Wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Airtel Rising Stars kwa nchi za Afrika (pichani), leo hii imetoka sare ya bao 1-1 na Burkina Fasso, katika mchezo uliofanyika katika uwanja wa Nyayo, jijini Nairobi, Kenya.
Matokeo hayo yanaiweka Tanzania shakani kusonga mbele katika michuano hiyo baada ya jana kuianza vibaya kwa kukubali kufungwa bao 1-0 na Gabon katika mchezo wake wa kwanza. Kufuatia matokeo hayo Tanzania inasubiri bahati tu ili kusonga mbele kwani sasa itabidi kushinda mchezo wake wa mwisho utakaofanyika kesho
23/08/2012 dhidi ya Zambia, na wakati huo huo kuiombea Gabon ifungwe na Zambia katika mchezo wao wa mwisho. Kila kundi itatoa timu moja kusonga mbele hatua ya robo fainali zinazotarajiwa kuanza kesho kutwa.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Kocha na mkuu wa msafara wa timu ya Tanzania, Salum Madadi alisema vijana wake walicheza vizuri isipokuwa tatizo ni kutopata muda wa kutosha wa wachezaji wake kuzoeana hasa ikizingatiwa kuwa timu hiyo inaundwa na kombaini ya wachezaji kutoka mikoa sita tofauti.
"Kwa mfano mchezo wetu wa juzi dhidi ya Gabon vijana walicheza vizuri sana pamoja na tatizo la kutozoeana hata hivyo waliweza kuwabana wapinzani kwa muda mwingi na hata kufika langoni mwa wapinzani wetu kwa kupiga mashuti kadhaa ila bahati haikua yetu tu," alisema Madadi.
Matokeo mengine ya mechi zilizochezwa jana kwa wanaume ni Kenya kutoka sare ya 1-1 na Ghana, Malawi pia kutoka sare ya 1-1 na Madagascar, Nigeria kutoka sare ya 1-1 na Niger, Congo DRC kuichakaza Chad bao 5-0
na Zambia kuichapa Burkina Fasso 5-0. Kwa upande wa wanawake Congo DRC iliichakaza Burkina Fasso magoli 8-0, Ghana nayo ikaichapa Kenya bao 7-2, Chad ikaifunga Nigeria bao 1-0 na Uganda kuifunga Sierre Leone
3-0.
Michuano hiyo ya Airtel Rising Stars kwa ngazi ya Afrika iliyoanzishwa kwa lengo la kuibua vipaji kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17, Inafikia kilele keshokutwa kwa bingwa kupatikana ambapo mshindi huyo atapata nafasi kwa wachezaji wa timu nzima kuhudhuria kliniki ya soka ya kimataifa itakayoendeshwa na jopo la makocha kutoka klabu ya Manchester United na Arsenal za Uingereza itakayofanyika kuanzia Agosti 26 hadi 30 mwaka huu jijini Nairobi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...