Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mwamuzi wa zamani wa kimataifa Msafiri Mkeremi kilichotokea leo alfajiri (Agosti 2 mwaka huu) kwenye Hospitali ya Wilaya ya Urambo mkoani Tabora.

Licha ya kuwa mwamuzi, Mkeremi aliwahi kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) sasa TFF kwa vipindi viwili tofauti. Pia aliwahi kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT).

Vilevile aliwahi kuwa mkufunzi wa waamuzi, mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF na Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) Mkoa wa Pwani.

Kwa upande wa vyama vya mpira wa miguu aliwahi kuwa kiongozi katika mikoa ya Tabora, Pwani na wilayani Mpanda katika Mkoa wa Rukwa.

Msiba wa Mkeremi uko nyumbani kwake Urambo, na kwa mujibu wa mtoto wake Masoud Mkeremi, atazikwa Jumamosi kwenye makaburi ya Msafa yaliyoko wilayani Urambo.

TFF inatoa pole kwa familia na kuitaka kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu. Pia TFF itatoa ubani wa sh. 200,000 kwa familia ya marehemu kama rambirambi zake.

Marehemu aliyekuwa akisumbuliwa na presha na ugonjwa wa kisukari ameacha wajane wawili na watoto 12.  Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi. Amina

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...