Ewe bwana Mwamgongo, wa kule pwani ya Tanga
Asante kwavyo vigongo, vinavyocheza pachanga
Kana kwamba ni bolingo, waipendayo waTanga
Zangu mie shukurani, kunogesha libeneke
Na weye bwana Mroki, Hakika sijamaizi
Kwamba nawe wajikoki, kunogesha simulizi
Nilidhani husomeki, kwenye zetu anga hizi
Zangu mie shukurani, kunogesha libeneke
Zangu mie shukurani, kunogesha libeneke
Enyi marenga wa Pwani, mwanikosha kwa makeke
Yalosheheni utani, wa kunifanya nicheke
Zangu mie shukurani, kunogesha libeneke
Sina nia na upande, wa kushabikia hapa
Tungo zenu kama kande, zenye mchuzi wa papa
Wa kupenda na apende, la na aondoke hapa
Zangu Mie shukurani, kwa kunogesha libeneke
Katika zama za sasa, kweli adimu kuona
Wadau wenye hamasa, kwazo hoja zenye vina
Nyie kweli ni vitasa, na mfanowe hamna
Zangu mie shukurani, kunogesha libeneke
Hoja yangu mie hapa, kuhamasisha wadau
Muendelee kutupa, tuliyokwisha sahau
Mashairi ninaapa, wengi tumeyadharau
Zangu mie shukurani, kwa kunogesha libeneke
Naomba muendelee, kuleta vina na ngeli
Wadau wachekelee, umahiri wa kweli
Ya gubu tuyakemee, kwa hasira na ukali
Zangu mie shukurani, kwa kunogesha libeneke
Mshindi hapa hakuna, wala mshindwa wa hoja
Twendelee kubishana, bila ugomvi wa haja
Mashairi yatafana, kwa juhudi za pamoja
Zangu mie shukurani, kwa kunogesha libeneke
Beti hizi zinatosha, Mwamgongo na Mroki
Tuendelee kupasha, bila chuki na hamaki
Kwa we kinachokuwasha, lia chozi la samaki
Zangu mie Shukurani, kwa kunogesha libeneke
Na Ankal
Libeneke litanoga, cheka mbavu ziraruke,
ReplyDeleteWengine litawatoga, pepesuka waanguke,
Mwenye lake siwe mwoga, hapa sasa ndio pake,
Vina mizani vimwaga, ujumbe pake ufike!
Mwaweza fahamishana, lolote siharibike,
Mengi haelimishana, bakora zitumike,
Mabaya hakosowana, mtu asikasirike,
Vina mizani vimwaga, ujumbe pake ufike!
Enheee
ReplyDeleteMjomba una fiti kotekote!
Kumbe Ankal na wewe ni bonge la Malenga wa Mashairi ehhh?