Katibu Tawala wa mkoa wa Kigoma Bw. Sekulu Selungwi akifungua warsha ya wadau wa sheria katika wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma.
Katibu Tawala wa Wilaya Bw. Moses Msuluzya akizungumza katika warsha hiyo.
Afisa Sheria wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Mercy Mrutu akitoa ufafanuzi wakati akiwasilisha mada ya Utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa maafisa wa Jeshi la Polisi, Magereza, Uhamiaji, JWTZ, TAKUKURU, Mahakimu, Wanasheria na Walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari wilaya ya Kigoma.
Sehemu ya washiriki wa warsha.

Katibu Tawala wa mkoa wa Kigoma Bw. Sekulu Selungwi amesema upo umuhimu wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kufanya mapitio ya sheria za ardhi namba 4 na 5/1999 na sheria ya madini Na. 14/2010 ili kuondoa muingiliano wa majukumu wakati wa utekelezaji wa sheria hizo.

Bw. Selungwi amesema hayo jana wakati wa warsha juu ya masuala ya sheria kwa umma kwa wananchi wa mkoa wa Kigoma iliyokuwa ikiendeshwa na maafisa kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania katika wilaya ya Kigoma mkoani humo.

Bw. Selungwi alisema kwa mujibu wa sheria ya madini kifungu cha 16 Waziri wa madini anaweza kutwaa eneo la ardhi na kulitenga kwa shughuli za uchimbaji madini bila kujali kwamba ardhi hiyo ni ya kijiji au ya umma na hivyo kuamsha migogoro kati ya wawekezaji na wananchi.

Aidha, alisema sheria ya ardhi imekuwa ikichangia uwepo wa migogoro aliyoieleza kuwa imekuwa ikichukua sehemu kubwa ya muda wa watendaji katika maeneo mbalimbali na mahusiano baina ya wananchi vijijini huathirika pale wanapofikishana katika mabaraza ya ardhi na kusisitiza kuwa hali hiyo huwa mbaya zaidi pale uamuzi unapotilewa na kuwa tofauti na matarajio ya upande mmoja.

Alisema mapitio ya sheria hizo na nyingine yatasaidia kuondoa imani potofu kwamba serikali inawajali wawekezaji na kuwakandamiza wananchi wazawa.

Aidha, katibu tawala huyo wa mkoa wa Kigoma ametaka utafiti pia kufanyika kuhusu sheria ya wakimbizi ili mianya kuhusiana na sheria hiyo iweze kubainishwa na utaratibu wa kupeleka mapendekezo ya marekebisho ya sheria hiyo kunakohusika uweze kufanywa kwa ufanisi.

Hata hivyo, alisema ni wazi marekebisho hayo yatakapofanywa hayatovunja misingi ya haki za binadamu lakini bila shaka yataweka mazingira salama kwa wananchi wanaoishi jirani na kambi za wakimbizi.

Kwa mujibu wa Bw.Selungwi mkoa wa kigoma umekuwa mwenyeji wa wakimbizi kutoka Burundi na DRC kwa karibu miaka 20 mfululizo. Alisema hali hiyo siyo tu imesababisha kuwepo kwa changamoto nyingi za kiutendaji katika vyombo vya ulinzi na usalama bali imeondoa woga wa wananchi kwa makatazo yaliyowekwa na sheria mbalimbali.

Alisema kuwa, kutokana na hali ya kijiografia na historia ya mkoa wa Kigoma zipo changamoto ambazo si rahisi sana kuzilinganisha na maeneo mengine hali inayofanya mkoa huo kuwa tofauti sana na mikoa mingine. Alibainisha kuwa ukiwa Kigoma si ajabu ukakutana na migogoro ya ardhi, biashara na migogoro mingine ya kijamii kati ya watanzania na raia wa nchi nyingine na kubainisha kuwa migogoro ya aina hiyo ina changamoto zake na kwa kiasi kikubwa inaziweka sheria na viongozi wa utawala katika mtihani mkubwa.

Aidha, Katibu Tawala huyo wa mkoa wa kigoma alisema kuwa pamoja na Tume ya Kurekebisha Sheria kuwepo kwa karibu miaka 29 sasa bado shughuli zake hazijafahamika wazi katika maeneo mengi ingawa umuhimu wake uko wazi na uwepo wake umekuwa na manufaa ya kutosha kwa wananchi hivyo basi ameitaka kufanya kazi ya ziada kutambulisha shughuli za Tume katika maeneo mengi zaidi kwa kushirikiana na makundi mbalimbali ya wananchi ili kuwapa uelewa na kupata maoni yao.

Warsha hiyo ilikuwa ikiendeshwa na maafisa wa Tume ya kurekebisha sheria ikiwa na lengo la kuwaelimisha wananchi wa Wilaya ya kigoma mkoani Kigoma kuhusiana na Tume ya Kurekebisha Sheria, Utatuzi wa migogoro ya ardhi pamoja na suala la Jumuiya ya Afrika Mashariki

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...