelisheli , Jean-Paul Adam na Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro, Mohamed Ben Charif. Hafla hiyo ilifanyika juzi katika Ofisi ya Mambo ya Nje ya Ushelisheli mjini Mahe.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,Bernard Membe akishikana mikono na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ushelisheli, Jean-Paul Adam (kulia) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro, Mohamed Ben Charif (katikati) mara baada ya kulitiana saini Mkataba wa Makubaliano ya Mpaka wa Bahari wa Tanzania, Comoro na Ushelisheli.

Na Mwandishi Wetu

Serikali za Tanzania, Ushelisheli na Comoro zimesaini Mkataba wa Makubaliano ya Mpaka wa Bahari ya Hindi baina nchi hizo.

Utiaji saini huo ulifanyika Februari 17, mwaka huu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Ushelisheli, mjini Mahe.

Katika hafla hiyo, Tanzania iliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Ushelisheli iliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Jean-Paul Adam; na Comoro ilimtuma Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano, Mohamed Ben Charif.

Baada ya kusainiwa, Hati Thibitisho hizo zitapelekwa katika Umoja wa Mataifa ambako mipaka rasmi ya nchi hizo itathibitishwa na kutambulika kimataifa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Membe alisema kutiwa saini kwa hati hizo ni ukamilishaji kazi hiyo iliyochukua miongo miwili.

Alisema mataifa mengi ya Afrika yana migogoro ya mipaka, jambo ambalo limekuwa likisababisha migongano ya mara kwa mara kati ya nchi husika.

Alisema kutambuliwa kwa mipaka rasmi kutasaidia kuondoa migogoro, hasa pale inapotokea kuvumbuliwa kwa madini na rasilimali nyingine kwenye mipaka ya nchi husika.

Alisema ni robo tu ya mipaka katika nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara, ndiyo isiyokuwa na migogoro. Mwaka jana kwenye Mkutano wa Wakuu wa Umoja wa Afrika (AU) kuliongezwa muda wa kumaliza matatizo ya mipaka hadi mwaka 2017.

Aliipongeza Serikali ya Shirikisho ya Ujerumani kwa kuwezesha kukamilika kwa kazi ya upimaji mipaka kati ya Tanzania, Ushelisheli na Comoro. Serikali hiyo imekuwa mwezeshaji mkuu wa Programu ya Mipaka ya AU (AUBP).

“Baadhi ya mipaka inachorwa kwa bunduki na damu, tumechagua kuchora mpaka wetu kwa kalamu na wino. Tumekitendea haki kizazi chetu kijacho…tuiepushe Afrika na migogoro…,” alisema Membe.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Jamani haya makubaliano ya kienyeji-enyeji inakuwaje?kitu sensitive kama mipaka inabidi wananchi wahusishwe hata ikiwa ni kwa kupitia wawakilishi wao kadhaa lakini huu usiri usiri ndo nchi inaendelea tu kuuzwa na hawa jamaa.Na bahari ni muhimu saana kwasaabu hapo unaongelea samaki unaongelea mafuta unaongelea gesi unaongelea usafirishaji nk

    ReplyDelete
  2. acha siasa mdau....haya mambo yanaenda kitaalamu zaidi.

    ReplyDelete
  3. COmoro imeshaingizwa mkenge, Zanzibar mo?

    ReplyDelete
  4. Wajameni! Mbona sijaona mwakilishi kutoka Zanzibar ambako hivi karibuni Mwakilishi wa mji mkongwe alikuwa akilalamika kutohusishwa kikamilifu serikali ya mapinduzi ya Zanzibar katika Tanzania kuomba kuongezewa mipaka ya bahari?

    Mwe! sasa si itaonekana wazanzibari kazi yao kulalama tu wakati wana masuala ya msingi? wacheni kuwaburuza wenzenu mwe?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...