Shule ya Sekondari Bagamoyo ni shule ya bweni, ya mchanganyiko, yaani yenye wasichana na wavulana. Shule hii ina wanafunzi wa kidato cha Tano na Sita pekee. Jumla ya wanafunzi wote ni 760 na kati yao 100 ni wasichana na wavulana ni 660. Shule hii ina jumla ya walimu 65 ambapo  walimu wa kike ni 36 na wa kiume ni 29.
Tarehe 5/11/2012 Shule hiyo ilifungwa kutokana na kuwepo kwa dalili za kuvunjika kwa amani na utulivu shuleni hapo.
Baada ya shule kufungwa, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi  iliunda Kamati ili kuchunguza nini hasa chanzo cha mgogoro uliopelekea hata kuwepo kwa dalili za kuvunjika amani na utulivu shuleni hapo. Kamati imekamilisha kazi yake ikiwa na taarifa nzima ya mwenendo wote wa mgomo na vurugu zilizotokea.
Katika uchunguzi imebainika kuwa chanzo kikuu cha vurugu hizo ni mfarakano kati ya uongozi wa shule na baadhi ya wanafunzi. Mfarakano huo ulitokana na wanafunzi kutokubaliana na mabadiliko ya kinidhamu ambayo Mkuu wa Shule aliyaanzisha.
Aidha, Kamati imegundua kuwa kukosekana kwa umoja wa kikazi miongoni mwa walimu, utoro wa walimu kazini na utovu wa nidhamu kwa baadhi ya wanafunzi kumechangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa mgogoro huo. 
Baada ya kupitia kwa makini hali halisi ya mgogoro huu, Serikali imeamua yafuatayo:
1.    Ili kutoa nafasi kwa uongozi wa shule kujipanga upya, wanafunzi wote waliothibitika kutoshiriki katika mgomo watarudi shuleni mapema mwezi Januari 2013 kwa utaratibu watakaotangaziwa.

2.    Wanafunzi wote waliothibitika kuwa vinara wa vurugu watachukuliwa hatua za kinidhamu.

3.    Walimu walioonekana kutokuwajibika ipasavyo watachukuliwa hatua stahiki za kinidhamu.

Aidha, Serikali inaagiza kwamba Wakuu wote wa Shule wachukue hatua za haraka na watoe taarifa kwa viongozi wa Halmashauri za Wilaya na Mikoa pindi wanapogundua dalili za mgogoro ili hatua stahiki zichukuliwe mapema. Vile vile wanafunzi wote wanakumbushwa na kuagizwa kwamba kushiriki katika migomo ni kuvunja sheria za shule na wanapoteza muda wa masomo yao. Watumie njia halali kufuatilia mahitaji yao.

Dkt. Shukuru J. Kawambwa (Mb)
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi
24/11/2012

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Maoni au pendekezo langu ni kuwa uongozi wa Shule usipewe nafasi ya kujipanga upya!
    Uwajibishwe na ujumbe utakuwa umeshafikishwa kuwa Serikali ina "zero tolerance" linapokuja suala la maslahi ya nchi.
    Mkuu wa shule naye awajibishwe kwa kuwa naye ripoti inamtaja kusababisha au kuwa na share yake katika vurugu zilizotokea.
    Uwajibishaji ninaopendekeza uwe ni adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.
    Vinginevyo ni kukaribisha mizozo ya namna hii kutokea mara kwa mara

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...