Balozi Ramadhan M. Mwinyi, Naibu  Balozi wa Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania katika  Umoja wa Mataifa akisisitiza umuhimu wa kuimarishwa na kujengewa uwezo kwa Idhaa ya Radio ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, ilikuwa ni wakati wa Mkutano wa Kamati ya Nne ya Baraza  Kuu la 67 la UM uliokuwa ukijadili ajenda  namba 55 kuhusu  suala la  Habari na Mawasiliano ya Umma ya  UM. Idhaa hiyo ya Kiswahili ya UM,  inaongozwa na Mtanzania Bi. Flora Nducha.  Kazi kubwa iliyofanywa na Ubalozi wa Tanzania wa kukumbushia mara kwa mara  kuhusu upungufu wa wafanyakazi katika Idhaa hiyo,  imezaa matunda baada ya  UM kupitia Idara yake ya Habari na Mawasiliano kuongeza wafanyakazi watatu kati ya watano.  Mmoja kati ya wafanyakazi hao wapya ni  Mtanzania Bi. Asumpta Masoi aliyekuwa  Mwandishi  wa Habari Mkuu  kutoka Shirika la Utangazaji  Tanzania (TBC)  

 Na Mwandishi  Maalum
Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania Tanzania imeelezea kuridhishwa  na hatua ya Umoja wa Mataifa  kupitia Idara yake ya Habari na Mawasiliano ya Umma ya  kuiimarisha na kuiongezea  Uwezo  Radio Idhaa ya Kiswahili ya Umoja  Huo.
Hayo yameelezwa  jana ( jumatano) na  Ramadhan Muombwa Mwinyi, Naibu Balozi wa  Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  wakati  alipokuwa akichangia  majadiliano  ya Kamati ya Nne ya Baraza  Kuu la 67 la Umoja wa Mataifa, kuhusu ajenda namba 55 inayohusu masuala ya  Habari na Mawasiliano  katika  UM.
            Majadiliano ya ajenda hiyo yalitanguliwa na  hotuba ya  Rais wa Baraza Kuu la 67 la UM, Bw.  Vuk Jeremic  siku ya jumanne. Siku ambayo pia Katibu Mkuu Msaidizi anayesimamia Idara  hiyo  Bw Peter Launsky-Toeffenthal aliwasilisha mbale ya wajumbe wa Kamati   taarifa yake iliyoainisha kazi na majukumu  ambayo yametekelezwa na vitengo mbalimbali vivilivyo chini yake.
“ Mwenyekiti,   ujumbe wangu ungependa kuzungumzia jambo moja ambalo kwetu  lina umuhimu wa aina yake nalo ni hili la  Radio ya Idhaa ya Kiswahili” akasema Balozi Mwinyi
Na kuongeza. “ Tangu kuanzishwa kwake Idhaa hii tofauti na Idhaa nyingine    imekuwa ikitekeleza majukumu yake katika mazingira magumu hasa ya upungufu wa wafanyakazi. Lakini  tumefarijika  na taarifa za hivi karibuni kwamba, nafasi tatu kati ya tano zilizotengwa zimekwisha kujazwa. Nimatumaini yetu kwamba na hizi mbili zilizobaki zitajazwa  mapema iwezekanavyo” akasisitiza Balozi.
Aidha Naibu Balozi amesema  kwa kuongeza wafanyakazi zaidi, idhaa hiyo sasa itatekeleza majukumu yake  kwa ufanisi, weledi  na kwa ubora wa hali ya juu. Na  hivyo kutimiza vema  jukumu lake  la msingi ambalo ni   kuhabarisha na kuelimisha mamilioni ya watu wanaofahamu lugha ya kiswahili kuhusu majukumu ya   UM.
Halikadharika  Balozi Mwinyi akaeleza  kuwa, Tanzania  inafarijika pia  kwamba   baadhi ya  machapisho yanayolenga  kampeni mbalimbali yamekuwa yakitafsiriwa  katika lugha ya kiswahili.
“   Hatua hii ya kutafsiri kwa kiswahili baadhi ya machapisho ni kielelezo sahihi cha namna UM inavyotambua na  kuthamini mchango wa lugha ya Kiswahili. Tunaelewa  hali ngumu  ya rasilimali ilivyo kwa  UM na Idara hii kwa ujumla, lakini ni imani yetu    tafsiri hizi zitaendelea kufanyika”. Akasihi.
Kwa muda mrefu na    kwa nyakati tofauti,Mabalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa  kwa kushirikiana na maafisa wao wa Kamati ya Nne na ya  Tano wamekuwa  mstari wa mbele kuzungumzia  upungufu wa wafanyakazi katika idhaa hiyo na hivyo kuutaka UM kuitafutia  ufumbuzi  hali hiyo.
Malalamiko hayo pamoja na yale ya  kupandishwa  hadhi  Mkuu wa Idhaa hiyo hatimaye  yamezaa matunda ambayo yamepelekea kuongezwa kwa wafanyakazi na Mkuu wake kupandishwa Hadhi.
Kati ya  wafanyakazi walioogezwa yupo   Bi. Asumpta Masoi aliyekuwa Mwandishi  wa Habari Mkuu wa Shirika  la Utangazaji la Tanzania ( TBC) ambaye amejiunga    hivi karibuni  na hivyo kufanya  Idhaa hiyo sasa  kuwa na Watanzania  wawili. Wafanyakazi  wengine ni kutoka Kenya na Uganda.
 Ingawa lugha ya Kiswahili si  kati ya lugha  rasmi Sita   za UM, lakini miaka kadhaa iliyopita Umoja huo,   uliamua kuazisha Idhaa ya Kiswahili  sambamba na Idhaa ya lugha  ya Kireno ili kukidhi mahitaji ya wazungumzaji wa lugha hizo  kwa lengo pia la kufikisha habari zake kwa watu wengi zaidi na wa mataifa mbalimbali.
            Lugha rasmi za UM ni Kiingereza, Kifaransa, Kiarabu, Kirusi, Kichina na kihispania.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...