Habari Ankal,
Sisi ni vijana ambao tumeanzisha kituo cha taarifa hapa Pangani. Kituo hiki kitakuwa na mambo manne, maktaba, chumba cha computer, ukumbi wa filamu wa ndani na ukumbi wa filamu wa nje.
Maelezo zaidi yapo kwenye pendekezo ambalo nimekutumia, na watakaohitaji pendekezo hili pia tuwasiliane.
Kwa sasa tunatekeleza mpango wa maktaba na msaada tunaoumba kwa watanzania wenzetu wanaoishi ndani na nje ya nchi, ni vitabu kwa ajili ya shule za msingi na sekondari ambavyo tutavitumia katika maktaba yetu.
Pia wanaweza kutusaidia kwa kututaarifu au kutuunganisha na watu, mashirika au taasisi ndani au nje ya nchi ambazo zinasaidia mambo ya maktaba na vinavyofanana na hivyo.
Pamoja na ombi hili nimekutumia nakala ya cheti cha usajili kwa uthibitisho.
Mawasiliano yetu ni;
PANGANI INFORMATION ALLIANCE
P.O.BOX 27 PANGANI, TANGA, TANZANIA.
E-mail; panganikwetu@gmail.com
Tuko tayari kuwasiliana na yeyote atakayehitaji maelezo zaidi.
NB; Tutashukuru zaidi kama watu watatusaidia vitu zaidi kuliko fedha.
Kamburuta, Ally Said
Mratibu.



Nimeguswa na ujumbe wenu. Mimi ni profesa m-Tanzania huku Marekani. Ninakuja Tanzania tarehe 3 Januari, na nina ahidi kuwa nitawaletea vitabu kadhaa, kuchangia mpango wenu murua.
ReplyDeleteKupeleka vitabu kwenye taasisi na vyuo vya Tanzania ni kitu ambacho nimefanya tangu miaka iliyopita, kwa kujibana matumizi mengine.
Mwezi huo Januari nitakuwa katika mikoa ya Arusha na Manyara. Sina hakika kama nitapata fursa ya kuja Tanga, ila vitabu nitakuwa navyo. Kwa hivi, tuwasiliane. Anwani yangu ya barua pepe ni info@africonexion.com