Shule ya
Sekondari Bagamoyo ni shule ya bweni, ya mchanganyiko, yaani yenye wasichana na
wavulana. Shule hii ina wanafunzi wa kidato cha Tano na Sita pekee. Jumla ya wanafunzi
wote ni 760 na kati yao 100 ni wasichana na wavulana ni 660. Shule hii ina
jumla ya walimu 65 ambapo walimu wa kike
ni 36 na wa kiume ni 29.
Tarehe
5/11/2012 Shule hiyo ilifungwa kutokana na kuwepo kwa dalili za kuvunjika kwa amani
na utulivu shuleni hapo.
Baada ya
shule kufungwa, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliunda Kamati ili kuchunguza nini hasa chanzo
cha mgogoro uliopelekea hata kuwepo kwa dalili za kuvunjika amani na utulivu
shuleni hapo. Kamati imekamilisha kazi yake ikiwa na taarifa nzima ya mwenendo
wote wa mgomo na vurugu zilizotokea.
Katika
uchunguzi imebainika kuwa chanzo kikuu cha vurugu hizo ni mfarakano kati ya uongozi
wa shule na baadhi ya wanafunzi. Mfarakano huo ulitokana na wanafunzi
kutokubaliana na mabadiliko ya kinidhamu ambayo Mkuu wa Shule aliyaanzisha.
Aidha, Kamati
imegundua kuwa kukosekana kwa umoja wa kikazi miongoni mwa walimu, utoro wa
walimu kazini na utovu wa nidhamu kwa baadhi ya wanafunzi kumechangia kwa kiasi
kikubwa kukua kwa mgogoro huo.
Baada ya
kupitia kwa makini hali halisi ya mgogoro huu, Serikali imeamua yafuatayo:
1. Ili kutoa
nafasi kwa uongozi wa shule kujipanga upya, wanafunzi wote waliothibitika kutoshiriki
katika mgomo watarudi shuleni mapema mwezi Januari 2013 kwa utaratibu watakaotangaziwa.
2. Wanafunzi
wote waliothibitika kuwa vinara wa vurugu watachukuliwa hatua za kinidhamu.
3. Walimu
walioonekana kutokuwajibika ipasavyo watachukuliwa hatua stahiki za kinidhamu.
Aidha, Serikali inaagiza kwamba Wakuu wote
wa Shule wachukue hatua za haraka na watoe taarifa kwa viongozi wa Halmashauri
za Wilaya na Mikoa pindi wanapogundua dalili za mgogoro ili hatua stahiki
zichukuliwe mapema. Vile vile wanafunzi wote wanakumbushwa na kuagizwa kwamba
kushiriki katika migomo ni kuvunja sheria za shule na wanapoteza muda wa masomo
yao. Watumie njia halali kufuatilia mahitaji yao.
Dkt.
Shukuru J. Kawambwa (Mb)
Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi
24/11/2012


Maoni au pendekezo langu ni kuwa uongozi wa Shule usipewe nafasi ya kujipanga upya!
ReplyDeleteUwajibishwe na ujumbe utakuwa umeshafikishwa kuwa Serikali ina "zero tolerance" linapokuja suala la maslahi ya nchi.
Mkuu wa shule naye awajibishwe kwa kuwa naye ripoti inamtaja kusababisha au kuwa na share yake katika vurugu zilizotokea.
Uwajibishaji ninaopendekeza uwe ni adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.
Vinginevyo ni kukaribisha mizozo ya namna hii kutokea mara kwa mara