Jumapili iliyopita nilizungumia umuhimu wa kupata na kuhifadhi kumbukumbu kwa njia ya picha, hususan kwenye matukio ya kihistoria kama ya Olimpiki, ya wanamichezo wetu wakiwa katika michuano hiyo kwa faida ya vizazi vya leo na kesho.
Mada hiyo ilitokana na ukweli kwamba sisi wa-Tanzania hatuna utamaduni wa kutuma mtu ama watu wa kuweka kumbukumbuku hizo adhimu, tukitegemea tu mashirika ya habari, ama picha mbili tatu zinazopigwa na wanamichezo wenyewe ama viongozi wao ama marafiki kwa ajili ya albamu binafsi badala ya rekodi za kitaifa ambazo ni muhimu kuwa nazo.


Naam, zipo njia kadhaa za kuhifadhia picha kibao unazopiga, ambazo si lazima iwe katika kompyuta yako, ambayo, nasisitiza, hujaa baada ya muda si mrefu kutokana na ukubwa wa faili za picha kutoka kwenye kamera yako.
Wakati njia ya kwanza, ambayo hapa nadiriki kusema ni ya muda mfupi, ni hiyo ya kushusha picha zako katika kompyuta. Ila  nadhani ni vyema kuanza kujifunza  kutumia njia mbadala ili kuokoa nafasi katika kompyuta yako.
Njia hiyo ya kwanza ni kutumia CD ambazo hata hivyo  kwa bahati mbaya, kiwango chake cha kuhifadhi picha ni mdogo, ukizingatia kwamba CD moja ina uwezo wa kuchukua picha zenye ukubwa usiozidi megabyte (MB) 700 tu. Yaani, baada ya kuhifadhi picha kwenye kompyuta, unachukua CD na kuchoma mafaili yote ya picha na kuyahifadhi humo, kabla ya kufuta ili kurejesha nafasi kwenye kompyuta yako.
Hivyo unajikuta inakulazimu uwe na rundo la CD kutosheleza mahitaji yao. Nayo njia hiyo ya CD nadhani tuiweke kwenye fungu la njia mbadala ya kwanza na ya  muda mfupi tu. Vingienvyo baada ya muda mfupi tu utajikuta unatafuta kabati zima la kuhifadhia hizo CD ambazo nazo zina mchezo wa kupoteza ubora na hata kufuta kabisa uhalisia wa picha zako, hasa hasa usipozitunza inavyotakikana. Na hapo sijazungumzia adha ya kukwaruzika ama kuvunjika kwa bahati mbaya, na kukutia hasara ya kupoteza faili zenye kumbukumbu zako muhimu.

Nashukuru kwamba wengi waliafikiana nami, na wengi zaidi walitoa maoni kwamba kasoro hiyo lazima ifanyiwe kazi, vinginevyo tutajikuta hatuna kumbukumbu ya wanamichezo wetu wakiwa ulingoni.
Wadau wengine walikwenda mbali zaidi, kutaka kujua mbinu mbalimbali za kuhifadhi picha, ikizingatiwa kwamba siku hizi wengi wetu hutumia kamera za digital, na mahali pekee pa kuhifadhia wengi wanajua ni katika kompyuta zao tu. 

Na hii ndio mada yangu ya leo; kuzungumzia njia mbalimbali za kuhifadhia taswira zetu, ikizingatiwa kwamba faili za picha za digital ni kubwa mno kiasi ya kwamba haichukui muda nafasi katika kompyuta hujaa haraka, na kumfanya mtu ahangaike na asijue la kufanya.

Njia ya pili, ambayo kidogo ina nafuu katika kuhifadhi picha zako ni kutumia DVD ambazo nafasi yake ambayo huwa ya takriban gigabyte (GB) 4. Hivyo hata kama unapiga picha nyingi, uwezekano wa wewe kukomboa nafasi kwenye kompyuta ni kuzihifadhi katika DVD. Hapo utajikuta unatumia DVD chache na picha nyingi zikahamishiwa humo. 
Njia hii pia nayo ni ya muda mfupi, maana kama unapiga picha nyingi, itakubidi pia uwe na rundo la DVD ili kukidhi mahitaji. Hizi nazo zina hatari ya kupata madhara kama zilivyo CD.
Njia muafaka na nzuri ya kuhifadhi picha zako kupita hizo mbili za hapo juu ni kutumia External Hard Drive (hapa tafsiri yake kwa Kimatumbi nitaomba mnisaidie, maana nimepekua kila mahali sijakuta t  inayoeleweka). Kifaa hiki, ambacho, kama zilivyo CD, utakipata kwenye maduka mengi yanayouza kompyuta na vifaa vyake, kina uwezo wa kubeba kiasi kikubwa cha faili za picha – kuanzia GB 100 hadi Terabyte (TB) 1 ambayo ni sawa na GB1000,   au hata TB2 ambayo ni sawa na GB 2000. 
Njia ingine, ambayo ni ya kisasa zaidi, ni kutumia hifadhi maalumu ya mafaili ya digital kwa njia ya mtandao. Ipo mitandao mingi ambayo inakuwezesha kutunza kumbukumbu zako mbalimbali ikiwemo za picha kwa kutotumia CD ama DVD ama External Hard Drive, bali kwa njia hii ambayo ni maarufu kama kuhifadhi mafaili hewani ama kwenye ‘mawingu’.
Kwa mifano kuna mtandao huu wa  www.dropbox.com ambao baada ya kujisajili (kama kufungua akaunti  ya email vile) unaweza kuhifadhi mafaili mbalimbali na hata picha zako pasipo kuhitaji  kubeba na  kutembea na kifaa ama chombo cha kuhifadhia hizo picha ama mafaili yako mengine.  


Hapo kazi yako inakuwa ni kukusanya  mafaili yako yote na kuyahifadhi humo. Kisha, hata kama utasafiri, popote pale penye intaneti utaweza kufungua anuani yako kwa jina na password (kama ufanyavyo wakati wa kufungua akaunti yakeo ya email) na kutumia mafaili yako wakati wowote na mahali popote palipo na intaneti.
Kama nilivyosema, zipo njia nyingi mithili ya hiyo Dropbox, ila naitaja hii kwa kuwa ni rahisi na yenye uhakika kiasi.  
Mie mwenyewe nimekuwa nikiitumia kwa muda sasa, na sijajuta. Yaani mambo ya kubeba ma CD ama ma DVD ama hata hizo External Hard drive nimeshayasahau kitambo. Maktaba yangu ya picha ipo hewani ama ‘mawinguni’, na popote nilipo, mradi kuwe na intaneti, naweza kuita mafaili yangu yote na kutumia yaliyomo. Adha ya moto, wizi ama kuharibika kwa kifaa cha kuhifadhia inakuwa haipo tena.
Uzuri mwingine wa kutumia njia hii ni kwamba endapo mtu atataka umtumie picha ni kwamba wewe kazi yako ni kufungua akaunti yako ya Dropbox, ama inayofanana nayo, kisha unatuma kwa email kupitia humo humo kwenye anuani yako. Na kama hata yeye unayemtumia  atakuwa na akaunti hiyo ya Dropbox, kazi inakuwa rahisi zaidi.
Ila tu ikumbukwe wenzetu wanatoa huduma za namna hii kibisahara. Kwa hiyo ukitaka kupata nafasi kubwa zaidi katika akaunti ya Dropbox yako inabidi ulipie kiasi, japo kwa kuanzia wanakupa ofa ya bure ya nafasi kiasi cha GB 100 hivi… Bei aghalabu si ya kutisha. Utakuta unatakiw kulipa kati ya dola 20 hadi 100 kwa mwaka, kulingana na mahitaji na uwezo wako.
Namna ya kulipia huduma hizo pia sio ya kusumbua kama unavyoweaza kudhania. Wewe kama una akaunti katika benki inayotoa huduma kama vile za Visa ama Mastecard, unaweza kununua nafasi ya ziada kwa njia ya mtandao. Nenda hapo benki ukaisajili kadi yako iunganishwe kwenye huduma ya manunuzi mtandaoni, nawe unaweza kufanya manunuzi mara moja. Fuata maelekezo ya hapo benki na yaliyo katika akaunti yako nawe utafanikiwa tu.
Njia zingine, kwa mfano wale wenye kutumia vifaa vya Apple, kama vile kompyuta, ipad na iphone, ni ile inayojulikana kama iCloud, ambayo akaunti yake pia huweza kutumika kwenye kompyuta zingine pia. 
Kazi yake nayo ni ile ile ya kuhifadhi mafaili yako ‘kwenye mawingu’. Yaani bila kuwa na haja ya kubeba vifaa vya ziada. Na hii pia unaanza kwa huduma ya dezo, nawe ukitaka nafasi zaidi unachangia uchakavu kidogo.
Natumai nimeeleweka kwa hilo, na mwenye maswali zaidi anaweza kuuliza tu, ama hata kutoa mwongozo zaidi ili wadau mnufaike. Pia jaribu kuwa mtundu wa kucheza na google na kusaka huduma za kuhifadhia mafaili kwa njia ya mtandao. 
Naomba kuwasilisha;
-Ankal

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. Ankal vipi,FUFU limekulewesha hadi umechelewa kuweka mada..?Asante Ankal,drop box nilikuwa nahifahamu sana ila sikujua kama unaweza kuitumia kwa kutunza mafaili makubwa kiasi hicho.Na umeandika kama mwandishi uliyebobea kweli kweli,haichoshi kusoma..kila nilipomaliza paragraph nilitaka kurukia inayofuata haraka.Kila ulichosema nilidhani ndiyo suluhisho kumbe kuna kingine chini yake!!

    David V

    ReplyDelete
  2. Nassor A.SAugust 13, 2012

    Nilidhani leo umetusahau au fufu la Ghana limekulevya.

    Ahsante sana hii dropbox kwa kweli sisi wengine ndio mwanzo tuisikie kutoka kwako. Tunashukuru kwa taaluma.

    Ujumbe umetufikia.

    ReplyDelete
  3. Asante kweli shule ya bure. Kweli mwisho hauna elimu!

    ReplyDelete
  4. https://drive.google.com/start#home

    Here you get 5GB free, it is not like the 2gb of dropbox

    ReplyDelete
  5. dropbox na Icloud sio teknolojia za kushabikia. Hata muasisi wa Apple alilia akipinga utumiwaji wa Icloud sasa wewe mwenye kupigia debe inaelekea hujajua maana ya data confidentiality. kama una computer yenye gigabyte 500, sidhani kama unahitaji internet kuhifadhi faili zako hata siku moja hao dropbox ambao mafaili yako ukiyaweka yanakuwa mlango wazi kwa wenye kujua nini maana ya internet hawawezi kukupa gigabyte 500 za bure. kama waungwana mjuavyo "BURE GHALI" AMA CHEAP OR FREE IS EXPENSIVE BUSINESS. Kwa hiyo mimi kama mtaalam wa mambo ya computer sishauri mtu aweke faili lake kwenye dropbox ama icloud.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...