Mtoto anayetuhumiwa kukojolea Quran Tukufu pamoja na wakaazi 35 wa Mbagala, Dar es Salaam, wanaodaiwa kuchoma makanisa na kuharibu magari za Serikali wamefikishwa kizimbani  leo  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu chini ya ulinzi mkali wa Polisi.
Mtoto huyo mwenye umri wa miaka 14 (jina limehifadhiwa), na ni mwanafunzi, alifikishwa mahakamani hapo kwa shtaka la kudhalilisha dini ya Kiislamu kwa kukojolea Quran Tukufu Oktoba 10 mwaka huu, akiwa eneo la Mbagala Chamazi. Kesi hiyo inasikilizwa katika mahakama ya watoto kwa sababu mtoto huyo ana umri chini ya miaka 18.
Washtakiwa wengine  waliosomewa mashtaka yao ni Maenga Yusuph (28), Hamad Euli (26),Shego Musa (26), Abdallah Said (22),Ramadhan Salum (28), Mashaka Iman (21), Kassimu Juma (33), Ibrahim Jumanne (20), Sospeter  John (33), Hamza Mohamed (22), Mwanahamisi Mohamed (30) , Dodo Mohamed (20) na wengine 23.
Wakaazi hao wa Mbagala wanashtakiwa na makosa manne ya kula njama, kuharibu mali, wizi, kuvunja majengo na kuchoma moto makanisa  kati ya Oktoba 10 na 12 mwaka huu kwa nia ovu ya kutenda kosa.
Wakili wa Serikali, Tumaini Kweka, alimwambia  Hakimu Sundi Fimbo wa mahakama hiyo kuwa washtakiwa walivunja na kuingia ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mbagala, na kutenda makosa hayo.
Washtakiwa hao pia wanatuhumiwa kuharibu mali mbali mbali zenye thamani ya sh. milioni 500 za  kanisa la KKKT.
Pia wanatuhumiwa kuiba vitu mbalimbali  vyenye thamani ya sh. milioni 20, lakini kabla ya kuiba mali hizo walimtishia Michael Samwel kwa kutumia nondo na matofali kwa nia yakufanikiwa kuiba mali hizo.
Washtakiwa hao wanatuhumiwa kuchoma moto kanisa la ELCT, kanisa la Agape Usharika wa Mbagala na kusababisha uharibifu wa mali zenye thamani ya sh. milioni 80.
Vile vile washtakiwa wanatuhumiwa kuharibu magari tisa, ambapo thamani ya uharibifu huo ni sh. milioni 20. Katika ya gari ambazo zimeharibiwa  lipo gari la  Serikali PT 2068 mali ya Jeshi la Polisi,  gari lingine ni la  Mchungaji Kinyota.
Pia wakili wa Serikali, Ladslaus Komanya, alidai kuwa washtakiwa wanatuhumiwa kuvunja kanisa la  Tanzania Assemblies of God (TAG), KKKT na kuiba vitu mbali mbali vyenye thamani ya sh. milioni 8 mali ya Kanisa la Waadventisti Wasabato (SDA).
Mawakili hao wa Serikali walidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, na waliomba mahakama itoe masharti ya dhamana kwa kuzingatia kifungu namba 148 kifungu kidogo cha 5 (e).
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 30 mwaka huu kwa kuangalia dhamana za washtakiwa, ambapo kuna washtakiwa wengine hawatapata dhamana kwa sababu wamepatikana na shtaka la unyang'anyi wa kutumia silaha. Kisheria shtaka hilo halina dhamana kwa hiyo washtakiwa hao wataendelea kusota rumande.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 7 mpaka sasa

  1. Kukojolea Quran Tukufu ni kosa lisilovumilika na aliyelifanya aadhibiwe iwe onyo kwa wengine. Mtakaomtetea au kumpendelea mtalihatarisha taifa letu maana mchelea mwana kulia atalia yeye.

    ReplyDelete
  2. Kukojolea Quran Tukufu ni kosa lisilovumilika na aliyelifanya aadhibiwe iwe onyo kwa wengine. Mtakaomtetea au kumpendelea mtalihatarisha taifa letu maana mchelea mwana kulia atalia yeye.

    ReplyDelete
  3. watazijua mbivu na mbichi. wakitoka rumande wamechokaa, magonjwa ya ngozi, n.k, nyumbani biashara zimefungwa, wanafunzi shule wamesimamishwa, vigogo waliowachochea wafanye vurugu wanapeta tu kwa raha zao. ama kweli wajinga ndi waliwao

    ReplyDelete
  4. Mnaofundisha dini msitumie uongo au vitisho. Badala ya kuwafundisha watoto kuwa ukikojolea koran utageuka mjusi au utakuwa chizi waambieni tu kuwa msahafu unapaswa kuheshimiwa hata kama hupatikani na lolote ukiudhihaki.

    Sasa kama huyo mtoto wa kiislamu asingemwambia mtoto wa kikristo kuwa atakuwa chizi ubishi usingetokea.
    Walimu wa dini tumieni maarifa namna ya kufundisha watu kuheshimu dini.

    ReplyDelete
  5. Laiti busara ingetumika basi yote haya yasingetokea.

    Ni kweli kosa alilofanya huyo kijana ni kubwa lakini kama wazazi wangeomba radhi kwa unyenyekevu basi yangeisha.

    Bado nashauri waombe radhi ili yaishe.

    ReplyDelete
  6. anon wa Wed Oct 17, 09:37:00 AM 2012 umenifurahisha sana, ni mawazo mazuri wenzetu madrasa sijui huwa wanafundisha nini?! mh...

    ReplyDelete
  7. Jamani, kukojolea kitabu cha dini, iwe biblia, quran au kitabu chochote za hadithi za watu wa kale, sio kosa kisheria. Kama kuna moral issue basi tuseme hivyo... cha msingi tuache kufundisha watoto hadithi au 'fairy tales' za kwenye biblia na quran kama vile ni ukweli. Tuwaambie watoto ukweli unaostahili. Na ukweli ni kuwa kinachosema quran, biblia na vitabu vingine 'vitakatifu' ni theories tu na ni maswala ya imani - no truth bearing at all. Swala la huyu mtoto ni kama mtu yoyote anayekaa juu ya haki yake ya kuzungumza/kutoa maoni/freedom of expression.
    Sasa kama watu wamekuwa offended basi hayo ni matatizo ya watu wengine. Ni kosa kubwa nafikiri kukiuka haki za watu za freedom of expression. Wanaposema ati mtoto amedhalilisha dini ya kiislamu, ni nani anaamua udhalilishaji wa dini nyingine ukoje? watu wa dini? nchi ina dini gani? mimi naomba tukue kifikra, kama mtu una dini yako ni wewe na imani zako. Total waste mtoto anapelekwa mahakamani kwa mambo haya. Tunakuwa tunalea watoto kuwa waoga a kifira. Mbaya sana!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...