Kesi ya mauaji ya aliyekuwa mtoto wa Chifu Abdallah Fundikira, Swetu Fundikira imeanza kusikilizwa leo katika Mahakama Kuu Kanda ya dar es Salaam ambapo mashahidi wawili Mtangazaji wa TBC, Benedicto Kinyaiya na Sostenes Mbuya walitoa ushahidi wao.

Washitakiwa katika kesi hiyo ni wanajeshi, Rhoda Robert, MT 85067 Mohamed Rashid na Koplo Ali Ngumbe, aidha wanadaiwa kumuua Fundikira kwa kukusudia Januari 23, 2010 saa 1;30 usiku katika Barabara ya Mwinjuma eneo la Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Mbele ya Jaji Zainab Mruke wakiongozwa na wakili wa serikali Charles Kato, mashahidi hao walitoa ushahidi wao.

Shahidi Ben Kinyaiya alielezea kuwa Januari 22, 2010 alitoka kwenda kwenye starehe zake Mango Garden, kabla hajafika hapo alikutana na Swetu akamuuliza 'wapi hiyo?' alimjibu 'Mango'.

Alidai mahakamani hapo kuwa baadaye kidogo akiwa njiani barabara ya Mwinjuma kwenye mataa ya kuungana na barabara ya Kawawa alikuta kundi la watu kama kuna ugomvi akamuona Swetu akaamua kuegesha gari pembeni kumfata.

Alipofika hapo swetu alikuwa shati imechanika kifuani na mdomo unadam kama mtu aliyepigwa, alimuuliza nini tatizo? alidai Swetu alisema 'wananipiga hawa, wananipiga hawa, wananipiga hawa.'

Beni ambaye anadai kuwa anamfaham Swetu kwa miaka mingi alimuuliza chanzo cha ugomvi huo lakini mshitakiwa mmoja kati ya hao watatu ambaye ni mwanamke alimjibu kuwa kama anahitaji maelezo zaidi aende polisi Ostabey wanampeleka huko.

"walimuingiza Swetu kwenye gari ili waondoke naye, mimi nilivuka barabara ambako nilipaki gari langu nikapanda nikawahi huko polisi," alidai Beni.

Alidai kuwa alipofika huko hakuwakuta wale watu waliomchukua Swetu wala Swetu na hata alipouliza mapokezi kama kuna watu walifika hapo muda mfupi uliopita walidai hakuna, aliamua kusubiri nje.

Anadai baada ya nusu saa hajawaona kufika hapo aliamua kuondoka kuendelea na ratiba zake akiamini watakuwa waliamua kumalizana na kumuacha andelee na mambo yake.

Aidha alidai baada ya muda akiwa kwenye pub ya Zonghua Garden alipigiwa simu na rafiki zake aliemtaka atoke nje, alitii na alipofika nje wakamueleza kuwa wamepokea taarifa kuwa Swetu ametupwa eneo la Sea View na kwamba wakati huo alikuwa anapelekwa Polisi Salenda Breage na baada ya hapo akapelekwa Hospitali ya Muhimbili.

waliondoka kwenda huko salenda,ambapo lilikuja Difender la Polisi na kuegeshwa hapo, aliweza kumuona Swetu ndani amelazwa amevimba sana mwili umejaa majeraha na damu lakini akiwa mtupu bila nguo. baadaye waliondoka kumpeleka Muhimbili.

Hata hivyo katika maelezo yake Beni alishindwa kuieleza mahakama kuwa ni kwanini katika maelezo yake ya polisi hakueleza kuhusu kwenda kwake salenda na kama alimuona marehemu akiwa katika hali mbaya kwenye Difender.

Beni pia alishindwa kueleza ni saa ngapi na lini aliandika maelezo hayo polisi. na ni kwanini baada ya kutomkuta Swetu kituo cha polisi Osterbey kama kweli alikuwa jamaa yake hakuendelea kumtafuta nyumbani kwake au kwenda kutoa taarifa kwa ndugu zake badala yake aliendelea na starehe zake.

Kwa mujibu wa shahidi, Mbuya alidai kuwa alikuwa na Swetu siku ya tukio akiwa amempakia katika gari lake ambalo ni taxi huku akiwa amekaa siti ya nyuma, baada ya kuipisha gari ya washitakiwa pale Mango na wao kuendelea na safari yao, walipofika kwenye eneo la tukio alikuja mmoja wa watuhumiwa na kumpiga kibao.

Alidai Swetu alishuka garini na kwenda upande ule wa dereva na kuanza kumuondoa yule mtu aliempiga kibao Mbuya, wale washitakiwa wengine walishuka kwenye gari lao na hapo ndipo ukaanza ugomvi ambao ulikusanya watu kuja kushangaa kinachoendelea.

Madereva Taxi waliokuwepo eneo hilo walifika katika eneo la tukio na walishauri waende kituo cha polisi,washitakiwa wakajitambulisha kuwa wao ni askari na wakatoa na vitambulisho vyao huku wakisema wanatangulia na Swetu kituo cha polisi kwa kutumia gari yao na kumtaka Mbuya awafate. 

hata hivyo shahidi huyo aliambiwa na Swetu arudi pale kijiweni kwa Ben kuwapa taarifa jamaa zao aende nao polisi.

Aliwaacha hapo washitakiwa na Swetu yeye akatangulia kutoa taarifa kama alivyotumwa wakaenda polisi Osterbey. hawakuwakuta washitakiwa wala Swetu.

Hata hivyo shahidi huyo alidai kuwa anamfaham Swetu kama mteja wake katika baa ya Kontena pale Kinondoni. Kesho yake alisafiri kwenda Dodoma, akiwa huko alipata taarifa kuwa Swetu ni mgonjwa sana na amelazwa anahitajika aje kutoa maelezo polisi akaamua kurudi, akiwa njiani alipata taarifa kuwa amekufa.

Kesi hiyo bado inaendelea kusikilizwa mahakamani hapo na Washitakiwa wanaendelea kusota rumande kutokana na kesi ya mauaji kuwa haina dhamana.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 11 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 04, 2012

    Huo ndiyo utawala wa sheria. Kila kitu kiko wazi, lakini bado mawakili wa utetezi wataendelea kuonyesha maujuzi yao ya sheria na kufanya mahakama kuendelea kubemenda pesa za walalahoi kwa miezi, pengine miaka!

    ReplyDelete
  2. AnonymousJune 05, 2012

    kama huo ndo ushaidi hakuna kitu hapo bora watafutwe mashaidi wengine waliona na wako serious

    ReplyDelete
  3. AnonymousJune 05, 2012

    Wanajeshi wamezoea kuchukua sheria mikononi wanajiona wao wako juu ya sheria na washaua raia wengi sana na pia kuasababisha vilema ka raia.Tunatarjia hakiitendeke katika hili na liwe fundisho kwa wanajeshi na askari wengine wanaodhani wako juu ya sheria.Nikimuangalia huyo mwanamke mwanajeshi muuaji nasikia hasira mpaka natamani kulia.

    Tumuombe MUNGU awape uvumilivu familia ya marehemu maana kesi hii inawakumbusha uchungu na maumivu ya kumpoteza ndugu yao.

    ReplyDelete
  4. AnonymousJune 05, 2012

    hawa wanjeshi wanadhani kazi yao ni kupiga raia, hapana, ni kupiga wanaopiga raia.

    wajeshi wasiofaham maana ya kazi yao, hawana nidhamu ya kazi hawa.

    ReplyDelete
  5. AnonymousJune 05, 2012

    Wewe unaesema kila kitu kiko wazi una uhakika gani? Je umesikia maelezo ya upande wa pili? Usiwe na haraka kiasi hicho,kesi ni maelezo ya pande mbili,sio mmoja. Hata nyumbani kwako ukiamulia wanao kamwe usimwadhibu mmoja kwa kugombana na mwenzie kabla hujapata maelezo ya upande wa pili.

    ReplyDelete
  6. AnonymousJune 05, 2012

    si shangai hii,mimi ilinikuta siku moja natoka kazini majira ya saa 12jioni nikakutana na kundi la watu,kuuliza nikaambiwa kuna madada walikuwa wanapigana hivyo polisi doria wamewakamata wanawapeleka kituoni msimbazi,ile nashaangaa nikastukia nimechapwa kibao cha uso nikasukumwa na kuunganishwa kwenye lile kundi,nilijitetea lkn wapi kulikuwa na ofisa wa kike huyo alikuwa kama kala pilipili haelewi kitu.mpaka kuja kuachiliwa ilikuwa saa 5 usiku.hii ndo bongo yetu.

    ReplyDelete
  7. AnonymousJune 05, 2012

    Kaka hii inasikitisha sana hasa pale unapoona wale wanaotakiwa kuchungunga usalama wetu ndio wanatisha zaidi kuliko hata majambazi. Kama hawa jamaa walio husika walijitambulisha kama ni askari basi hakuna budi kuuliza jee viongozi wao wanajua juu ya haya? Uchunguzi wa kina unahitajika kujua kama hizi ni mila za jeshi au kikundi fulani ili kama inahitajika basi viongozi husika wawajibishwe au mafunzo zaidi yanahitajika. Wakati umefika kwa raia wema kuishinikiza serikali juu ya jukumu lake la kulinda maisha ya raia wake. Wanasheria wakujitolea nao hii ni sehemu ya kuingalia juu ya kuwapatia wanyonge haki kwa kushtaki sio tu wahusika wa tukio bali hata taasisi zao. " corporate liability". Viongozi wetu wanajali raia wakati wa kura tu sasa inabidi sisi wenye tujaliane kwani hili laweza kumfika yeyote yule.

    ReplyDelete
  8. AnonymousJune 05, 2012

    So very sad.
    Dr Gangwe.

    ReplyDelete
  9. AnonymousJune 05, 2012

    Ben na Mbuya hamkusadia kuokoa maisha ya Swetu, mliwezaje kuwaamini hao jamaa na kuwaacha waendelee kumwadhibu Swetu? hata kama ni askari hawakuwa na haki ya kuchukua sheria mikononi. Wewe dereva kama Swetu alikuwa mteja wako wa siku nyingi kwanini ulimwacha na wauaji? Wewe Ben kama Swetu alikuwa rafiki yako wa siku nyingi kwanini ulimwacha na wauaji? RIP rafiki yangu wa utoto nakumbuka tulikuwa tunacheza chandimu wote, wewe pekee ukiwa umevaa njumu za addidas.

    ReplyDelete
  10. AnonymousJune 05, 2012

    Hawa mbongola ndio zao, hivyo vitambulisho vyao ndio tiketi za dhulma uswahilini na mitaani...sasa mjomba Ben ndio anajikuta ananyooshewa vidole mahakamani kama vile yeye ndio mkosaji!!! au kama vile yeye ndie alikuwa bodigadi wa marehemu, kimjinimjini alijua 'kimeeleweka' wamemuachia...usiku huo angeweza vipi kwenda eti kumuulizia nyumbani!??...ndio maana watu tunakwepa sana kutoa hizi nyushahidi na 'kusaidia polisi'

    ReplyDelete
  11. AnonymousJune 05, 2012

    bongo hakuna amani kabisa. roho mkononi tu. askari hawa! wanaua watu bila ya makosa hawa. ugomvi wa barabarani watu wanatoana roho. Dunia imekwisha jamani, mbona kwa mwenyeezi mungu siku ya malipo kuna kazi kwelikweli. Wameidhuilumu nafsi yake bure, innalillah wainailaahih rajiun. Mwenyeezi mungu amuweke pema swetu, wauwaji nao wauawe, maana kisasi ni haki.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...