Na Abdi Suleiman, Pemba
SAKATA la waamuzi wanaochezesha ligi daraja la pili Taifa Pemba kupigwa na wachezaji, limeendelea kurindima baada ya juzi mwamuzi mwengine kujikuta akiangushiwa kisago na wachezaji wa timu ya Chuoni.
Kasheshe hiyo imetokea katika uwanja wa Msaani, baada ya timu ya chuoni kufungwa magoli 2-1 na timu ya Nuru Boys, na kuamua kuhamishia hasira zao kwa mwamuzi wa pambano hilo, Ali Said na msaidizi wake nambari mbili Amour Ali.
Na katika hali isiyotarajiwa, wachezaji hao pia walimpa kichapo kocha wao Yahya Ali, aliyekuwa akiamua vurugu hizo zilizosababishwa na wachezaji wake. Wachezaji hao waliamua kuwachapa waamuzi baada ya kupuliza firimbi ya kumaliza mchezo, kwa madai kuwa, alivunja mechi hiyo kabla ya wakati wake.
Akizungmza na mwandishi wa habari hizi, baada ya kumalizika kwa tafrani hiyo, mwamuzi huyo alisema kuwa, katika vurugu hizo pia saa yake ya mkononi ilichukuliwa na wachezaji wa timu hiyo kutokana na vurugu walizofanya.
Mwamuzi huyo aliwataja wachezaji saba waliohusishwa na kadhia hiyo kuwa ni, Mohammed Bakari, Suleiman Ashrib, Ali Abdulrahman, Khamis Nassor, Said Ashrib, Seif Hamad na Nassor Mohamed.
Akizungumzia sakata hilo, Msaidizi Katibu wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Taifa (Pemba) Abdallah Suleiman Sharif, amekiri kusikia taarifa hiyo, na kusema kuwa taarifa kamili itatolewa baada ya kamati tendaji kupitia ripoti za mwamuzi na kamisaa.
Hata hivyo, ameelekeza lawama kwa Jeshi la Polisi, kutokana na kutopeleka askari uwanjani kwa ajli ya kuweka ulinzi, licha ya chama chake kuliandikia barua likiomba ulinzi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...