Samahani sana Anko, naomba uweke hii hoya yangu kwenye libeneke lako ili niweze ku-share mawazo yangu na watanzania wenzangu popote walipo. Nimeshindwa kuvumilia kukaa na mawazo haya moyoni mwangu kutokana na jinsi hali ya Muungano wetu inavyojadiliwa na kuhusishwa na Katiba mpya ambayo mchakato wake umeanza kushika kasi.

Kama alivyowahi kusema Mh. Zitto “idadi ya wapinga muungano inazidi kuongezeka siku hata siku. Ukiwauliza kwa nini hawataki muungano wanasema aah, basi tu. Kama ni Mzanzibari atasema Tanganyika wanatutawala. Kama ni Mtanganyika atasema Wazanzibari wamezidi kelele, tunataka Tanganyika yetu. Lakini ni lazima tuurekebishe Muungano huu. Ulivyo sasa utavunjika tu. Kuulinda muungano ni kuufanyia marekebisho makubwa”. Kusema kweli hoja yangu kubwa iko hapa, na inatokana na sababu kubwa mbili zinazofanya nikose imani kabisa na wanasiasa wetu. 

Moja, ni hii tabia ya wanasiasa wengi kutosema ukweli kuhusu kwanini wazanzibari wengi hawataki muungano. Sijui kama ni kweli kwamba hawajui wazanzibari wanalilia nini hasa? au hawajafanya utafiki wa kutosha kujua kwanini wazanzibari wengi wanapinga huu muungano?
Jamani, tatizo kubwa la wazanzibari si udini kama baadhi wanavyodhani, si wabara wanaoishi au kufanyakazi Zanzibar, si wakristo wanaopenyeza ukristo Zanzibar, si uwiano wa nafasi za ajira katika taasisi na mashirika ya umma, na wala si mafuta kama wengine wanavyofikiria. Haya na mengine ambayo sikuyataja ni geresha tu, ila shida kubwa ya wazanzibari ni UTAIFA.

 Wazanzibari wanaona kwamba kuwa kwao ktk muungano kumeua kabisa nchi yao. Wanataka wajulikane na mataifa mengine kama nchi. Wanaamini wakijulikana kama nchi na mataifa mengine watapata fursa nyingi ambazo wamekuwa wakizikosa kwa kuwa ndani ya muungano. Tena ukiongea na wazanzibari kuhusu marekebisho ya muungano, watakwambia wanataka muungano kama wa nchi za Ulaya au kama ule wa EAC (shirikisho) ambapo kila nchi inajulikana kama nchi ndani ya muungano. Kwa hiyo shida kubwa ya wazanzibari iko hapa! Na ukitaka kutimiza kiu ya wazanzibari maana yake utavunja muungano wa sasa (kitu ambacho serikali ya JK haiku tayari kukiona), halafu sasa ndo mkae mjadili kuhusu hilo shirikisho.

Sababu ya pili ya msingi wa hoja yangu, ni kuhusu marekebisho ambayo wanasiasa wetu wanapendekeza yafanyike ili kuulinda muungano. Kusema kweli hapa ndo nachoka kabisa, maana mapendekezo yao mengi yanaangalia zaidi maslahi yao binafsi na ya vyama vyao kuliko wananchi wanaowaweka katika madaraka. Wabara wengi, Chadema, CUF n.k wanaamini kwamba hoja ya kuwa na serikali tatu ndo itakuwa suluhisho la matatizo ya muungano. Binafsi nasita kuamini hilo kwa sababu hoja ya serikali tatu itakuwa haijategua kitendawili cha utaifa wa wazanzibari, hivyo wataendelea kuupinga tu muungano. Kwa maana hoja hii itakuwa ni mzigo bure kwa serikali katika kuziendesha hizi serikali tatu, na utakuwa ni ufujaji wa pesa za walipa kodi. Isitoshe ni hoja yenye kulenga kuwapa ulaji wanasiasa kwa kuwatengenezea nafasi nyingi za kisiasa.

Ngoja nimalizie hoja yangu kwa kutoa angalizo. Mchakato wa katiba mpya umeanza. Serikali imeishaahidi kuwa itahakikisha mchakato unamalizika kwa wakati ili katiba mpya iweze kutumika katika uchaguzi mkuu ujao. Hizi zinaonekana kama habari njema sana kwa vyama vya upinzani na watanzania kwa ujumla ambao wamekuwa wakilalamikia mapungufu yaliyomo katika katiba ya sasa katika kuhakikisha demokrasia ya kweli inatendeka katika kuchagua viongozi wetu wa kisiasa. 

Lakini nyuma ya pazia kuna hili! Watu binafsi, vyama vya siasa, na taasisi mbalimbali vinashauri baada ya kuandaa rasimu ya katiba mpya basi ipelekwe kwa wananchi kupigiwa kura ya maoni (referendum). 

Huu ni ushauri mzuri lakini kutokana na hali ilivyo nashawishika kusema uchaguzi ujao unaweza kufanyika kwa kutumia katiba ya zamani, unajua kwanini? Kuna kila dalili kuwa wananchi wengi hasa wa Zanzibar hawawezi kupitisha rasimu ya katiba mpya ambayo haitatambua utaifa wao. 

Kwa maana hiyo kuna uwezekano mkubwa wa katiba mpya kukataliwa na wananchi. Je hali hii ikitokea itakuwaje? Kumbuka uchaguzi mkuu utakuwa umekaribia, je itabidi rasimu ikafanyiwe marekebisho kwanza halafu irudi tena kwa wananchi kupigiwa kura ndo uchaguzi ufanyike? Au itabidi uchaguzi ufanyike tu kwa katiba ya zamani? Au je itabidi serikali iliyopo madarakani iendelee tu hadi katiba mpya itakapopatikana ndo uchaguzi ufanyike?
Wadau nawasilisha!
Mdau Halisia

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 14 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 01, 2012

    well said

    ReplyDelete
  2. AnonymousJune 02, 2012

    Mada yako inajikanganya, mfano unasema tatizo la Wanzibara kutaka kuvunja Muungano si kwa kuwa kuna mafuta,Uislamu au kuongezeka kwa Ukristo bali ni kutaka kuwa nchi yao ili wapate fursa zaidi. Sasa fursa gani wanazotaka ambazo hawataki Waliotoka Bara wakae hapo? au fursa gani wanataka kuchoma makanisa ya Wakristo?? kulalamika kuwa Wakristo wanahamia Zanzibar kwa wingi?? umejaribu kufukiri lakini bado hujapata jibu sahihi. Zanzibar wana mambo kadhaa ambayo hata ukisema sio tatizo lakini ni tatizo , Zanzibar wanashida na Wakristo wanaohamia huko kutoka Bara, kama wangehamia Waislamu kutoka Bara isingekuwa tatizo sana kwa sasa(japo bade litakuwa tatizo)
    Zanzibar wana hisia za wao kuwa Waarabu na kuutaka uurabu kwa nguvu, na hata wale Wazenji weusi lakini Waislamu wanajiona kuwa wao ni Waarabu. Zanzibar wana ubinafsi na mafuta yao wanafikri kwa kuwa wapo wachache basi watakuwa matajiri kwa mafuta. CUF wanataka Zanzibar ijitenge ili wapate kuongoza nchi kwa jinsi wanavyoona ni nzuri kwao.
    Na wakijitahidi wakiuvunja Muungano kabla ya miaka hamsini mingine kwisha labda wataomba kurudisha Muungano au watajigawa zaidi kuwe na sisi Waarabu wa Pemba ninyi Wanyamwezi au Wamakonde wa Unguja na Bara.
    MUNGU IBARIKI TANZANIA

    ReplyDelete
  3. AnonymousJune 02, 2012

    Safi sana, brilliantly put.... Utaifa ni hoja ya msingi

    ReplyDelete
  4. AnonymousJune 02, 2012

    Sasa wewe ndio 'watchdog' wa waZanzibari. Umejiuliza, iwapo wananchi watairidhia CUF iongoze Zanzibar huru, tatizo liko wapi! Wananchi ndio wenye mamlaka ya kuchangua ni chama gani kiongoze nchi yao na ni mfumo gani wa maisha unawafaa.

    Tatizo lako (kama walivyo wenzako wengi), mmeshazoea kututawala ndio maana mnaleta maneno mengi mkituona waZanzibari tunadai nchi yetu!

    Halafu, huu ni mwaka 2012, acha siasa zako za 'Nyerere' (ambaye, wengi wenu mnamuona kama Mtume), ilhali, alivyoviamini vingi vimeshindwa ku-survive, mf; siasa ya ujamaa na kujitegemea, vijiji vya ujamaa, Azimio la Arusha n.k. Na muungano, pia utafuatia.

    Tuacheni tupumueeeee!

    ReplyDelete
  5. AnonymousJune 02, 2012

    Hawa wachangiaji wawili wamesema ukweli ulivyo kwa sura mbili za shilingi moja. Sura ya mbele UTAIFA na nyuma DINI. Somo: Sudani ya Kusini na Kaskazini. Je tuwachie UN ama Tz tunaweza? USHIRIKIANO WETU HAUTAYUMBA kama haki ikitendeka vilicvyo.
    (maoni binafsi)

    ReplyDelete
  6. AnonymousJune 02, 2012

    Mchangiaji wa Sat Jun 02,12:31:00 AM 2012, sasa wewe ndio 'watchdog' wa visiwa vya Znz?! Mamlaka hayo umepewa nani,au mabwana zako wa Marekani na wa Ingereza?!

    Sisi (wa Zbari wengi) tunataka nchi yetu yenye mamlaka kamili. Na wala msijidanganye kwamba tutakufa masikini,endapo muungano huu utavunjika. Tukishakuwa na znz yetu huru na nyie Tanganyika yenu huru,tutaangalia kama ipo 'haja' ya kuungana. Tena si kwa mfumo huu wa KIKOLONI kama uliokuwepo sasa.

    Tuacheni tupumueee.....!

    ReplyDelete
  7. AnonymousJune 02, 2012

    mdau wa mwanzo wewe ndo kabisa hamnazo sijategemea katika karne hii kuna mtu hamnazo kama wewe, well its true tunataka UTAIFA WETU NA SIO KWAMBA HATUWATAKI WAKIRISTO WAJE HUKU NO THATS NOT TRUE AT ALL, SOME HISTORIA YETU BWANA USILETE BLA BLA HAPA NA KUJIFANYA MUEREFU KUMBE PUMBA PUMBA

    NENDA ARABUNI UONE AU FANYA RESEARCH UONA ALIYE MUARABU HALISI NI WA NGOZI GANI,KAMA HUJUI BASI NI WA NGOZI NYEUSI

    MUUNGANO UMETULETEA BALAAA BIN BALAA BIN TAAFRANI NA TUNATAKA KUVUA HIVI SASA TUPUMUWEE JAMANI

    SAY AND WRITE WHAT EVERY YOU WANT BUT WE ARE EXHAUSTED WITH THIS MUUNGANO WENYE MFUMO KIRISTO.

    UMETULETEA MADAWA YA KULEVYA,VIJANA KWA WAZEE WAMEATHIRIKA,UMETULETEA UMALAYA, USENGE,USAGAJI ETC

    MUUNGANO GANI WAKATI KATIKA WIZARA YA MAMBO YA NJE HATA MZANZIBARI HATA MMOJA HAYUPO NA UN,RAIS WETU NDO RAIS AKIFIKA HUKU KWENU KAWA WAZIRI,MITIHANI YETU WATOTO WETU WAKIFAULU MAASKOFU WAKIJA JUU MITIHANI INAFUTWA MNAWAZIMU BADO TU TUTAKE MUUNGANO, MUUNGANO HUU HAKUNA HAKI SAWA KWA SOTE,MUUNGANO WA AINA GANI NENDENI MKAUNGANE NA WAKENYA,NA KONGO ETC

    TUNATAKA NCHI YETU PERIOD SAY AND WRITE WHAT EVER YOU WANT BUT ONE DAY WE WILL GET OUR NATION AND WE WILL STAND UP PROUD LIKE WE USED TO.INSHALLAH MAY ALLAH HELP US.AMIN.
    WAZEE WETU WAMEDHALILIKA NA HATA MPAKA SISI NA KUONEWA KAMA WATOTO MAYATIMA. ENOUGH IS ENOUGH

    WE HAVE ALREADY WOKEN UP FROM OUR COMA SLEEP NA HATUTA WACHA KUPIGANIA NCHI YETU MPAKA KIELEWEKE
    KWA NGUVU ZA RABANA ATAKUWA PAMOJA NA SISI AMIN.

    ReplyDelete
  8. AnonymousJune 02, 2012

    na sisi WATANGANYIKA tumechoka na tunasema MUUNGANO NI UTUMWA. Muungano uvunjwe hata kesho kila mtu aiche katika nchi yake kwa amani.

    ReplyDelete
  9. AnonymousJune 02, 2012

    Huyu anonymous wa hiyo second comment inaonekana hata haijuwi hii zanzibar. Kwanza Wanzibara ni kina nani? Mwandishi wa hii article ameeleza kwa ufasaha tatizo la muungano kwa wazanzibar. Na hilo ndio tatizo kubwa. Ndio yapo mengine madogo madogo lakini si kweli kwamba wazanzibari wanachukia wakristo. Wakristo wamekuwapo enzi na enzi huko zanzibar. Tulisoma nao, temefanya kazi nao, na tunaendelea kuishi nao katika kila kichochoro. Mambo yaliotekea hivi karibuni hayana uhusiano wowote na wazanzibari kudai utaifa wao. Usisome tu kwenye vigazeti uchwara uchwara na kuyajaza kwenye kichwa chako. Bali fuatilia kwa makini na utajuwa ukweli mambo. Kuna baadhi ya Watanganyika wanafikiria hii Zanzibar ni sehemu ya Tanzania tu kama vile ilivyo morogoro au kisarawe, hawajuwi kwamba kabla ya muungano zanzibar haikuwa wilaya au mkowa wa tanganyika bali ilikuwa ni nchi kamili na wana haki kamili ya kuujadili huu muungano wakiona kama hauna manufaa na wao.

    ReplyDelete
  10. AnonymousJune 02, 2012

    anoni wa pili unafikiri kwa moyo.

    hivi zanzibar inaweza kuomba msaada nje kujengewa barabara billa wizara kupinga au ku-divert hela ziende rungwe au mpanda?

    ReplyDelete
  11. AnonymousJune 02, 2012

    wanaona jinsi walivyobadilika kutoka NHCI kwenda KITONGOJI

    ReplyDelete
  12. AnonymousJune 02, 2012

    Ndugu zangu W'TZA tunapojadili mambo ya UTAIFA tujaribu kuwa WAZALENDO na 'OBJECTIVES'

    Tusijaribu kutanguliza maslahi ya dini zetu tukaacha UTAIFA nyuma, 'afterall' dini ni imani ya mtu na haina uhusiano wa moja kwa moja na maendeleo, ndio maana hata wale wasio kua na dini kabisa wapo ambao 'mambo safi'

    Mkiharibu nchi yenu hata kama mnalala makanisani, misikitini au kwenye mahekalu mjue mtaumia tuu!

    Hili neno UDINI sio la kulihubiri hasa kwa vile lina maana pana zaidi ya watu wanavyofikiria.

    Neno UDINI halina maana ya kupenda dini au kuchukia waumini wa wadini nyingine bali ni kuwanyima watu fursa za kisiasa, kiuchumi au kijamii kwa kutumia misingi ya DINI. jambo ambalo kwenye nchi yetu halipo!

    Sasa hivi kuna watu tayari wanasema waumini wa dini fulani ktk nchi hii wananyimwa fursa hizi kwa kisingizio cha kwamba hawakusoma huku wakiuliza kama hawakusoma basi hata zile za UDEREVA, UMESENJA, ULINZI, UANGALIZI WA OFISI, USEKERETARI NA UPISHI WA CHAI pia hawawezi?

    Jamani kama kuna mtu anaona hawezi kuishi ktk nchi yenye mchanganyikao wa imani aombe uraia wa SAUDI ARABIA, VATICAN, ZAMBIA, PAKISTAN, IRAN. au ISRAEL atuwache tupumzikeeeeee!

    ReplyDelete
  13. AnonymousJune 02, 2012

    "Na sisi watanganyika tunasema, tunasema tumechoka, MUUNGANO ni UTUMWA. uvunjike hata kesho, kila mtu aishi ktk nchi yake kwa amani"

    Ndugu yangu, unapokuwa kwenye bahari au ziwa ukisema umechoka kuogelea ujuwe utakufa maji!

    Sijui utakuwa na msaada gani lakini sisi wenzako tunahisi nchi yetu ina mambo mengi ya kushughulikia badala ya kupambana na AL SHABAB ambao watakua only 25miles from mainland coast.

    ReplyDelete
  14. AnonymousJune 03, 2012

    Waacheni wazanzibari na Zanzibar yao....tunawacheleweshea maendeleo, Tanganyika yenyewe longo longo kibao, mambo hayaendi. Mi naaminiwakipewa nchi yao watapata maendeleo haraka sana na maisha kwao yatakuwa mazuri sana coz wapo serious na wanaweza kuchukua maamuzi magumu katika jambo lolote

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...