Katibu Mkuu wa Umoja wa  Mataifa, Ban Ki Moon akiwa na Dkt Asha-Rose Migiro katika hafla ya kumuaga rasmi iliyofanyika leo katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa baada ya kumaliza muda wake kama Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
 Dkt Asha-Rose Migiro akiongea katika hafla hiyo ya kumuaga rasmi
 Katibu Mkuu wa Umoja wa  Mataifa, Ban Ki Moon akiongea katika hafla hiyo
 Dkt Asha-Rose Migiro baada ya kupokea zawadi ya maua katika hafla hiyo ya kumuaga rasmi

·         
   *Yamshukuru kwa mchango wake katika kutetea afya ya wanyonge
·         *Yasema alikuwa na mchago mkubwa sana katika vita dhidi ya malaria, ukimwi, kifua kikuu na afya ya wanawake na watoto
·         *Ban ki Moon asema alikuwa si mtu wa makuu na mtu wa watu

Na  Mwandishi Maalum

Mashirika ya  Umoja wa Mataifa yanayohusika na  masuala ya  Idadi ya Watu ( UNFPA),Ugonjwa wa Ukimwi ( UNAIDS) na   Mpango wa  kupambana na Ugonjwa wa Malaria ( RBM) jana jumanne yaliandaa tafrija kamambe ya kumshukuru  na kumuaga Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha-Rose Migiro.
 Tafrija hiyo ya aina yake  na ambayo  mgeni  rasmi alikuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa  Mataifa, Ban Ki Moon,  akiambatana na mke wake na kuhudhuriwa pia na  wadau  mbalimbali  akiwamo Mtendaji  Mkuu wa UNDP Bi Helen Clark, mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao katika UM,  sekta binafsi na taasisi za kiraia imefanyika hapa makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Akizungumza wakati wa  tafrija hiyo, Katibu Mkuu Ban ki Moom ameleezea baadhi ya  sababu  zilizomsukuma  kumteua Dkt. Asha- Rose Migiro kuwa msaidizi wake wa karibu.
 “ Nilianza kumfahamu Asha- Rose Migiro wakati huo sote tukiwa mawaziri wa mambo ya nje  katika nchi zote. Uwezo wake na uelewa wake wa mambo ulinivutia sana, lakini nilivutiwa zaidi pale nilipofahamu kwamba aliwahi kuwa waziri anayehusika na masuala ya wanawake na watoto. Nikajiridhisha kwamba huyu ndiye alikuwa ananifaa kuwa msaidizi wangu wa karibu” akasema Ban Ki Moon na kuufanya umati ulihohudhiria tafrija hiyo kushangilia kwa nguvu.
 Kama hiyo haitoshi, Ban Ki Moon amemuelezea Dkt. Asha- Rose Migiro kama msaidizi wake wa karibu ambaye licha ya kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa lakini ni mtu ambaye alikuwa hana makuu na wala hata siku moja hakujikweza.
“ Katika kipindi chote ambacho Migiro amekuwa msaidi wangu wa karibu, amenisaidia katika mambo mengi, ni mtu muadilifu sana, ni mtu aliyekaribu sana na watu, aliyeamsha matumaini na kuwapa tabasamu watu waliokuwa katika mazingira magumu.  Daima amekuwa mstari  wa mbele kunisaidia  na hakuna hata siku moja alipojikwenza. Na kwa sababu hii  anastahili tafrija hii” akasisitiza Ban Ki Moon.
Aidha Ban Ki Moon akamuelezea  Asha- Rose Migiro kama kiongozi ambaye daima alitoa kipaumbele  cha aina yake katika masuala ya afya ya jamii  eneo alilotumia uwezo wake wote, maarifa yake yote kama naibu katibu mkuu kupigania afya ya wanawake na watoto na watu wote walio katika mazingira magumu
Kwa upande wao waandaaji  wa tafria hiyo na wakizungumza kwa nyakati tofauti wamemuelezea  Naibu Katibu Mkuu, kama kiongozi ambaye mchango  wake umesaidia sana katika  kuihamasisha jumuiya kimataifa kuweka mkazo wa aina yake katika kushughulika afya ya jamii.
Bw. Michel Sidibe, Mkurugenzi mtendaji wa  UNAIDS yeyé alimuelezea Asha- Rose Migiro kama dada yake ambaye sifa zake zinaazia mbali.
“ Asha- Rose Migiro ni dada yangu, ni dada ambaye anasifa za kipekee, ni mwanamke wa kwanza  aliyefaulu  kwa daraja la kwanza katika sheria kutoka chuo kikuu cha dar es Salaam,  ni mwanamke wa kwanza kuwa waziri wa mambo ya nje nchini Tanzania,  na ni mwanamke wa kwanza kutoka afrika kuwa naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa” akasema Bw. Sidibe kauli iliyoamsha tena makofi kutoka kwa wageni waalikwa.
Hakuishia hapo, Michel Sidibe akamuelezea Migiro kama kiongozi aliyefanya kazi  kwa karibu na  Shirika lake katika kuhakikisha kwamba  maambukizi ya  virusi vya ukimwi yalikuwa yakipungua ikiwa   ni pamoja na kupatika kwa tiba ya uhakika kwa waathirika.
“ Tunakila sababu leo hii kumshukuru kwa namna alivyoshirikiana nasi, na ingawa  unaondoka lakini tambua kwamba mchango wake utaendelea kukumbukwa na kuenziwa” akasisitiza  Bw. Michel Sidibe.
Naye  Mkurugenzi Mtendaji wa  Shirika la Umoja wa Maifa la  Idadi ya Watu, Dr. Babatunde Osotimehin amesema  juhudi kubwa zilizoonyeshwa na  Naibu Katibu Mkuu  katika  kushughulikia masuala ya afya ya jamii, kumefanikisha kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya vifo vya wanawake vitokanavyo na uzazi  hali kadhalika vifo vya watoto wachanga chini ya miaka mitano.
“Katika kipindi  cha uongozi wako, umefanikisha sana katika kuhamasisha  jumuia ya kimataifa kuongeza  misaada yao na kutoa kupaumbele katika afya ya mama na mtoto, tunakushukuru sana kwa hili, na   Mungu aendelee kukubariki” akasema Dr. Babatunde Osotimehin.
Kwa upande wake,  Bw. Herve Verhoosel,  Mwakilishi wa  Mapango wa kupunguza Malaria, yeyé alimuelezea  Dkt. Asha-Rose Migiro kwamba chini ya  uongozi wa Ban Ki Moon, ameweza kujenga misingi bora ya  ushirikiano   na muamko   miongoni mwa wadau mbalimbali katika kuhakikisha kwamba  kunakuwapo na uhusiano kati ya sekta za umma za zile za binafasi katika kutimiza malengo ya afya ya jamii ikiwa ni pamoja na kasi ya kupunguza malaria
 Akiwashukuru waandaji wa tafrija hiyo, Naibu Katibu Mkuu amemshukuru Katibu Mkuu Ban Ki Moon kwa kumuamini kuwa msaidizi wake wa karibu katika kipindi cha miaka mitano na nusu.
Akasema   ingawa yeyé amejituma  na kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu, lakini amefanya hivyo kwa kuwa Ban Ki Moon alimuamini kwamba anaweza. Na kwamba daima ataendelea kuienzi heshima hiyo.
Akatumia fursa hiyo kumueelezea Ban Ki Moon kama kiongozi ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba kila mtoto angalau alikuwa analala kwenye chandarua, akina mama wajawazito walikuwa hawapotezi maisha kutoka  na uzazi.
Aidha  Migiro amewashukuru kwa moyo wa dhati wasaidizi wake wa karibu  aliofanya nao kazi akiwa naibu katibu mkuu na kwamba bila wao asingefika hapo alipo, akawashukuri pia wadau mbalimbali wakiwamo mabalozi kwa ushirikiano wa hali na mali waliompatiwa muda wote wa miaka mitano na nusu

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 10 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 14, 2012

    karibu nyumbani kipenzi chetu, umeiwakilisha Tanzania vyema,pamoja na kuitangaza Tanzania dunia nzima Mungu akubariki na akupe afya njema daima.

    ReplyDelete
  2. AnonymousJune 14, 2012

    Well come Home our sisy, for all the best you have done you deserve congratulation, you do the best lol...

    ReplyDelete
  3. AnonymousJune 14, 2012

    well done Asha Rose Migiro, nafuata nyayo zako..

    ReplyDelete
  4. AnonymousJune 14, 2012

    Angalieni namna kuagwa UN kulivyo simple, hakuna stage lilipambwa maua,viti ni vya kawaida hamna pedera, wala matambara hakuna maua ya gharama, na Asha Rose hakupewa hata kitabu, kapewa mauwa tu ambayo bei ni $30. Hebu tusome mfano huo, na nguo aliyovaa ya kawaida tu, bazee la bei kidogo. Hakuna kikundi cha ngoma (Huku vikundi vinacost 250,000 na 10% juu). Yaani ndio maana bajeti haitoshi. Petty cash ya boss ya kunulia sambusa na cake, apple basi secretary na messenger ndio hiyo hiyo. Na hamtaki kuacha.

    ReplyDelete
  5. AnonymousJune 14, 2012

    Well done Dr Asha Rose Migiro, unakaribishwa home kishujaa na kama Mh. Dr JK akikupa post msaidie mama kumaliza muda wake salama. All z best

    ReplyDelete
  6. AnonymousJune 14, 2012

    anony hapo juu umenigusa! mambo huko majuu simpo simpo tu! a biggup mama!

    ReplyDelete
  7. AnonymousJune 14, 2012

    Mawaziri wa CCM Matumbo moto...Mama Migiro lazima apewe nafasi na JK. Karibu Mama...Unayo kazi nyingine ya kupambana na mafisadi.

    ReplyDelete
  8. AnonymousJune 15, 2012

    Ma Migiro Welcome home, hongera toto la weru weru, umetusafisha nyuso. all the best, Mchango unasubiriwa hapa nyumbani kwa hamu kubwa. We are very proud of you.

    ReplyDelete
  9. AnonymousJune 15, 2012

    HAYA HAYA JUNGU LIMEIVA, BAN KI MOON KAKUMWAGIA SIFA TELE ZA UADILIFU, KARIBU KWA MAFISADI, TUNAKUOMBEA MUNGU USIWE MMOJA KATIKA HAO, NAWAONAJE WANAVINYANGANYIRO VYA URAIS 2015 MATUMBO MOTO, MAMA NCHI IMEOZA USIKUBALI HATA KIDOGO KUCHUKUA WATAKUCHAFUACHAFUA TU, HAPA UFISADI NA UVIVU NDIO UNANAFASI UKIWA MCHAPA KAZI HUNA CV. KARIBU TENA.

    ReplyDelete
  10. AnonymousJune 15, 2012

    MAMA MAMA MAMA HUYOOOOO KARIBU MHESHIMIWA MIGIRO, KARIBU DADA, HAPA NDIO KWENU JAPO SIFA NI UFISADI, KARIBU MAMA UTOE MCHANGO WAKO PENGINE UTAOKOA JAHAZI, HONGERA SANA KWA KAZI NZURI ULIYOFANYA UN, UMETUFUTA TONGO.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...